Serikali yaeleza sababu kupungua usafirishaji mizigo uwanja wa ndege Mwanza
- Sababu mojawapo ni athari za janga la Corona baada ya baadhi ya nchi kusitisha usafiri wa ndege.
- Yakarabati sehemu ya kupakulia na kupakilia mizigo.
Mwanza. Licha ya kutatua changamoto ya upakuaji wa mizigo katika uwanja wa ndege wa Mwanza, kumeripotiwa upungufu wa shehena ya mizigo ikiwemo minofu ya samaki iliyokuwa ikisafirishwa kwenda barani Ulaya katika miezi miwili iliyopita kutokana na athari za janga la Corona.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Dk Leonard Chamuriho akizungumza hivi karibuni jijini Mwanza amesema ugonjwa wa Corona kwenye baadhi ya nchi za Ulaya umeathiri biashara na safari za ndege.
Amesema kwa muda sasa ndege nyingi hazijatua katika uwanja huo na sababu nyingine ni kuwa nchi ambazo wateja huagiza minofu ya samaki wamesitisha kutoa oda kutokana na ugonjwa wa corona.
Dk Chamuriho amesema kwa sasa ni wateja wachache wanaoagiza mizigo hiyo na husafirishwa kwa kutumia ndege za abiria kupitia viwanja vya Kilimanjaro (KIA) na Julius Nyerere (JNIA).
“Maboresho ya mfumo wa ubebaji wa mizigo katika uwanja huo ni sehemu ya kujiweka tayari kukabiliana na soko la wateja baada ya kurejea tena kwa biashara baina ya Mwanza na mataifa ya Ulaya,” amesema Dk Chamuriho.
Zinazohusiana:
- Airbus yatundika daruga kutengeneza ndege za kifahari za Airbus A380 Superjumbo
- Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
Serikali imetumia zaidi ya Sh300 milioni kutatua changamoto ya ubebaji wa mizigo katika uwanja wa ndege wa Mwanza kwa kutengeneza mfumo rahisi wa uchukuzi ambapo shehena ya mizigo itatelezeshwa kwenye reli maalum kabla ya kupakiwa kwenye ndege au wakati wa kupakuliwa.
Mfumo huo umekuja baada ya kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaotumia uwanja huo kusafirisha minofu ya samaki kwenda barani Ulaya.
Meneja wa Uwanja wa ndege huo, Paschal Kalumbete aliyekua akizungumza hivi karibuni amesema mfumo utapunguza muda wa kupakia na kushusha mizigo na hivyo kulinda usalama wa mizigo hiyo ambayo haihitaji mitikisiko.
“Kabla ya hapo wafanyabiashara walitumia muda wa saa 1:30 kushusha na kupakia tani saba za mizigo kwenye ndege, suala ambalo linalolalamikiwa si wafanyabiashara tu hata watendaji wa ndege,” amesema Kalumbete na kuongeza
“Kama mamlaka ya viwanja vya ndege tukaamua kuja na suruhisho kwa kupata mkandarasi aliyebuni mfumo huu ambao sasa shehana ya tani Saba itashushwa au kupakiwa kwa daki 25 hadi 30.”