Tanzania yazidi kuunadi uwindaji wa kitalii kimataifa

January 21, 2022 11:55 am · Wilson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro (katikati) akiwa pamoja na ujumbe aliombatana nao kutoka Tanzania wakiwa kwenye picha ya pamoja na mmiliki wa Kampuni ya uwindaji wa Kitalii ya Michel Mantheakis Safaris Ltd, Michel Mantheakis (wa tatu kulia) ambaye ni mmiliki wa  vitalu vya uwindaji wa kitalii nchini Tanzania, ikiwa ni miongoni mwa Makampuni nane kutoka Tanzania yaliyoshiriki katika mkutano wa  50 wa mwaka  wa Uwindaji wa Kitalii (Annual Hunting Convention) ulioanza rasmi leo  katika Jiji la  Las Vegas, Nevada nchini Marekani. Picha| Wizara ya Maliasili na Utalii.


  • Makampuni zaidi ya nane kutoka Tanzania kuitangaza nchi kiutalii Marekani.
  • Yashiriki mkutano wa 50 wa mwaka wa uwindaji wa kitalii nchini Marekani.
  • Yavutia wawekezaji katika sekta hiyo na wageni kuja kwa wingi nchini.

Dar Es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro ametoa pongezi kwa makampuni zaidi ya nane ya Tanzania yaliyopo nchini Marekani kwa kazi nzuri ya  kutangaza sekta ya uwindaji wa kitalii  kwa kushiriki katika mkutano wa masuala ya uwindaji wa kitalii.

Mkutano huo wa 50 wa mwaka  wa Uwindaji wa Kitalii (Annual Hunting Convention) ulioandaliwa  na shirika la Safari Club International  (SCI) umeanza  leo  na  unafanyika  katika Jiji la Las  Vegas, Nevada nchini Marekani

Dk Ndumbaro amesema maonyesho hayo yanatoa fursa kwa Tanzania   yakiwemo makampuni, viongozi na maofisa wa Serikali  walioshiriki  mkutano huo  kujifunza na kuinadi Tanzania katika masuala ya uwindaji wa kitalii katika nyanja za kimataifa 

“Katika maonyesho haya zaidi ya makampuni 200 yanayofanya biashara ya windaji wa kitalii kutoka kila kona ya dunia yapo hapa ikiwemo kutoka  bara la Ulaya, Amerika, Afrika, lakini pia nchi za Canada  na Marekani yenyewe,” amesema Dk Ndumbaro.

Amesema pia maonyesho  hayo  yanatoa fursa kwa nchi  kujifunza sekta ya uwindaji wa kitalii kuwa ipo wapi hasa kipindi hiki cha ugonjwa wa Uviko-19. 

“Mimi kama Waziri mwenye dhamana na utalii najisikia fahari kuona makampuni zaidi ya nane ya Kitanzania yapo hapa yakiiuza Tanzania kwenye sekta ya uwindaji wa kitalii. 

“Huu  ni ushahidi tosha  kuwa makampuni hayo yanafanya vizuri, na yanakubalika kimataifa  lakini pia tumechukua fursa hii ya kuweza kukutana nao kwa ujumla wake, mmoja mmoja kuweza kuzungumza nao na kubadilishana mawazo,’’ amesema Ndumbaro.

Amesema mkutano huo pia umewafundisha kuanza kuitazama sekta ya uwindaji wa kitalii kwa namna ya tofauti ili kuiwezesha kuwa na mchango mkubwa katika pato la Taifa.


Soma zaidi:


Mmoja wa wanaoendesha biashara ya utalii wa uwindaji nchini Tanzania ambaye yupo kwenye mkutano huo, Michael Mantheakis amesema kuwa mikutano kama hiyo ni muhimu kuhudhuria kwani inawakutanisha na wageni mbalimbali na bila kuhudhuria unakosa fursa muhimu za wateja. 

“Hapa kuna Washiriki wa kutoka nchi zote za Afrika hivyo  usipohudhuria mkutano huu  utakosa soko. Hapa ndipo  tunapokutana na wageni wetu tunapata faida ya kuweza kuendesha safari zetu, wateja na mawakala wanapata fursa ya kutufanyia usahili na pia wanaona jinsi  tunayonadi bidhaa zetu,” amesema Mantheakis.

Mkutano huo umeanza  rasmi Januari 19, 2022 na kufunguliwa rasmi  Januari 21, 2022 jijini Las Vegas, Nevada nchini Marekani ukiwa na lengo la kuwakutanisha watunga sera na wafanya maamuzi katika ngazi  za juu kutoka nchi  mbalimbali duniani kujadili masuala ya kisera katika kuendeleza sekta ya uwindaji.

Katika mkutano huo, Ndumbaro anazinadi fursa za uwekezaji katika uwindaji wa kitalii zilizopo nchini kwa lengo la kuwawezesha matajiri wakubwa duniani kuchangamkia uwekezaji huo uliopo nchini Tanzania

Kupitia Mkutano huo, Tanzania itaweza kuongeza uelewa zaidi katika masuala ya kisera na maamuzi katika kuendeleza sekta ya uwindaji wa kitalii nchini.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW