Utajiri uliojificha kwenye harusi za kisasa Tanzania

November 9, 2018 1:13 pm · Zahara
Share
Tweet
Copy Link


Mapambo katika sherehe ya harusi huvutia zaidi na kufanya watu wajione wako paradiso ya duniani..Picha| http://www.ritzcarlton.com


  • Wajasiriamali wazitumia kunoa vipaji vyao, kuingiza kipato na kuendeleza familia zao.
  • Harusi ni ishara ya ufahari, kila mtu hutamani kufanya kwa mbembwe ili tu kuwaonyesha watu kuwa amefanya jambo la maana katika jamii.
  • Wadau washauri mitandao ya kijamii itumike kuwaunganisha wajasiriamali na shughuli za harusi.

Dar es Salaam. Kwa wanaoishi katika miji inayokuwa kwa kasi kama Jiji la Dar es Salaam, ni kitu cha kawaida siku ya mwisho wa juma au ‘weekend’ kuona kumbi zikitawaliwa na shughuli mbalimbali ikiwemo sherehe za harusi.

Hiyo ni ishara kuwa idadi ya wanaooa na kuolewa inaongezeka nchini ikiwa ni hatua ya kukamilisha kiapo cha ndoa zinazofungwa katika nyumba za ibada. 

Katika kipindi hiki ambacho dunia inashuhudia mabadiliko makubwa ya teknolojia, harusi ni ishara ya ufahari, kila mtu hutamani kufanya tukio hilo kwa mbwembwe ili tu kuwaonyesha watu kuwa amefanya jambo la maana katika jamii.

Wakati maharusi wakijivunia kufunga harusi za kifahari, kwa wengine hasa wajasiriamali kwao ni fursa ya kuingiza kipato kupitia shughuli mbalimbali zinazoambatana na harusi, jambo linalowafanya waendelee kuishi mjini na kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Shughuli hizo huusisha upambaji wa kumbi au bustani, upishi wa vyakula na keki, usambazaji wa vinywaji, washereheshaji na hata watengenezaji wa kadi za mialiko. Nukta inakuchambulia fursa hizo kwa undani zaidi.

Keki ya harusi ni muhimu kwasababu ni moja ya njia ya kufanya muunganiko wa kifamilia hasa katika kitendo cha kulishana na kupeleka ukweni. Hapo ndipo wajasiriamali wanaweza kufaidika na fursa ya kusambaza keki kulingana na mahitaji ya waagizaji.

“Kwa kawaida keki za harusi kwa Dar es Salaam zinaweza kuuzwa kuanzia Sh300,000 na kuendelea inategemea na aina gani ya keki na idadi zinazohitajika,” anasema Clever Paul muuzaji keki ambaye kwa sasa anaishi Mtwara. 

Paul anakiri kuwa wanakumbana na changamoto ya wahusika kutokulipa kwa wakati bila kujua haichukui siku moja kutengeneza keki kubwa kama za harusi, “Unaweza kukuta mtu anataka keki ya Sh800,000 kwa Sh400,000 au Sh300,000 na hapo ndio huwa mtihani.”

Ukiachana na keki soko lingine ni kuuza vyakula katika sherehe, hapa unachotakiwa ni kuwa na chakula kizuri na kitamu, bei iwe ilingane na aina ya chakula unachopika, hasa ukiwa msafi na mwenye kupika kwa njia iliyo sahihi kwasababu chakula ni sehemu muhimu ya afya ya binadamu. 

Lakini sherehe bila kumbukumbu haijakamilika, hapa ndio fursa ilipolala. Wajanja waliojaaliwa ubunifu wa kupiga picha basi mfuko utatuna wakati wote kutokana na tenda wanazopata.  

“Kupiga picha maharusini kumenisaidia sana ambapo mpaka sasa nimeajiri watu wawili na kuhakikisha kampuni yangu ya kupiga picha imesimama,” anasema Emmanuel Feruzi mmiliki wa kampuni ya kupiga picha ya  K15 Photos.

Hata hivyo, bado kilio chake kikubwa anakielekeza kwa wanaofanya harusi kuwapa muitikio mdogo wapiga picha na kutokuchukulia kama ni moja ya kazi rasmi ya mtu, huku wakisahau ni watu muhimu ambao wanaweka kumbukumbu za kudumu katika maisha.

Anasema wanaoingia kwenye sekta ya picha wasikate tamaa bali waongeze bidii ya kutoa huduma zenye ubora, kuwa na jicho pevu la kuona kila fursa inayokuja mbele yao.   

Pamoja na hayo sherehe ni kupendeza na ili upendeze maharusi wanahitaji kujua nani atawavalisha nguo nzuri. Hapo wabunifu na washonaji wa mavazi wanaingia kujipatia kipato kuendeleza maisha. 

Harusi ni ishara ya ufahari, kila mtu hutamani kufanya kwa mbembwe ili tu kuwaonyesha watu kuwa amefanya jambo la maana katika jamii. Picha| mmpoffice.com

Muonekano wa bibi harusi hasa usoni ni fursa nyingine kwa wajasiriamali waliojikita kwenye sekta ya urembo hasa wapakaji ‘Make up’ wanaweza kuitumia fursa hii kuwatengeneza wanawake katika muonekano tofauti kulingana na rangi za sura zao.  

Msingi mkubwa wa kuwafanyia watu ‘Make up’ ni kujifunza kwa wataalam wa masuala ya urembo, kuwa na vifaa vya kisasa vinavyoendana na ngozi ya mtu. Unatakiwa ujue ni vipi utampendezesha mteja wako kiasi hata akipigwa picha hataonekana kituko na asibadilishe sana mwonekano wa kila siku.


Zinazohusiana: 


Pamoja na maandalizi yote lakini kukamilika kwa sherehe ni kuwa na mshereheshaji ‘MC’ anayeweza kuitambua na kuendana na hadhira yake. 

Godfrey Rugalabamu maarufu kwa jina MC GaraB ameiambia Nukta kuwa ushereheshaji ni shughuli kama shughuli zingine ambayo ikitumiwa vizuri inaendeleza kipaji cha mtu na kumuingizia kipato. 

“Ni fursa ya ajira, kwa mtu kujiongezea kipato na kuwaajiri vijana wengine, mfano mimi nyuma yangu nina watu wa muziki, mpiga picha na anayenishonea suti,” anasema GaraB.

Pamoja na hayo anawasihi vijana wanaopenda kazi hii wafanye kama wao na si kuiga wengine wanafanya nini, hii itawapa nafasi ya kusimama katika soko la wanaosherehesha harusini.

Lakini mafanikio ya sherehe yeyote hutegemea ukumbi au bustani ilivyo ambayo inatakiwa kuwa na huduma ya vyoo vya kisasa, hewa ya kutosha pamoja na steji nzuri ambayo itakuwa rahisi kwenye kuipamba na mwisho kabisa eneo liwe na ulinzi wa kutosha na sehemu nzuri ya kuegeshea magari.

Kazi kwako mjasiriamali unayetaka kuingia kwenye soko la harusi, uchaguzi wa kujitafakari na kujua unachotaka ili kufanikisha hatma ya maisha yako.

Enable Notifications OK No thanks