Acha kuwaza kuwa mfanyabiashara, anza kufanya biashara

Zahara Tunda 0432Hrs   Aprili 23, 2018 Maoni & Uchambuzi
  • Miongoni mwa mambo muhimu ni kuandaa mpango wa biashara ili ukuongoze katika kuiendesha.
  • Ubunifu na kujiamini ni nguzo muhimu zitakazokutoa katika biashara.

“Nani kakuambia eti huwezi kutajirika? Unaweza, tena sana. Lakini kwanza vunja vunja minyororo ya kutojiamini." Hii ni moja ya nukuu maarufu za Mfanyabiashara maarufu nchini Reginand Mengi.

Kupitia kauli hii unaweza  kujifunza kuwa ni vigumu kutajirika kama hutajiamini na kujua unataka kufanya nini na lini na kwa wakati gani? Kwako utajiri utakuwa ni ndoto. 

Biashara imekuwa kimbilio kubwa sana kwa wengi katika kujikwamua kiuchumi.  Hata hivyo, siyo wote wanafanikiwa. Wafanyabiashara wengi na wataalamu wa biashara wameainisha mengi kuhusu ufanyaji biashara lakini ngoja nami nikupe mbinu za kuanzisha biashara. Japo zinaweza zisitatue matatizo yote lakini zinaweza kukupa msingi wa kusimama.

Mosi, chagua wazo la biashara.  Huu ndiyo mtego mkubwa katika biashara. Ukiweza hapa mengine ni rahisi. Maswali ya kujiuliza ni wahitaji au wateja wako ni kina nani? Je, kuna washindani wowote katika utoaji huduma au bidhaa unayotaka kuzalisha? 


Soma habari inayofanana: Mambo ya kuzingatia unapoanzisha 'brand' yako ya biashara


Pili, fanya utafiti wa kutosha kuhusu  biashara yako ujue soko la biashara yako lipoje. Kama ni chakula basi ujue ni wakati gani watu wanahitaji chakula , eneo utakalofanyia biashara, je kuna mkusanyiko wa watu? Na hao watu wa aina gani? Lakini pia inapaswa kumjua mshindani wako.

Uliza wanaofanya biashara kama yako changamoto wanazokumbana nazo. Nenda kwa mpinzani wako angalia jinsi anavyohudumia wateja wake ili upate kujifunza kutoka kwake. Soma katika mitandao mbalimbali kuhusu biashara yako.


Duka kubwa la kisasa la bidhaa za chakula. Ni muhimu kufanya utafiti wa kina ili kubaini fursa na changamoto ya biashara yako. Picha ya Mtandao. 


Vipi kuhusu mtaji? 

Panga jinsi gani utapata mtaji wa kuanzia biashara yako. Hii ifanyike pale utakapokuwa umejitosheleza na utafiti ulioufanya kuhusu hiyo biashara. 

Katika mtaji wa biashara anza na ulichonacho mfukoni. Ni ngumu sana kupata mkopo ukiwa unaanza biashara. Hata ukipata mkopo inapaswa kutumia vizuri kwa sababu kama biashara ikienda ndivyo sivyo unaweza kupoteza biashara yako na kusalia na madeni lukuki yatakayokutesa mbeleni. 

Angalia kama mtaji ulionao utasaidia biashara kujiendeleza kwa mwaka mmoja. Yaani katika kulipa kodi, kulipa wafanyakazi, usafiri na matumizi ya bidhaa.

Mfano wa fedha taslimu. Mtaji ndiyo kila kitu katika baishara. Hata ukiwa mdogo kiasi gani hakikisha unatumia vizuri kwa malengo uliyojiwekea. Picha ya Mtandao. 


Weka mpango wa biashara yako 

Andika mpango wa biashara yako yote kuanzia mwanzo hadi mwisho ili iwe rahisi kama kuna kitu ulikisahau au utahitaji kuendelea kukifuatilia kwa ukaribu zaidi. Weka wazi biashara yako ni nini? Soko lipoje, uongozi na utendaji wake upoje na mwisho kabisa fedha zitakuwa zinatumikaje katika kufanikisha biashara yako.


Fanya biashara kisasa

Malizia kwa kufanya usajili katika mamlaka husika. Tafuta hakimiliki ya biashara yako, fungua leseni ya biashara, lipa vitu vyote ambavyo vinahitajika katika usajili. Hii itachangia sana kufanya biashara yako iwe ya kipekee na kuaminika.

Pia utakuza jina la kampuni au biashara yako kwa sababu watu wengi wanaamini katika biashara iliyosajiliwa na kuwa na nyaraka za usajili. Hii itakuongezea wigo wa kufanya biashara zaidi.

Baada ya kukamilisha yote haya unaweza kuanza biashara yako rasmi. Usisahau jinsi ya kupanua soko lako zaidi tumia mitandao ya kijamii kutangaza biashara yako na kuwa mbunifu ili kujitofautisha na wengine.

Jitahidi kuhakikisha unawafurahisha wateja wako kwani ndio silaha kubwa katika biashara yako.


Related Post