Una mpango wa kuipeleka biashara mtandaoni? Zingatia haya
- Fanya utafiti juu ya mtandao unaokufaa kusimamia biashara yako.
- Zingatia ubora wa bidhaa na mpe thamani kila mteja.
Dar es Salaam. Wakati kasi ya matumizi ya mitandao ya kijamii ikizidi kuongezeka duniani, kampuni zinazotoa huduma hiyo zinabuni teknolojia rahisi kuwafikia watu wengi na kuwafungulia milango wafanyabiashara kuwafikia watu wengi mtandaoni ili kuwauzia bidhaa na huduma.
Kwa Tanzania mitandao ya kijamii inayotumiwa zaidi na wafanyabiashara ni Facebook, Instagram, Twitter pamoja na YouTube ikiwa ni njia ya kutangaza na kuwafikia wateja popote walipo.
Lakini kabla ya kutumia mitandao ya kijamii kibiashara kuna mambo mbalimbali ya kuzingatia ili mikakati na malengo yako yafanikiwe, kwasababu mtandao ni dhana pana yenye watu tofauti wenye mitazamo tofauti kuhusu jamii.
Mambo haya yatakusaidia kutekeleza mkakati wako wa kuuza bidhaa na kujipatia faida;
Kwanza kabisa tengeneza mpango kazi wa kusimamia mitandao ya kijamii ambao utaonyesha bajeti, mitandao utakayotumia, vitu utakavyoweka, muda na jinsi utakasimamia mwenendo wa biashara yako mtandaoni.
Fahamu walengwa wako wakuu wapo katika mtandao gani? Hii itakusaidia jinsi ya kuwapata na kuwafikia. Fanya utafiti kujua aina za watu na vitu wanavyopenda kwa kupitia kurasa, makundi yao kwenye mtandao, itakusaidia kuwapata watu sahihi na kupunguza muda na gharama za kutangaza biashara kwa watu ambao hawana mpango na bidhaa yako.
Mpango kazi wa kusimamia biashara mtandaoni ndiyo nguzo muhimu ya kuimarisha mahusiano na wateja wako. Picha| nsfre.
Unapaswa kujua nani atakayeisimamia ukurasa wako ili uweze kusimamiwa kitaalamu. Unaweza kumuajiri mtu aliyebobea katika masuala ya mitandao ya kijamii ili asimamie ukurasa wako. Chagua mtu sahihi ambaye anaijua vizuri biashara yako kwasababu ana mchanga mkubwa wa kuvuta au kupunguza wateja kununua bidhaa.
Unapaswa kujiuliza utaitumiaje mitandao ya kijamii uliyochagua? Hapa unaweza kuchagua kuitangaza biashara, kuuza au kuelekeza wateja wako juu ya matumizi ya bidhaa yako au vyote kwa pamoja.
Ulinzi wa ukurasa zako za mitandao ya kijamii ni muhimu. Unaweza kuvamiwa na watu wasio na nia njema dhidi ya biashara yako na kukupotezea wateja. Ni muhimu kuhakikisha unaulinda ukurasa wako kwa kuweka neno la siri (nywila ngumu) lisiloweza kutambulika kirahisi na hakikisha unabadilisha mara kwa mara.
Swali la mwisho la kujiuliza umejiandaaje kuimarisha mahusiano na wateja wako katika mitandao ya kijamii? Ukiingia katika mitandao ya kijamii hakikisha unachowapa wateja wako kina ubora na zingatia kuwasaidia kutambua thamani ya bidhaa unayouza.
Hata hivyo, mafanikio ya biashara yoyote ni zaidi ya kuitangaza au kuuza mtandaoni. Muhimu unatakiwa kuwa mwaminifu, zingatia viwango vya ubora wa bidhaa au huduma unayotoa na teknolojia ya uzalishaji.