Seedstars, First Growth Ventures kuwekeza Sh230 bilioni kwenye ‘startups’ za Afrika
Mmoja ya vijana kutoka Ghana akibebwa juu baada ya kushindia tuzo na mtaji kutoka Seedstars. Picha|VC4A.
- Uamuzi huo umetangazwa jana katika mkutano wa kampuni wa Seedstars uliofanyika Uholanzi ambapo unalenga zaidi kuwanufaisha wabunifu na wajasiriamali wa teknolojia.
- Kampuni hizo hazijaweka wazi ni lini wataanza kufanya uwekezaji huo na kampuni zipi zitafaidika na fursa hiyo.
- Wadau nchini wamesema uwekezaji huo utawasaidia vijana kuimarisha na kukuza mitaji ya biashara zao.
Dar es Salaam. Huenda wasariamali wa teknolojia wa Tanzania wakaimarisha na kuendeleza biashara zao, baada ya kampuni ya Seedstars kwa kushirikiana na kampuni ya First Growth Ventures ya nchini Ufaransa kutangaza nia ya kuwekeza Dola za Marekani 100 milioni (Sh230 bilioni) katika kampuni zinazochipukia za Afrika.
Tangazo hilo limetolewa jana (Aprili 4, 2019) na Afisa Uwekezaji wa kampuni hiyo, Charlie Brown katika mkutano wa Seedstars unaofanyika katika kituo cha mikutano cha SwissTech jijini Lausanne, Switzerland..
Brown amesema ni mkakati wao kuhakikisha kila bara ambako kuna ofisi zao wanatoa takribani Dola 100 milioni ili kuzisaidia kampuni zinazochipukia hasa katika teknolojia kupata mtaji wa kuendeleza shughuli zao na kuleta matokeo chanya kwenye jamii.
Uwekezaji huo mkubwa utakuwa wa kwanza kufanywa na Seedstars katika bara la Afrika, licha ya kuwa sio mara ya kwanza kwa kampuni hiyo kuzisaidia kampuni zinazochipukia hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Hata hivyo, kampuni hiyo haijaweka wazi ni lini wataanza kufanya uwekezaji huo na aina ya kampuni ambazo zitafaidika na uwekezaji huo.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
Mwanzilishi wa kampuni hiyo, Alisée de Tonnac amesema tangu kampuni hiyo ianzishwe mwaka 2013 imewekeza mtaji kati ya Dola za Marekani 50,000 na 500,000 (kati ya Sh115 milioni na Sh1.15 trilioni) katika kampuni 40 duniani.
Kampuni nne kati ya 40 zilizowezeshwa mtaji zilianzishwa na Seedstars yenyewe nchini Nigeria zikijikita zaidi katika sekta ya fedha na zingine nne nchini Ivory Coast zikijikita katika matumizi ya teknolojia katika sekta ya elimu.
Seedstars ni kampuni mama ambayo inasimamia kampuni ya uwekezaji na ujasiriamali wa teknolojia ya Seedspace ambayo ina matawi mbalimbali Afrika ikiwemo Tanzania.
Meneja Jamii wa SeedSpace Dar es Salaam, Mohammed Shellimoh ameiambia www.nukta.co.tz kuwa bado hawajapata taarifa rasmi ya uwekezaji huo na kuwa anaona ni fursa muhimu kwa vijana wanaotumia teknolojia kuanzisha kampuni kwasababu itawasaidia kuimarisha na kukuza mitaji ya biashara zao na kuwafikia watu wengi kwenye soko la ushindani.
Licha ya vijana wabunifu wa Tanzania kuchangamkia fursa za kujiajiri na kuwekeza katika teknolojia bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mitaji, kodi kubwa kutoka mamlaka za Serikali na kukosa mipango endelevu ya kukuza biashara zao.