Bosi mpya wa Vodacom kuziwezesha ‘startups’ intaneti ya uhakika

Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Philip Basiimire (aliyevaa tai nyekundu) akiwa pamoja na wafanyakazi wa maabara ya teknolojia ya Smart Lab baada ya kutembelea ofisi zake leo Disemba 14, 2022. Picha | Vodacom Accelerator.
- Amesema ukosefu wa intaneti ni miongoni changamoto zinazorudisha nyuma maendeleo ya kampuni zinazochipukia.
- Vodacom Tanzania itaangalia namna ya kuziwezesha ili zitoe huduma na bidhaa bora sokoni.
- Miongobi mwa mipango mingine ni kuongeza idadi ya wanawake kwenye masuala ya teknolojia.
Dar es Salaam. Mkurugenzi Mtendaji mpya wa kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, Philip Basiimire amesema moja ya mikakati iliyopo kwa sasa ni kuziwezesha kampuni zinazochipukia nchini (Startups) kuunganishwa na intaneti yenye kasi ili kuzirahisha utendaji na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa jamii.
Basiimire, aliyeanza kuitumikia nafasi hiyo Oktoba 15, 2022, amesema kutokuwa na uhakika wa intaneti ni miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo waanzilishi wa startups, hivyo kupunguza kasi yao ya kutoa suluhu za teknolojia zenye matokeo makubwa kwa watu na jamii.
Kabla ya kujiunga na Vodacom, Basiimire alikuwa Mkuu wa masoko, usambazaji na uendeshaji wa kikanda wa kampuni ya MTN ya Afrika Kusini tangu mwaka 2019.
Intaneti, gharama bado tatizo kwa startups
Bosi huyo mpya, aliyekuwa akizungumza leo Disemba 14, 2022 mara baada ya kutembelea maabara ya teknolojia ya Smart Lab iliyopo jijini Dar es Salaam, amesema kampuni yake itaangalia uwezekano kulifanyia kazi suala hilo katika programu zake za kuzisaidia startups nchini.
“Intaneti ni miongoni mwa changamoto nyingi wanazokumbana nazo. Jambo muhimu kwetu ni kuelewa mfumo mzima wa mnyororo wa thamani na kuhakikisha wanaunganishwa kwa intaneti,” amesema Basiimire.
Amesema changamoto nyingine zinazorudisha nyuma maendeleo ya startups za Tanzania ni pamoja na ukosefu wa mitaji, mifumo endelevu ya kibiashara, uelewa mdogo wa sera za kibiashara na kodi.
Hata hivyo, kupunguza changamoto hizo, Vodacom Tanzania na Smart Lab wanaendesha programu maalum ya mafunzo inayojulikana kama “Vodacom Accelerator” ambayo inazisaidia startups zinazochipukia na zinazokua kuendeleza bidhaa na huduma zinazotumia teknolojia kuwa na matokeo makubwa kwenye soko la ushindani.
Programu hiyo ambayo ipo katika awamu ya pili inawawezesha waanzilishi wa startups hizo kupata mafunzo ya kitaalam, ushauri na usaidizi wa kiufundi. Pia, inawawezesha kupata zana za kidijitali na fursa za ufadhili ili kukuza biashara zao zenye faida.
Katika awamu ya kwanza, programu imezifikia startups zinazoendesha shughuli zao katika sekta za fedha, kilimo, elimu, utalii, burudani, afya, biashara mtandao na usalama mtandaoni.
Soma zaidi:
- Mambo muhimu yatakayozisaidia kampuni zinazochipukia Tanzania kukua
- Startups za Tanzania zilizotamba mwaka 2018
- Starups nne Zanzibar zapenya shindano la Seedstars
Mkurugenzi wa Biashara wa Smart Lab, Larry Ayo amesema wanatoa ujuzi na uwezo utakaowasaidia waanzilishi wa startups kujiendesha kibiashara na kukidhi gharama za uendeshaji ikiwemo intaneti.
Ayo amesema wataendelea kushirikiana na Vodacom kuhakikisha wanaongeza idadi ya wabunifu na kampuni zinazotumia teknolojia ili kutatua changamoto za jamii.
Licha ya idadi kubwa ya vijana kuanzisha biashara za kidijitali Tanzania, bado wengi wamekosa msaada wa mafunzo ya usimamizi wa biashara jambo linalofanya wengi washindwe kukua kwa wakati na kutoa huduma bora.
Kuongeza idadi ya wanawake kwenye startups
Bosi huyo amekuwa mteule wa tatu ya kampuni hiyo ndani ya mwaka mmoja, amesema mipango mingine iliyopo ni kuongeza idadi ya wanawake katika teknolojia ili kuifikia jamii kwa upana na kuhakikisha usawa wa kijinsia.
Amesema kupitia program yake ya startups watahimiza wanwake wengi kushiriki katika uanzishaji wa kampuni hizo kutoa mchango wa maendeleo kwenye jamii kupitia teknolojia.
Latest
