Safari bado ndefu kwa wajasiriamali wenye ulemavu Tanzania

November 26, 2021 7:20 am · admin
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni wale ambao biashara zao zimeathirika na Uviko-19.
  • Waanza kuchangamkia mikopo kukuza biashara zao.
  • Serikali yafungua milango kuwasaidia.

Mbeya. Ni katika Mji Mdogo wa Mbalizi mkoani Mbeya, ndipo utakapomkuta mwanaume huyu akiendelea na kazi yake anayofanya kwa mikono. 

Licha ya ulemavu wa viungo alionao, ni mchapakazi aliyejiajiri katika shughuli za kutengeneza viatu ili kujipatia kipato.

Ni Joseph Njole (42) mmiliki wa kiwanda kidogo cha kutengeneza viatu cha Malongo Shoe Markers. 

Njole mwenye mke na watoto watatu anayetegemea biashara hii ya viatu, ni miongoni mwa watu ambao biashara zao ziliathiriwa na janga la Corona tangu lilipoingia Tanzania Machi 2020.

Kutokana na na vikwazo mbalimbali ikiwemo mikusanyiko ya watu, wateja aliokuwa anawategemea walipungua kwa kiasi kikubwa, jambo lililotishia uhai wa biashara yake.

“Corona tangu imeanza imetuathiri pakubwa, ukizingatia kuna kipindi shule zilifunga na wateja wetu wengi ni wanafunzi, tulikosa wateja, mpaka sasa bado hatujaimarika,” anasema Njole ambaye ameajiri watu watatu katika biashara yake.

Licha ya kuwa Serikali imechukua hatua mbalimbali kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo kutoa chanjo, bado biashara ya Njole haijaimarika kwa sababu hapati wateja kama ilivyokuwa zamani.

“Nina mke na watoto watatu, wote wanategemea biashara hii, minada ndiyo tulikuwa tunategemea lakini kwa sasa hatuendi kutokana na uwepo wa Corona, mahitaji ni makubwa lakini tunalazimika kujibana bajeti,” anasema.

Mjasiriamali mwenye ulemavu wa viungo, Joseph Njole akiwa katika eneo la kutengenezea viatu katika ofisi yake iliyopo Mbalizi mkoani Mbeya. Picha| Isakwisa Mbyale.

Malongo Shoe Markers imelazimika kupunguza idadi ya wafanyakazi ili kumudu gharama za uendeshaji kutoka watano mpaka watatu huku changamoto ya soko bado ikiendelea kuwa kitendawili.

“Kwa sasa tuna watengenezaji watatu pekee, na upande wa soko bado linaleta changamoto tunaomba Serikali itoe hamasa katika taasisi zake kama shule na hospitali kutumia bidhaa zetu,” anasisitiza mjasiriamali huyo.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa zaidi ya watu bilioni 1 duniani (asilimia 15) wanaishi na ulemavu, huku nusu ya idadi hiyo ikikumbana na changamoto mbalimbali za huduma za afya na kiuchumi hasa wakati huu wa janga la Corona.

Kutokana na hatari ya janga la Uviko-19, ni muhimu kwa Serikali na jamii kwa ujumla kuchukua hatua mbalimbali za kusaidia kifedha ili waweze kujikinga dhidi ya janga hilo.

Huenda Njole na wajasiriamali wengine wakaimarika siku za hivi karibuni kutokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa duniani kukabiliana na Uviko-19 ikiwemo kutoa chanjo na kulegeza masharti ya usafiri kimataifa.

Moses Mengo ni mmoja wa wafanyabiashara wa viatu kutoka katika eneo hili la Mbalizi anasema ili kumudu gharama za maisha wanalazimika kukopesha bidhaa kwa wateja wao na wakiuza wanawapatia fedha zao.

“Wateja wa moja kwa moja ni wachache, saivi tunaona tu bora umkopeshe mtu ndani ya wiki moja akulipe ili mzigo upungue,” anasema Mengo.

Mikakati ya kuwasaidia walemavu wajasiriamali

Mwenyekiti wa Chama cha Walemavu Mkoa wa Mbeya (CHAWATA), Jimmy Ambilikile anasema biashara za watu wenye ulemavu zimeathirika mara mbili ya watu wa kawaida na jukumu lao kama viongozi ni kuwahamasisha walemavu kujiunga katika vikundi ili kupunguza makali ya athari hizo.

“Kama chama tuna jitahidi kuwahamasisha wadau mbalimbali na watu wenyewe wenye ulemavu kuwa katika vikundi na kupata mkopo wa halmashauri wa asilimia mbili ili kupunguza makali,” anasema Ambilikile.

Ili kupunguza makali ya athari hizo, Serikali nayo inawashauri walemavu ambao ni wajasiriamali kuchangamkia mikopo ya halmashauri itakayowasaidia kupata fedha za kuendesha biashara zao na kuinua mitaji iliyokufa.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Oliva Mgeni  anasema ni kweli athari za Uviko-19 zimejitokeza bayana kwa makundi mbalimbali ikiwemo watu wenye ulemavu, hivyo anashauri kutumia mikopo inayotolewa na halmashauri ili kuimarisha biashara zao.

“Mikopo ya walemavu inatolewa hivyo wanapaswa kufika ofisi za maendeleo ya jamii ili wapatiwe maelekezo ya nini wanapaswa kufanya ili wapatiwe mikopo hiyo na kuamsha biashara zao,” anasema Oliva.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi kutoka hapa jijini Mbeya, Shama Nkembo anasema ni vema watu wakawa na tabia za kujiwekea akiba zitakazowasaidia pindi biashara zinapoenda vibaya.

“Ni vema watu wajenge utamaduni wa kuweka akiba utawasaidia sana wakati wa dharura kama ilivyo katika kipindi hiki cha corona,” anashauri Shama.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW