Hifadhi ya Taifa ya Tarangire: Nyumba ya makundi makubwa ya tembo
- Iko kaskazini mwa Tanzania, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,850, iko umbali wa kilomita 118 Kusini Magharibi mwa jiji la Arusha.
- Tarangire ni maarufu kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo wanaoweza kuonekana katika eneo dogo na mandhari nzuri ya kuvutia yanayotokana na maumbile ya miti ya mibuyu.
Dar es Salaam. Iko kaskazini mwa Tanzania, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,850, umbali wa kilomita 118 Kusini Magharibi mwa jiji la Arusha.
Ni hifadhi ya Taifa ya Tarangire, nyumba ya makundi makubwa ya tembo wenye maumbo makubwa, ikiwa imepambwa na miti mikubwa ya mibuyu yenye kutoa kivuli kwa wanyama hao.
Hivyo ndivyo unavyoweza kuipa sifa hifadhi ya Taifa ya Tarangire inayofikika kirahisi kutokea katika miji ya Arusha na Babati mkoani Manyara.
Ilitangazwa rasmi kuwa hifadhi ya Taifa mwaka 1970 kwa lengo la kuwalinda wanyama hasa faru weusi ambao wako hatarini kutoweka duniani ambapo jina hifadhi hiyo limetokana na wananchi wa kabila la Wambugwe likiwa na maana ya mto wa ngiri ( TARA=MTO na NGIRE=NGIRI).
Historia ya eneo hilo inaeleza kuwa mto huo umeanzia katika milima ya Kondoa mkoani Dodoma na kukatiza katikati ya hifadhi hiyo ambapo humwaga maji yake katika Ziwa Burunge.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Tarangire ni maarufu kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo wanaoweza kuonekana katika eneo dogo na mandhari nzuri ya kuvutia yanayotokana na maumbile ya miti ya mibuyu inayosadikiwa kuwa na umri wa zaidi ya miaka elfu nane.
“Wanyama wa aina nyingi wanaopatikana ndani ya hifadhi hii ni pamoja na pundamilia, nyumbu, swala, simba, nyati, kongoni, chui, duma na wengineo wengi. Aina 550 za ndege hupatikana ndani ya hifadhi hii pia,” inasomeka sehemu ya taarifa ya TTB kuhusu hifadhi hiyo.
Iko kaskazini mwa Tanzania, yenye ukubwa wa kilomita za mraba 2,850, umbali wa kilomita 118 Kusini Magharibi mwa jiji la Arusha. Picha|Tanapa.
Hifadhi hii ni maarufu katika ukanda wa kaskazini mwa Tanzania ikiungana na hifadhi nyingine za Arusha, Mnyara, Mkomazi na Mlima Kilimanjaro kutokana na wageni wengi wanaopenda kutembelea hifadhi hiyo.
Umaarufu mwingine wa hifadhi hiyo ambayo awali ilikuwa pori la akiba ni pamoja na aina ya chatu walio na uwezo wa kukwea miti.
Zinazohusiana:
- Saadani: Mahali unapoweza kuwaona simba, twiga wakila upepo wa ‘beach’
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii.
- Prince William atua Tanzania kuendeleza mapambano dhidi ya ujangiri wanyamapori
- Tamasha la ‘Urithi Festival’ kufanyika mikoani kila mwaka
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inaeleza kuwa unaweza kutembelea hifadhi hii wakati wote wa mwaka na kuwaona wanyama wote bila matatizo kutokana na mazingira mazuri ya hifadhi yanayosaidiwa na mto Tarangire unaokatiza katikati ya hifadhi.
Kutokana na umaarufu wa hifadhi hii idadi ya Watanzania wanaotembelea hifadhi hii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Ndani ya hifadhi kuna nyumba za kulala wageni Hoteli za kitalii, maeneo ya kupiga mahema na kambi maalum kwa ajili ya watalii wanaotembelea hifadhi hii. Malazi yanaweza kupatikana nje ya hifadhi ambako pia kuna hoteli na nyumba za kulala wageni.
Hifadhi hiyo imekuwa ikipokea wageni wa kimataifa ambao huvutiwa zaidi na makundi ya tembo pamoja na eneo kubwa la hifadhi ambao linatoa fursa ya kupiga kambi.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Mwanamitindo na muigizaji maarufu Marekani aliyewahi kung’ara katika taji la Miss Universe, Marisela De Montecristo alifanya utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Tarangire, jambo lililoitangaza zaidi hifadhi hiyo kimataifa.
Mwanamitindo na muigizaji maarufu Marekani aliyewahi kung’ara katika taji la Miss Universe, Marisela De Montecristo akivalishwa mavazi ya asili ya kimasai alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Tarangire na kupokelewa na Mkuu wa Idara ya Utalii katika Hifadhi hiyo.
Latest