Serikali yafuatilia kuzuiwa kwa ndege ya Air Tanzania nchini Afrika Kusini
- Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliyokuwa inatoka Afrika Kusini kwenda jijini Dar es Salaam imezuiliwa kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg.
- Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu inafuatilia suala hilo ili ndege hiyo iendelea kutoa huduma kama kawaida.
Dar es Salaam. Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano imesema inafuatilia taarifa za kuzuiliwa kuruka kwa ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) iliyokuwa inatoka Afrika Kusini kwenda jijini Dar es Salaam, kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg ili ndege hiyo iachiwe na kuendelea na safari zake.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Serikali imezipokea kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, ndege hiyo ambayo ilitakiwa kuruka jana (Agosti 23, 2019) kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wa Johannesburg imezuiliwa kwa amri ya mahakama hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Leonard Chamuriho inaeleza kuwa Serikali kupitia Mwanasheria Mkuu inafuatilia suala hilo ili ndege hiyo iendelea kutoa huduma kama kawaida.
Aidha, wizara imewaomba radhi wasafiri wote waliotakiwa kusafiri jana kuja Dar es Salaam kwa usumbufu wowote uliojitokeza na kwamba inalifanyia kazi suala hilo.
Hata hivyo, Serikali haijaeleza sababu za kuzuiliwa kwa ndege hiyo ambayo imekua ikifanya safari za Afrika Kusini kila wiki.
Soma zaidi:
- Waziri azungumzia ndege za ATCL kuchelewa, kuahirisha safari
- Shirika la ndege la Ethiopia limesitisha safari zote za ndege aina ya Boeing 737
- ATCL inavyojitanua kimataifa
ATCL ilizindua safari zake rasmi za kwenda Afrika Kusini Juni 28 mwaka huu kwa ndege aina ya Airbus 220-300 kutua katika jiji la Johannesburg ikiwa ni mkakati wa kujitanua kimataifa kwa huduma za ndege.
Wiki mbili baadaye ATCL ikazindua safari za kwenda Mumbai nchini India ili kuongeza ushindani na shirika la ndege la Ethiopia (Ethiopian Airlines) ambalo linatoa huduma za ndege katika miji zaidi ya mitatu ya nchi hiyo.
Kwa sasa ATCL pia inafanya safari za anga katika nchi nne za Burundi, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
ATCL Ilikuwa na ndege moja aina ya Bombardier DASH8 Q300 ambayo ilikuwa ikihudumu tangu 2011 kabla ya Serikali kuanza mkakati wa kulifufua shirika hilo lililoanzishwa mwaka 1977.
Kwa sasa Serikali imenunua ndege saba; Bombardier DASH8 Q400 tatu, mbili ambazo zilifika Tanzania Septemba 2016 na moja Juni 2017; Airbus mbili na Boeing 787 Dreamliner ambazo zilitua Tanzania kati ya Mei na Julai 2018. Hata hivyo, Serikali imesema ndege nyingine moja itawasili Tanzania mwishoni mwa mwaka huu.
Latest