Ndege nyingine yaanguka, yaua wawili Tanzania
Dar es Salaam. Ndege ya Kampuni ya Auric Air imeanguka leo asubuhi katika uwanja mdogo wa ndege Seronera uliopo katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Ajali hiyo imetokea leo (Septemba 23, 2019) majira ya 1:30 asubuhi ambapo watu wawili wamepoteza maisha akiwemo rubani mmoja na abiria mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Mamlaka ya hifadhi za Taifa (Tanapa), rubani na abiria wote ni raia wa Tanzania na kueleza kuwa taarifa kuhusu ajali hiyo zitatolewa baadaye.
Ndege ya Kampuni ya Auric Air imeanguka leo asubuhi katika uwanja mdogo wa ndege Seronera, Serengeti. Rubani mmoja na abiria mmoja wamepoteza maisha. Taarifa zaidi zitatolewa.
— Tanzania Parks (@tzparks) September 23, 2019
Hii ni ndege ya tatu kuanguka na kusababisha vifo na majeruhi ndani ya kipindi cha miezi mitatu ambapo nyingine ilitokea mkoani Tabora na kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.
Agosti 6, 2019, ndege ndogo ya abiria (5H-NOW) ya kampuni ya Tropical iliyokuwa inatokea katika kisiwa cha Mafia kuja jijini Dar es Salaam ilianguka na kuwaka moto maeneo ya Mafia, ambapo watu tisa walinusurika kifo.
Pia Agosti 3 mwaka huu, ndege ya usaidizi ya mradi wa wanafunzi wa Afrika Kusini ya U-Dream ilianguka dakika moja baada ya kupaa angani kutoka katika uwanja wa ndege uliopo kijiji cha Igigwa Wilayani Sikonge mkoani Tabora magharibi mwa Tanzania.
Ndege hiyo ilikuwa inaendeshwa na raia wa Afrika Kusini, Des Werner na Wener Froneman kutoka Cape Town kuelekea Cairo Misri ambapo wote wawili walipoteza maisha.
Latest