Hatma walioomba mikopo Heslb kujulikana Oktoba 15
- Itatoa orodha ya majina ya waombaji waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020, Jumanne Oktoba 15, 2019.
- Yasema imepokea jumla ya maombi 87,747.
- Yaongeza muda wa siku sita zaidi kwa waombaji wenye mapungufu kurekebisha taarifa zao.
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema itatoa orodha ya majina ya waombaji waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020, Jumanne Oktoba 15, 2019 baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa maombi yaliyowasilishwa.
Heslb imesema imepokea jumla ya maombi 87,747 ambapo kati ya maombi hayo, ni maombi 82,043 sawa na asilimia 93.4 yalikuwa yamekidhi vigezo vya maombi.
Gazeti la Serikali la Daily News limemnukuu Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru kuwa idadi ya maombi yaliyokamilika ya mwaka huu imeongezeka ukilinganisha na mwaka jana ambapo yalikuwa maombi 81,425.
Badru amethibitisha kuwa hadi sasa bodi hiyo imepokea Sh125 bilioni kutoka kwa Serikali ikiwa ni pesa ya kukamilisha malipo ya robo ya kwanza ya utoaji wa mikopo hiyo.
Katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali imetenga Sh450 bilioni kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu, ikiwa imeongezeka kutoka Sh427 bilioni zilizotengwa mwaka uliopita.
Zinazohusiana
- Waombaji 10,452 Heslb wapewa siku nne kurekebisha kasoro
- Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu 2019-2020
- Wanafunzi zaidi ya 2,400 wa elimu ya juu wanufaika na mikopo ya HESLB
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha ameiomba bodi hiyo kuwasaidia waombaji ambao maombi yao hayajakamilika kwa sababu wapo baadhi wanakabiliwa na changamoto zao teknolojia, licha kuwa wana vigezo vyote vya kupata mikopo.
Kutokana na changamoto hizo, jana bodi hiyo imetoa muda wa hadi Oktoba 15 kwa waombaji ambao fomu zao zina mapungufu, kurekebisha kabla hawajatangaza orodha ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo.
Septemba 29, 2019, bodi hiyo ilitoa muda wa kuanzia Septemba 30 hadi Oktoba 4, 2019 kwa waombaji wenye mapungufu kurekebisha taarifa zao ili Oktoba 6, 2019 itangaze orodha ya waombaji waliofanikiwa kupata mikopo mwaka huu.
Naibu Waziri huyo aliyekuwa akizungumza jana alipotembelea ofisi za Heslb, ameitaka bodi hiyo kuhakikisha fedha hizo zinawafikia wanafunzi kwa wakati kwa sababu tayari Serikali imetoa fedha za awamu ya kwanza.