“Buku” ilivyonihamasisha kufanya biashara ya juisi
- Ni ngumu kuamini lakini kijana ambaye sina historia ya kufanya biashara niliweza kuitumia pesa hiyo kwa kujiongezea kipato.
- Sikusubiri niwe na pesa nyingi ninunue blenda na vifungashio, nilitumia rasilimali zilizokuwepo.
- Tabasamu, kupenda nilichokifanya na kusikiliza maoni ya wateja, kiliifanya biashara yangu ifanikiwe.
Dar es Salaam. Watu wengi husubiri kupata mtaji mkubwa na kuwa na kila kitu ili kuanzisha biashara ya kujiongezea kipato.
Wengi wakiwaza maelfu na mamilioni ya fedha lakini hivi ndivyo Sh1,000 maarufu kama “buku” ilivyochochea kufanya biashara yangu ya ziada ya kutengeneza juisi (sharubati).
Ndiyo! sijakosea, siyo Sh10,000, sio Sh100,000 na wala siyo Sh1 milioni. Ni buku.
Tuanzie hapa. Ni kawaida yangu kupita kwa jamaa yangu Uwezo Paskali ambaye ni muuza matunda karibu na nyumbani Boko Basiaya jijini Dar es Salaam.
Nikifika hapa huwa najinunulia maembe, ndizi au makakara almaarufu kama “Passion” kwa ajili ya kujitengenezea juisi kwa matumizi binafsi.
Kila siku, Paskali hujinyakulia Sh1,000 kutoka kwangu.
Buku hiyo hunipatia juisi chupa mbili ambayo moja huwa naitumia asubuhi na nyingine, huburudisha kinywa changu mchana kwa kuwa mara nyingi napenda kutumia chakula ninachokiamini ninapokuwa kazini.
Ningeweza kununua kinywaji hicho karibu na eneo langu la kazi lakini sipendi kutumia kilichotengenezwa na mtu nisiyemjua japo katika pilikapilika za maisha yetu tunakula au kunywa vinywaji vilivyotengenezwa na watu wengine.
Hali hiyo husababishwa na hofu juu ya maji na ubora wa matunda yaliyotumika, usafi na hata muda iliyokaa tangu kutengenezwa.
Nina historia mbaya na juisi hizo lakini hiyo ni simulizi ya siku nyingine. Hata hivyo, hii inaweza kuwa changamoto kwa sisi watoa huduma kuboresha mazingira yetu ya kuandaa chakula na vinywaji.
Nilikuwa nikiziuza juisi hizo kwa Sh1000 na kila siku ndani ya wiki, zilikuwa na ladha tofauti. Picha| Rodgers George.
Mazoea yalivyoanza kuwa biashara
“Ninaomba uanze kunitengenezea na mimi,” aliniambia mfanyakazi mwenzangu na rafiki yangu wa muda mrefu, Tulinagwe Malopa baada ya kuonja karibu kila juisi niliyotengeneza. Nilimuambia, atachangia buku tu kila siku.
Unaweza kusema pesa hiyo ni ndogo lakini kwangu sikuihesabu kama pesa ya kujipatia faida. Sikutoa tena pesa ya kununua matunda kutoka mfukoni kwangu bali, ilitoka kwenye pochi ya Tulinagwe.
Hata hivyo, mbali na buku, zipo gharama zingine ambazo zinaweza zisionekane zikiwemo Blenda ya kutengenezea juisi, umeme pamoja na maji ambayo kwa kuwa mimi ninaishi nyumbani, gharama hizo zililipwa na shangazi yangu.
Mlezi huyo alifanya biashara yangu kuwa mtelezo kwani baadhi ya siku, hata matunda nayo alininunulia bila kusahau hamasa ya pale nilipotaka kukata tamaa.
Kifungashio kilivyovutia wateja zaidi
Mara kadhaa, wateja wangu walitoka nje ya ofisi na chupa zangu za juisi na hapo baadhi yao waliuliza wapi walipozipata. Walionyeshwa kwangu na hiyo ilisababisha idadi ya watu waliogonga kwenye mlango wa ofisi yetu kuongezeka.
“Juisi zipo?” waliuliza kila mara “hapana, ninaleta kwa oda tu,” nilijibu, baadaye waliniambia niwaletee na nilifanya hivyo. Idadi ilizidi kiasi cha kujiuliza ni vipi ningeweza “kubalance” muda wa kazi na kuhudumia wateja wangu wa juisi kama wangeongezeka kwa kasi.
Lakini niliweza kulimudu hili kwasababu nilikuwa nasambaza juisi muda wa mapumziko au kabla sijaanza kufanya kazi za ofisini.
Ilikuwa ndani ya wiki tatu, nilipata wateja wa kila siku zaidi ya 10 ambao wote walianza kwa “Niletee kesho nionje,” hawakuonja bure.
Zinazohusiana
- Unawezaje kuishi na kila mtu kwenye makazi mapya?
- Hivi ndivyo ninavyotabasamu kwa kila kazi ninayofanya
- Hii ndiyo zawadi unayoweza kumpatia mama yako
Binti Malopa alivyonifungulia dunia
Baada ya Tulinagwe kunywa juisi yangu kwa wiki, wafanyakazi wenzetu ofisini walianza kumuuliza ni wapi anapata wapi? Naye bila kujibu lolote, alinyoosha kidole kwangu huku akinywa juisi yake muda huo.
“Niletee kesho” alisema bosi wangu. “Na mimi pia” alisema mmoja kati ya wafanyakazi wangu.
Usiku huo, nilinunua machungwa ya Sh1,500 na rafiki yangu Paskali aliniongeza chungwa moja na hivyo kufanya idadi yangu ya machungwa kuwa nane.
Sikuwaza pia kuhusu vibebeo kwani mara kadhaa nilinunua juisi za “Fresh Garden” ambazo zilinivutia chupa yake ambazo sikuzitupa na badala yake nilizihifadhi nyumbani nikiwa na malengo ya kuzitafutia kitu cha kufanya.
Hatimaye kazi yake iliwadia kwani nilizitumia kuweka juisi kwa wateja wangu. Sikuwa na mawazo juu ya kununua glasi.
Kwa kipindi hicho chote, nilikuwa najaribu kubuni na kuibuka na ladha za matunda mbalimbali. Picha| Rodgers George.
Kiungo cha siri katika biashara yangu
Siyo kwamba kila siku nilitengeneza kitu “kizuri” hapana!, kuna siku, maji yalizidi, matunda yalikuwa machachu na wakati mwingine, kutengeneza juisi ya tunda ambalo halikupendwa.
Hata hivyo, nilikuwa naongea na wateja wangu kuwauliza wangependa nini, matunda wayapendayo na nashukuru wengi hawakupenda kuwekewa sukari kwenye juisi zao hivyo sukari haikuwa gharama na pale ilipobidi, shangazi yangu alinibariki na sukari ya nyumbani.
Kilichonisaidia kufanikiwa ni tabasamu langu lililotokea na kufanya kazi ambayo niliipenda na mahaba nayo yalizidi kukua pale wateja wangu walipokuwa wakifarijika na kinywaji chao cha kila siku.
Usikose muendelezo wa simulizi hii kufahamu safari yangu ilikuwaje hadi kupata Sh8,000 kwa siku sawa na Sh160,000 au zaidi kwa mwezi kama faida ya kazi inayohitaji kuamka mapema na kubeba jagi la lita tano kwenye begi.
Latest