Nguo, nyama vyachangia kupandisha mfumuko wa bei Tanzania
- Umeongezeka kidogo katika mwaka ulioshia Desemba 2020 hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3 iliyorekodiwa Novemba mwaka jana.
- Umechangiwa na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Mfumuko wa bei wa Taifa umeongezeka kidogo katika mwaka ulioshia Desemba 2020 hadi asilimia 3.2 kutoka asilimia 3 iliyorekodiwa Novemba mwaka jana, ikichangiwa zaidi na kupaa kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
“Hii inaamanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka Desemba 2020 imeongezeka kidogo ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Novemba 2020,” inasomeka sehemu ya taarifa ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo Januari 8, 2021.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa mfumuko huo wa bei unatokana na kuongezeka kwa kwa baadhi ya bei za bidhaa za vyakula na zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Desemba 2020 ikilinganishwa na kile kilichoishia Desemba 2019.
Zinazohusiana:
- Mfuko wa bei washuka kwa mara ya tatu mfululizo Tanzania
- Ijue mikoa kumi inayoongoza kwa mbuzi wengi Tanzania
Bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei katika kipindi hicho ni nyama kwa asilimia 3.1, samaki (asilimia 15.6), mayai (asilimia 3), dagaa (asilimia 13.2), matunda (asilimia 13.9), maharage (asilimia 6.2), choroko (asilimia 12), viazi mviringo (asilimia 5.5), mihogo (asilimia 13.5) na mafuta ya kupikia kwa asilimia tisa.
“Mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Desemba 2020 umeongezeka hadi asilimia 3 kutoka asilimia 2.8 mwaka ulioishia mwezi Novemba, 2020,” inaeleza taarifa hiyo.
Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko huo wa bei ni nguo za wanaume kwa asilimia 3.9, nguo za wanawake (asilimia 3.3), viatu vya wanaume (asilimia 2.5), viatu vya wanawake (asilimia 2), gesi ya kupikia (asilimia 7.1) na mkaa kwa asilimia 12.3.