Dk Mpango apendekezwa kuwa Makamu wa Rais Tanzania
- Rais Samia Suluhu Hassan amependekeza jina la Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amempendekeza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania.
Taarifa ya kupendekezwa na kwa Dk Mpango ambaye kitaaluma ni mchumi imetolewa leo Machi 30, 2021 Bungeni jijini Dodona Spika Job Ndugai baada ya kumalizika kipindi cha maswali na majibu.
“Mheshimiwa Rais kwa Mamlaka aliyopewa na Katiba chini ya Ibara ya 35 (5) amempendekeza Dk Philip Mpango kuwa Makamu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Ndugai na baadaye kufuatiwa na nderemo na vifijo kutoka kwa Wabunge.
Tangazo hilo lilikuwa linasubiriwa kwa hamu tangu kufariki kwa Hayati Rais Magufuli ambaye nafasi yake imechukuliwa na Rais Samia.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema taratibu za awali za kutangazwa jina la mteuliwa imekamilika na hatua inayofuata ni jina kupitishwa na Bunge kwa zaidi ya asilimia 50.
“Utaratibu ambao tunaweza kuutumia kama ambao umedokeza kwa uzoefu ambao ulijitokeza wakati wa kifo cha Makamu wa Rais Mheshimiwa Omari Juma tunaweza kuufuata utaratibu ule,” amesema Majaliwa.
Soma zaidi:
- Dk Mpango: Uchumi wa Tanzania kukua kwa asilimia 4 mwaka 2020
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
Dk Mpango azungumza
Baada ya utaratibu wa kuthibitisha jina la Dk Mpango, alipewa nafasi ya kuongea mbele ya Bunge ambapo amesema “ni heshima kubwa sana na sikuwahi kuota” huku akiweka wazi kuwa uteuzi huo umemwacha akiwa amepigwa na butwaa.
Amemshukuru Rais Samia kwa kupendekeza jina lake na kuwa msaidizi wa karibu katika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi.
“Napenda kumshukuru sana Mheshimiwa mama yetu Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu kwa kupendekeza jia langu na kuridhiwa na chama chetu Mapinduzi ili liweze kuletwa hapa kwa ajili ya kuthibitishwa na Bunge,” amesema Dk Mpango ambaye alikuwa Waziri wa Fedha na Mipango tangu Rais Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015.
Amesema endapo bunge litamthibitisha katika nafasi aliyopendekezwa atafanya kazi kwa bidii kwa kusimamia rasilimali za nchi na kuibadilisha Tanzania na kuhakikisha viongozi wa umma wanaishi maadili ya uongozi.
“Nimesema mara kadhaa humu ndani ningependa sana tutoke sasa kuwa low middle income country(nchi ya uchumi wa kati wa chini) twende kuwa a high income country(nchi ya uchumi wa juu) katika kipindi kifupi na inawezekana kwa pamoja tukiamua kama Watanzania,” amesema Dk Mpango akielezea matamanio yake ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania.
Huku akishangilia mara kwa mara na Wabunge, amesema yeye ni mtoto wa masikini na kama kiatu cha umasikini anakijua kinavyouma hivyo endapo bunge litamthibitisha ameahidi kuendelea kusimamia haki za Watanzania na kufanya kazi na viongozi wengine kwa uwezo wake wote.
Ikiwa Wabunge watapisha jina la Dk Mpango kwa asilimia 50 basi atathibitishwa kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania na atafanya kazi kwa karibu na Mama Samia ambaye ni Rais wa sita wa Taifa hilo la Afrika Mashariki.
Kufahamu kwa undani kuhusu mchakato wa Bunge kumthibitisha Dk Mpango unaoendelea leo katika kikao cha mhimili huo, tazama hapa mubashara.