CAG alivyobaini ‘matundu’ mfumo wa Tehama wizara ya maliasili na utalii
- Abaini mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa Wizara ya Maliasili na Utalii unakabiliwa na changamoto mbalimbali za tehama zinazochangia Serikali kukosa mapato.
- Changamoto hizo zimejitokeza katka utoaji wa vibali na usimamizi wa wageni wanaoingia mbugani.
Dar es Salaam. Wakati joto la mjadala wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Charles Kichere kwa mwaka 2019/20 likiwa bado halijapoa, imebainika kuwa mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa Wizara ya Maliasili na Utalii unakabiliwa na changamoto mbalimbali za tehama zinazochangia kuvujisha mapato ya Serikali.
Wizara hiyo imekuwa gumzo katika mitandao ya kijamii tangu wiki iliyopita baada ripoti ya CAG ikubainisha masuala mbalimbali ya matumizi mabaya ya fedha za umma ndani ya wizara hiyo iliyokuwa inaongozwa na Dk Hamisi Kigwangalla.
Dk Kigwangalla alikuwa waziri katika wizara hiyo kuanzia Oktoba 7, 2017 hadi Novemba 2020 katika utawala wa Hayati Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu kwa maradhi ya moyo.
Baadhi ya mambo yaliyozua mjadala hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii kuhusu wizara hiyo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Mfuko wa Tozo za Maendeleo ya Utalii zilichangia Sh1,56 bilioni kufadhili Tamasha la Urithi bila ya kuwapo kwenye bajeti zao.
CAG Kichere alisema Septemba 28, 2019, Dk Kigwangalla ambaye ni Mbunge wa Nzega Vijijini alizindua tamasha aliloliita `Kingwangalla Kili Challenge’ ambalo lililenga kuhamasisha watu kupanda Mlima Kilimanjaro.
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Tanzania yaangazi masoko 18 kukuza utalii duniani
CAG mengine kwenye wizara hiyo
Licha ya ubadhirifu huo uliofanywa na watendaji wa wizara, CAG amebaini kuwa mfumo wa ukusanyaji mapato wa wizara hiyo MNRT Portal una mapungufu mbalimbali ambayo yanatoa mianya ya kupotea kwa mapato ya Serikali katika sekta ya utalii.
CAG amesema vibali vya wageni kuingia katika hifadhi za Taifa vinatolewa na waendeshaji wa utalii kupitia mfumo huo na malipo hufanywa kwa njia ya kielektroniki kupitia mfumo wa malipo serikalini (GePG).
Amesema kutokuwepo kwa lango la kuingia na lango la kutoka ndani ya hifadhi au vivutio vilivyo chini ya Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania(TAWA) na kutowasilisha vibali wakati wa kuingia au kutoka nje ya hifadhi kumesababisha vibali kuonekana havijatumika wakati tayari vimetumika (paid but unutilized).
“Hali hii imesababisha kushindwa kukusanya mapato kwa watalii waliokaa mbugani zaidi ya muda waliolipia,” amesema CAG, Kichere katika ripoti hiyo.
Mapungufu hayo yalibainika kwa kuangalia vibali vilivyotolewa kwa watalii mbalimbali kati ya Januari 1, 2020 na Septemba 29, 2020.
Mathalan, vibali 223 vilivyotolewa kwa watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere vilionyesha kuwa vimekwishalipiwa na havijatumika bado, wakati vibali vingi kati ya hivyo vilikuwa vimeshatumika ingawa kwa sababu havikuwekewa alama wakati watalii wanaingia na kutoka.
“Kwa hivyo inasababisha uwezekanano wa upoteaji wa mapato ikiwa mgeni atakaa zaidi ya muda aliolipia. Vivyo hivyo, kutengeneza mwanya wa kutumiwa tena kwa vibali bila malipo,” ameeleza CAG.
Wizara ya Maliasili na Utalii ndiyo yenye jukumu la kusimamia mbuga za wanyama ambazo zimekuwa kivutio kikubwa cha watalii nchini. Picha|World Nomads.
Aidha, amebaini kuwa vibali 12 vyenye kiasi cha malipo ya sifuri ambayo inamaanisha kuwa wageni wenye vibali hivi walitumia huduma bure huku vibali 432 vyenye tarehe ya maombi ya kibali ya mbele kuliko tarehe ya kuingia ambayo inamaanisha kuwa vibali viliundwa baada ya huduma kutolewa.
“Vibali vya siku 14 vina tofauti kati ya tarehe ya kuingia na tarehe ya kutoka kwa zaidi ya siku 1 ambayo inamaanisha udhaifu wa udhibiti wa mfumo kuhakikisha aina ya uingiaji iliyochaguliwa inaendana na idadi ya siku husika,” amesema Kichere.
Pia amebaini katika mfumo huo, jozi 21 za maombi zinatumia namba moja ya kibali wakati kila ombi la kibali linatakiwa kuwa na nambari ya kipekee ya kibali inayohusishwa na kiwango chake kilicholipwa.
Amesema ikiwa maombi mawili yanatumia namba moja ya kibali inaweza kumaanisha kibali kimoja kilitolewa bila malipo.
CAG katika ripoti hiyo anaeleza kuwa udhaifu huo unasababishwa na kutozingatia mahitaji muhimu ya udhibiti wakati wa kukusanya mahitaji ambayo mfumo unatakiwa ufanye na utoaji wa taarifa za mapato zisizo sahihi.
Kutokana na mapungufu hayo CAG amependekeza kuboresha mfumo wa ‘MNRT portal’ kuhakikisha aina ya uingiaji (entry type) inayochaguliwa inaendana na idadi ya siku kati ya tarehe ya kuingia na tarehe ya kutoka.
“Kuzuia wasimamizi wa mfumo kutekeleza majukumu mengi hasa yaliyo nje ya majukumu wanayopaswa kufanya kama vile kuunda vibali,” amesema.
Latest
