CAG aibua mapya bodi ya utalii Tanzania

April 14, 2023 8:53 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Abaini kuchelewa kuanza kazi kwa kituo cha kutangaza utalii kidijitali.
  • Bodi hiyo inatumia kanuni za fedha zilizopitwa na wakati.
  • TTB ilifanya manunuzi nje ya mfumo wa manunuzi wa Serikali. 

Dar es Salaam. Licha ya Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa kiungo muhimu cha ukuaji wa utalii nchini, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema bodi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo matumizi yasiyoridhisha ya fedha, hali inayoweza kurudisha nyuma sekta ya utalii nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG kuhusu Mashirika ya Umma ya mwaka 2021/22 iliyotolewa hivi karibu imebaini mapungufu mbalimbali ya utendaji na usimamizi wa rasilimali za bodi hiyo, jambo ambalo likiachwa linaweza kuathiri kwa sehemu kubwa shughuli za utalii nchini.

Miongoni mwa mapungufu yaliyoibuliwa na CAG Charles Kichere katika ripoti hiyo ni kuchelewa kuanza kufanya kazi kwa kituo cha kidijitali cha TTB kwa ajili ya kutangaza utalii.

Kituo hicho kilianza kujengwa mwaka 2017/18 na kukikamilisha Aprili 2022 kwa gharama ya Sh1.06 bilioni 1.06.

“Hata hivyo, hadi kufikia wakati wa ukaguzi wangu mwezi Desemba 2022, kituo hicho kilikuwa hakijafunguliwa ili kuanza kufanya kazi huku ikiwa ni muda wa miezi nane tangu kukamilika kwake, kwa sababu ya ukosefu wa wafanyakazi tisa wanaohitajika wenye ujuzi na weledi unaohitajika kwa ajili ya kukiendesha kituo hicho,” imeeleza ripoti hiyo.

Licha ya TTB kuomba kibali cha kuajiri kutoka Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Juni 9, 2022, hata hivyo kibali hicho kilikuwa hakijatolewa hadi wakati wa ukaguzi ambacho ni kipindi cha miezi sita tangu kibali kuombwa. 

Lengo kuu la Kituo hicho ni kupanua wigo wa kutangaza vivutio na utalii wa Tanzania kwa njia ya kisasa zaidi ya kidijitali kwa kuviweka vivutio vya utalii vya Tanzania katika kiwango cha kimataifa ili kuzidi kujulikana kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii. 

Ndani ya mtumbwi ukiwa juu ya maji tulivu yaliyopo kwenye msitu wa Mgoroto mkoani Tanga, ni kiburudisho kingine cha kukuongea ihai wa kuishi. Picha| K15 Photos.

Manufaa na matarajio mengine yanayotarajiwa kutoka kwenye kituo hicho hayajapatikana kwa wakati kufuatia kuchelewa kufunguliwa kwa kituo hicho. 

“Hii ni pamoja na kuchelewa kwa utangazaji wa vivutio vya utalii vya Tanzania kulikotarajiwa kuongeza idadi ya watalii watokanao na matangazo ya kituo hicho. Ninapendekeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kuidhinisha kibali cha kuajiri watumishi wa kituo hicho ili kiweze kuanza kazi ya kutangaza utalii kidijitali,” ameeleza CAG Kichere katika ripoti hiyo. 

Serikali ya Tanzania inalenga kuongeza mchango wa utalii katika kuchangia pato la Taifa kutoka asilimia 6 hadi 11 ifikapo mwaka 2025. Lengo ni kuvutia watalii milioni 5 na kuingiza mapato ya Dola za Marekani bilioni 6 (Sh14.1 trilioni) kila mwaka. 


Kutangaza utalii bado bado

Mwaka 2021/22 Bodi ilitekeleza kazi 32 (asimia 68) kati ya 47 za masoko ilizopanga kutekeleza lakini CAG amebaini kuwa  kazi 15 ambazo hazikutekelezwa ni miongoni mwa kazi muhimu zinazohusiana na utangazaji wa utalii kama vile kuandaa na kushiriki katika maonyesho ya utalii nchini Korea Kusini, Hong Kong, Thailand na China hadi Juni 2022. 

Pia amebaini kuwa bajeti ya Sh1.98 bilioni iliyopangwa kwa kazi 15 za masoko hayo ilitumika kusaidia kufanikisha Maonesho ya Utalii ya Kanda ya Afrika Mashariki ambayo hayakuwa kwenye mpango. 

“Ninapendekeza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii katika siku zijazo endapo kutakuwa na matukio ambayo hayajapangwa, itafute fedha kutoka Hazina kwa ajili ya kugharamia matukio hayo bila kuathiri kazi zilizopangwa za Bodi ya Utalii,” imeeleza ripoti ya CAG.


Zinazohusiana


Madudu zaidi

CAG katika ukaguzi wake wa 2021/22 alibaini kuwa TTB ni miongoni mwa mashirika 13 ya umma ambayo hayana kamati ya bajeti.

Kamati za bajeti zina wajibu katika kutathmini utekelezaji wa bajeti na mgawanyo wa rasilimali kulingana na vipaumbele vya mpango mkakati na vipaumbele vya Kitaifa kama ilivyoelezwa katika kifungu cha 17(3) cha Kanuni ya Bajeti ya mwaka 2015. 

Mapungufu mengine ni TTB ilifanya manunuzi nje ya Mfumo wa Ununuzi wa Kielektroniki (TANePS) kwa kuingia mikataba 44 mwaka 2021/22 na kutokuwa na bodi ya wakurugenzi kwa miezi 10 hadi kufikia Februari 2023. 

CAG pia amebaini kuwa bodi hiyo haina nyaraka za miongozo ya kuendesha kazi zake hasa kwa kuwa na kanuni za fedha zilizopitwa na wakati hivyo hazikidhi mahitaji ya sasa. 

“Kutokuwepo kwa nyenzo hizo kunaweza kuwa na madhara kwa taasisi ikiwa ni upungufu katika usimamizi wa vihatarishi, kutokuwajibika na kupungua kwa ufanisi katika utoaji wa huduma,” amesema CAG Kichere katika ripoti yake. 

Enable Notifications OK No thanks