Ushindani wa Simu: Sony yaingiza simu mpya sokoni

April 15, 2021 11:22 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni simu ya Xperia1 mark 3 ambayo imewalenga wadau wa filamu, wapiga picha, wadau wa michezo ya simu na watengeneza muziki.
  • Simu hiyo inaambatana na kamera ya aina yake, spika za mfumo wa steji na skrini yenye kasi.
  • Ushindani wake na simu zilizopo sokoni huenda ukawa bado ni sintofahamu.

Dar es Salaam. Mapambano katika teknolojia ya simu janja bado yanaendelea ikiwa baada ya Samsung na One Plus kutangaza simu zao katika robo ya kwanza ya mwaka 2021, mdau mwingine, Sony ameingiza simu mpya sokoni kuendeleza ushindani wa soko.

Simu hiyo ni Xperia 1 mark III ambayo imetambulishwa jana Aprili 14, 2021. Sony imesema simu hiyo inawalenga wabunifu wanaofurahia ubunifu wakiwemo watumiaji na wanaotengeneza maudhui.

Hizi ndizo sifa za Sony Experia 1 mark III ambazo wadau wa ubunifu wanatakiwa kuziangazia kabla ya kununua simu hiyo:

Kamera za video na kupiga picha

Ni uhakika kuwa Sony imewekeza katika kamera katika simu zake. Xperia 1 mark III imekuja na kamera tatu nyuma ambazo zote uwezo wake ni Mega Pixel (MP) 12 ikiwemo kamera ya kupiga picha za upana (wide), picha za mbali (telephoto) na upana zaidi (ultrawide).

Kwa upande wa kamera ya mbele, Sony imeipatia uwezo wa MP 8.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Sony, Mitsuya Kishida kamera hizo zina uwezo mzuri wa kupiga picha wakati wa usiku, kupiga picha ya hadhira anayetembea kwa mwendo kasi na kutengeneza video zisizoathiriwa na kelele za nje ikiwemo upepo.

Tofauti na matoleo mengine maarufu ya Android yaliyotolewa mwaka huu. Sony bado imebaki na sehemu ya kuweka earphone za kawaida (3.5mm jack). Picha| Sony.

Spika za kusikiliza muziki ufanano na wa jukwaa

Katika uzinduzi wa simu hiyo, Sony imesema mfumo wa muziki unaoambatana na simu ya Xperia 1 mark III umefanania na ule ambao huandaliwa katika steji kwa ajili ya muziki.

Hiyo inamuwezesha mtu ambaye anaandaa muziki kupata nafasi ya kusikia ni kwa namna gani muziki wake unaweza kusikika katika simu.

“Muziki utasikika kwa nyuzi 360 iwe kwa earphones za waya au zisizo na waya,” imesema Sony.

Skrini ya kutazamia filamu na kuchezea michezo

Kwa wadau wa michezo ya simu (video games) huenda simu hii ikawa ni dodo chini ya mnazi kwani imetengeenzwa na uwezo wa kuipoza simu pale inapochemka na hivyo kumpatia mchezaji uwezo wa kucheza kwa muda mrefu bila simu kuathirika kasi, uwezo au kuganda.

Hata hivyo, kwa betri lenye uwezo wa mAh 4500 linaloambatana na simu hii huenda ikawa bado ni changamoto katika kutumia simu hiyo kwa muda mrefu ikizingatiwa kuwa simu kama Samsung Galaxy S21 Ultra ina uwezo wa mAh 5000. 

Hata hivyo, uwezo wake ni sawa na Oneplus 9 ambayo pia ni juu ya iPhone 12 ya mwaka 2020.

Simu hii inaweza kuchajiwa na kujaza betri kwa asilimia 50 ndani ya dakika 30 huku ikiwa na uwezo wa kuchaji simu janja zingine zilizo na mfumo wa kuchaji wa QI.


Soma zaidi: 


Mawazo ya watengeneza maudhui

Siganje Mjelwa ambaye ni mpiga picha na mtengeneza maudhui ya video mkoani Dar es Salaam amesema uzuri wa simu ya Sony ni kuwa kamera zake zote zina uwiano yaani MP 12 ambayo endapo mtu anachukua video itakuwa na uwiano katika mapana, picha ya karibu na hata picha ya mbali.

Mjelwa amesema  ikilinganishwa na simu zingine ikiwemo One Plus 9 na Samsung S21, Samsung na Oneplus zimeizidi simu hii kwa kamera ikiwa Samsung ina kamera yenye MP 108 huku One Plus ikiwa na MP 50.

Nani atafuata baada ya Samsung, One Plus na Sony?kaa chonjo na Nukta Habari (www.nukta.co.tz).

Enable Notifications OK No thanks