Nyeusi, nyeupe: Yanayofahamika kuhusu OnePlus 9, OnePlus 9 Pro
- OnePlus wameweka kamera sawa katika simu zote mpya.
- Uhalisia wa rangi za picha ni kati ya vitu wanavyojivunia katika kamera ya simu hizo.
- Kununua aina mojawapo, unahitaji zaidi ya shilingi milioni moja na nusu za Tanzania.
Dar es Salaam. Pale unapoingia dukani kwa ajili ya kununua simu huwa unaangalia nini ili kupata simu ambayo unaihitaji?
Wapo wanaoangalia namna mfuko wao umetuna yaani pesa waliyonayo, wapo wanaoangalia uwezo wa betri na wanaoangalia uzuri wa nje wa simu. Kwa sifa hizo, huenda ikawa ni rahisi kufanya maamuzi lakini kwa wanaoangalia uwezo wa kamera, huenda wana kibarua kizito.
Kampuni ya OnePlus inayotengeneza vifaa vya kielektroniki ikiwemo simu na saa janja imeingiza sokoni toleo jipya la OnePlus mfululizo wa tisa (9 series) wa simu za OnePlus 9 na OnePlus 9 pro ambazo wapenzi wa kamera katika simu huenda ikawaacha katika njiapanda ya kuchagua simu kwa ajili yao.
Katika uzinduzi wa simu hiyo uliofanyika jioni ya Machi 23, 2021 OnePlus imesema kamera zake zimetengenezwa na kampuni ya Hasselblad ambayo ni maarufu kwa kutengeneza kamera zinazosifika zaidi na wapigapicha.
OnePlus 9 imetengenezwa na rangi tatu ambazo OnePlus wameziita Winter Mist, Arctic Sky, na Astral Black. Picha| OnePlus
Nini kipya katika kamera ya simu ya OnePlus?
Tofauti na kampuni nyingine zinazotengeneza simu, OnePlus imeweka usawa katika simu zake kwa upande wa kamera. OnePlus imeeleza simu ya OnePlus 9 na OnePlus 9Pro zina kamera tatu.
Kamera kuu (main camera) ina uwezo wa “Megapixel” (MP) 48, kamera ya picha pana (telephoto) ina MP50, kamera ya kupiga vitu vya mbali (telephoto) ina MP8.
Kamera za mbele za simu hizo, ambazo hutumika kwa ajili ya kupiga selfie, zinakuja na uwezo mkubwa wa kupiga picha (megapixel) kwa kiwango cha MP16 ambacho si haba sana.
Endapo OnePlus 9 Pro ikilinganishwa na iPhone 12 Pro Max, OnePlus imefanikiwa kuipita simu hiyo inayotengenezwa na kampuni Apple Inc yenye uwezo wa MP12. Hata hivyo, kamera ya mbele ya OnePlus 9 Pro bado ni chini takriban mara 15 ya Samsung Galaxy S21 Ultra ambayo ina MP108.
Hata hivyo, OnePlus imeambatana na sifa ambazo huenda mpiga picha yeyote anayetumia simu akavutiwa nazo ikiwemo uwezo wa kupiga picha zinazong’amua rangi halisia, kuondoa mikunjo ya kitu kilichopigwa picha ambayo kamera nyingi huziacha hasa katika pembe za picha.
“Ubia wetu na OnePlus unalenga kutengeneza kamera bora zaidi kuwahi kuwepo kwenye simu. Kuanzia kupata uhalisia katika rangi na kupata picha zinazoweza kusimulia hadithi, ndio lengo la kamera hii,” amesema Makamu wa Rais wa Kampuni ya Hasselblad, Jon Diele.
Uchambuzi wa awali wa baadhi ya wachambuzi wa vifaa vya kielektroni unabainisha kuwa One Plus pia ina uwezo mzuri wa kupiga picha nyakati za usiku ikilinganishwa na kamera ya simu za iPhone. Simu hiyo mpya inaambatana na mfumo wa kupiga picha kidijitali na mfumo wa “manual” kwa ajili ya wataalamu.
Endapo OnePlus 9 Pro ikilinganishwa na iPhone 12 Pro Max, OnePlus imefanikiwa kufua dafu kwa simu inayotengenezwa na kampuni Apple Inc yenye uwezo wa MP12. Picha| Mobile Syrup.
Betri lina maisha kuliko nyingine
Licha ya kuwa njia ya kuchaji simu bila waya sio kitu kigeni katika ulimwengu wa simu janja, OnePlus wameongeza teknolojia hiyo na mfumo wa “warp charging” ambao unachaji kwa kasi zaidi.
Kwa mujibu wa wataalamu wa kampuni hiyo, simu ya OnePlus inaambatana na betri lenye uwezo mkubwa wa kukaa na chaji wa MAh4,500, kiwango ambacho ni kikubwa kuliko iPhone 12 iliyo na MAh3,687).
Iwapo utachaji simu hiyo kwa njia ya kawaida ya waya OnePlus 9 na OnePlus 9 Pro zina uwezo wa kujaza asilimia 65 ya betri kwa dakika 15 na chini ya dakika 30 kufikia asilimia 100 ya kiwango cha chaji kinachotakiwa.
Tovuti ya teknolojia ya GSM Arena inabainisha kuwa simu mpya za OnePlus zina uwezo wa kuchaji asilimia 100 ya betri kwa dakika 43 bila way (wireless) ukilinganisha na hadi saa tatu zinazotumika na iPhone 12 Pro Max kujaza betri kwa asilimia 100 bila waya.
Soma zaidi:
- OnePlus: Simu yenye mapinduzi ya kamera kuwekwa hadharani leo
- Kijana anayetikisa mitandao ya kijamii kwa utamaduni wa Kimasai
- Uzazi wa mpango kufanyika kidijitali
Kioo kimeongezwa ubora kwa teknolojia mpya
Vioo vya simu hizo vimetengenezwa na teknlojia ya “Fluid dispaly 2.0” yenye uwezo wa kupunguza mionzi mibaya kwa macho kwa mtumiaji wake.
OnePlus imesema teknolojia hiyo ya kioo ina uwezo wa kupunguza matumizi makubwa ya betri na hivyo kufanya hata mtumiiaji mkubwa wa simu kuwa na uhakika wa kukaa na simu yake kwa siku nzima.
Zaongezwa kipooza simu
Pia, OnePlus imesema simu hizo zina teknolojia maalumu ya kupoza simu pale inapokuwa katika matumizi makubwa. Jambo hilo litaepusha simu kuchemka hata pale mtu anapocheza michezo ya kidijitali (games).
Simu za OnePlus zinakuja katika rangi tatu “Winter Mist, Arctic Sky, na Astral Black” kwa One Plus 9 na Astral Black, Morning Mist, na Pine Green kwa OnePlus 9 Pro.
Bei yako bado haishikiki
Hata hivyo, gharama za simu hizo zipo juu zaidi ya wastani wa simu janja nyingine ambazo zina bei rafiki kwa watu wenye kipato kidogo na wastani kama Tecno, Huawei na baadhi ya simu za Samsung.
Ili kununua simu hizo, utahitaji si chini ya Sh1.69 milioni kwa OnePlus 9 inayokuja na uhifadhi kuanzia GB 8-128 na Sh2.47 milioni kwa OnePlus 9 Pro inayokuja na uhifadhi kuanzia GB12-256 kwa njia ya maduka ya mtandaoni ikiwemo Amazon, Tmobile na Telenor.
Gharama hizi huenda zikabaki hivyo au zikawa kubwa kidogo Tanzania kwa ajili ya gharama nyingine za usafirishaji na masuala ya kikodi.