Waliofutiwa matokeo kidato cha nne 2025 waongezeka
- Idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka 2025 imepungua kulinganisha na iliyorekodiwa mwaka 2024.
- Waliofutiwa matokeo watapewa nafasi ya kurudia mitihani.
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wanafunzi wa kidato cha nne nchini wakifurahia matokeo yao, hali ni tofauti kwa wanafunzi 77 waliofutiwa matokeo yao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo udanganyifu.
Prof Said Mohamed, Katibu Mkuu wa Necta aliyekuwa akitangaza matokeo hayo leo Januari 31, 2026 jijini Dar es Salaam amesema wanafunzi 77 waliofanya Mtihani wa Kidato cha Nne (CSEE) walibainika kufanya udanganyifu kwenye matokeo yao na wawili kuandika matusi.
“Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 77 (30 wa shule na 47 wa kujitegemea) katika Mtihani wa Kidato cha Nne 2025 waliobainika kufanya udanganyifu katika mtihani na wawili wa shule walioandika lugha ya matusi katika skripti zao,” amesema Profesa Mohamed.
Matokeo hayo yamefutwa kwa mujibu wa Kifungu cha 5(2) (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani, Sura ya 107, kikisomwa pamoja na Kifungu cha 30(2)(b) cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016.
Hata hivyo, Necta imebainisha kuwa kufutiwa matokeo hayo sio mwisho wa elimu hivyo, wanafunzi hao wamepewa fursa ya kurudia mtihani katika mwaka mwingine.
Wanafunzi hao ambao wanapaswa kuomba kufanya mtihani wa marudio kwa kujisajili kama watahiniwa binafsi (Private Candidate) watafanya mitihani yao sambamba na kidato cha sita watakaokuwa wanamaliza ngazi hiyo ya elimu.
Idadi hiyo ya waliofutiwa matokeo katika mtihani CSEE kwa mwaka huu imepungua kulinganisha na ile iliyoripotiwa katika matokeo ya mwaka 2024.
Januari 23, mwaka 2025 Necta ilitangaza kufuta matokeo ya wanafunzi 72 kwa udanganyifu na kuandika matusi ambapo 67 walifanya udanganyifu na watano walioandika matusi katika karatasi za kujibia katika mitihani.
Kwa mujibu wa Necta kupungua kwa wanafunzi wanaofutiwa matokeo kunatokana na jitihada mbalimbali zinazofanywa na baraza hilo ikiwemo kutoa elimu kwa wasimamizi, wanafunzi na walimu.
Katika mtihani huo, jumla ya watahiniwa 595,810 walisajiliwa kufanya mtihani,wakiwemo wasichana 318,910, sawa na asilimia 53.53, na wavulana 276,900, sawa na asilimia 46.47.
Kati ya watahiniwa hao, 569,883 walikuwa watahiniwa wa shule na 25,927 walikuwa watahiniwa wa kujitegemea.
Latest