Bajeti wizara ya maji yashuka Tanzania, fedha za miradi ya maendeleo juu
- Bajeti hiyo imeshuka kwa Sh52.8 bilioni kwa mwaka 2021/22.
- Asilimia 95.1 ya bajeti hiyo kutekeleza miradi ya maji.
- Hali ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini yazidi kuimarika.
Dar es Salaam. Huenda uhakika wa upatikanaji wa huduma maji nchini Tanzania ukachelewa kidogo, kutokana na kupungua kwa bajeti ya Wizara ya Maji kwa Sh52.8 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/22.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso aliyekuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake leo Mei 6, 2021 bungeni jijini Dodoma ameliomba Bunge liidhinishe Sh680.4 bilioni kwa ajili ya mwaka 2021/22, kiwango ambacho kimeshuka kutoka Sh733.3 bilioni zilizotengwa mwaka 2020/21.
Bajeti ya wizara hiyo inayopendekezwa na Aweso katika mwaka wa fedha unaoanza Julai 2021, ipo chini ya ile ya mwaka jana kwa asilimia 7.2.
Hata wakati bajeti ya maji kwa mwaka ujao ikipungua, wizara hiyo imetenga kiwango kikubwa zaidi kwa ajili ya maendeleo baada ya kuainisha Sh646.6 bilioni zitatumika katika kutekeleza miradi ya maji sawa na asilimia 95.1 ya bajeti yote.
Kiasi kilichobaki cha wastani wa asilimia tano kimependekezwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi wa wizara hiyo.
Aweso ambaye ni Mbunge wa Pangani amesema kati ya fedha hizo za bajeti ya maendeleo zilizotengwa, Sh346.6 bilioni ni fedha za ndani.
Waziri huo anaomba fedha hizo licha ya kuwa utekelezaji wa bajeti ya sasa umefikia nusu tu licha ya kuwa tayari miezi 10 ya mwaka wa fedha 2020/21 imeshakatika.
“Hadi mwezi Aprili 2021, Wizara imepokea jumla ya Sh396.7 bilioni sawa na asilimia 54.1 ya bajeti (ya mwaka 2020/21),” amesema Aweso ambapo kati ya fedha zilizopokelewa, Sh376.5 bilioni ni fedha za maendeleo.
Zinazohusiana:
- Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano utunzaji bonde la mto Nile
- Visima kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama nchini?
Iwapo italinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21, bajeti ya maendeleo iliyotengwa katika wizara hiyo imepungua kidogo, jambo linaloweza kupunguza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.
Mwaka wa 2020/21 ambao unaisha Juni 30 mwaka huu, bajeti ya maendeleo ilikuwa asilimia 96.2 ya bajeti yote ya wizara hiyo.
Wizara ya Maji inakuwa miongoni mwa wizara chache ambazo zimefanikiwa kutenga zaidi ya asilimia 80 ya fedha zake kutekeleza miradi ya maendeleo katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa miaka mingi uhaba wa maji safi na salama umekuwa ukiziandama baadhi ya jamii za vijijini na mijini jambo linalosababisha magonjwa kama kuhara na kurejesha nyuma jitihada za kukuza uchumi.
Katika mwaka 2021/22, Aweso amesema Serikali imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1,527 ya maji katika maeneo ya vijijini na miradi 114 ya mijini ikihusisha miradi mipya, miradi ya upanuzi na ukarabati wa miundombinu.
Aidha, Serikali imepanga kuchimba visima 516 na kujenga mabwawa 33 hususan katika maeneo kame nchini ili kuwapunguzia wananchi adha ya upatikanaji wa maji.

Kwa mujibu wa Wizara ya Maji, hivi sasa, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji vijijini imefikia wastani wa asilimia 72.3 huku hali ya mijini ikiwa nzuri kidogo kwa asilimia 86.
Lengo ni kuhakikisha kuwa huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi inafikia zaidi ya asilimia 85 ifikapo mwaka 2025, kiwango ambacho tayari maeneo ya mijini yameshakifikia.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, Dk Christine Ishengoma amesema licha ya Serikali kutenga kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo kwa mwaka 2021/22, inapaswa kutazama namna ya kuongeza fedha za miradi ya maji kwa sababu zimepungua ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu.
Pia kamati hiyo imeshauri Serikali kuweka nguvu kubwa katika utunzaji wa vyanzo vya maji na ujenzi wa mabwawa yatakayosaidia uvunaji wa maji katika maeneo mbalimbali nchini.
“Kuanzishwa na kusimamia mpango mkakati kuhakikisha uvunaji wa maji ya mvua unakua endelevu kwa matumizi ya akiba na hasa wakati kiangazi,” amesema.