Tanzania kuendelea kutoa ushirikiano utunzaji bonde la mto Nile
Mto Nile ni chanzo muhimu cha maji kwa nchi za maziwa makuu. Picha| Interesting Facts
- Itashirikiana na nchi za ukanda wa maziwa makuu katika kusimamia matumizi endelevu ya maji ya mto Nile kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi wa nchi wanachama.
- Nchi hizo zimeshindwa kufikia makubaliano ya kuanzisha kamisheni ya kudumu ya bonde la mto Nile tangu mchakato wake ulipoanza miaka 10 iliyopita.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na nchi za ukanda wa maziwa makuu katika kusimamia matumizi endelevu ya maji ya mto Nile kwa ajili ya ustawi wa kiuchumi wa nchi wanachama.
Majaliwa amesema hayo leo (Novemba 22, 2018) wakati akifungua mkutano wa 21 wa Baraza la Mawaziri la nchi za bonde la mto Nile zilizopo ukanda wa maziwa makuu unaofanyika Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Rais John Magufuli.
Nchi wanachama zimepewa changamoto ya kuimarisha ushirikiano ili ziweze kusimamia vizuri matumizi endelevu ya maji ya mto Nile pamoja na kushughulikia changamoto zinazolikabili bonde hilo.
Majaliwa ametaja baadhi ya changamoto mbalimbali ikiwemo kushindwa kufikia makubaliano ya kuanzisha Kamisheni ya kudumu ya bonde la mto Nile tangu mchakato wake ulipoanza miaka 10 iliyopita.
Sambamba na changamoto hiyo nchi wananachama zimekuwa zikichelewa sana kutoa michango yao ili kuziwezesha taasisi zilizo chini ya jumuiya hiyo kutekeleza ipasavyo majukumu yake, jambo ambalo si tu linachelewesha maendeleo bali linatishia usalama wa maji katika bonde la mto Nile.
“Suala jingine ni ulipaji wa michango, taasisi zetu haziwezi kutekeleza majukumu yake kama hatulipi michango tena kwa wakati maana miradi ya maendeleo haiwezi kutekelezwa kwa haraka kwa kutegemea wafadhili, ni vema nchi zikalipa michango,” emesema Majaliwa.
Hata hivyo, Majaliwa amesema ili matumizi ya rasilimali za bonde la mto Nile ziwe endelevu, nchi wanachama zitoe elimu kwa wananchi katika maeneo yao kutunza mazingira na kuhakikisha shughuli zao haziathiri uhai wa bonde hilo.
Zinazohusiana:
- Namna tani zaidi ya 200,000 za korosho zitakavyonunuliwa na Serikali
- Rais Magufuli awafuta kazi Tizeba, Mwijage joto la korosho likipanda
- Kwanini ufuatilie mjadala wa bei ya korosho?
Amebainisha kuwa maji ni rasilimali muhimu duniani kwa ajili ya uhai wa binadamu, maendeleo ya kiuchumi na kijamii hususani katika kuendesha shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji, utalii na ujenzi, hivyo lazima vyanzo vitunzwe.
Bara la Afrika ni miongoni mwa maeneo yanayokabiliwa na matatizo makubwa ya maji duniani, ambapo Majaliwa amesema takwimu zinaonesha kuwa takribani nchi 14 hivi sasa zinakabiliwa na uhaba ama upungufu wa maji huku zingine 11 zinatarajiwa kuingia katika kundi hilo ifikapo 2025.
Kutokana na hali hiyo mikakati ya makusudi inahitajika ili kuhakikisha chanzo cha maji katika bonde la mto Nile kinalindwa na kutumika vizuri.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa ambaye ndiye Mwenyekiti wa baraza la mawaziri wa nchi za bonde hilo za ukanda wa maziwa makuu; waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani.
Wengine ni Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Awesu, mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao nchini, watendaji wa sekretarieti ya Bonde la Mto Nile kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu pamoja na Ukanda wa Mashariki na maafisa wengine wa Serikali.