Umekata tamaa ya maisha? Tazama filamu hii

May 24, 2021 12:58 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni filamu ya “Those Who Wish Me Dead” inamuhusu Conor, kijana mwenye umri wa miaka 12 anayepambana ili kufikia ya ndoto ya baba yake.
  • Ni baada ya Baba yake kuuwawa na majambazi ambao wanaendelea kumtafuta Conor ili kufuta ushahidi.
  • Ethan pamoja na mkewe Allison wanaingia matatizoni baada ya kuonekana wao ndiyo wasaidizi pekee wa Conor.

Dar es salaam. Wakati wewe ukiamini katika utendaji wako wa kazi kuwa ni sawa na wa haki, kuna watu wanaona ni kama unawaingilia katika maisha na kazi zao. Wanatafuta jinsi ya kukuondosha ili wao wabaki salama.

Hali hii inamkuta Owen, mhasibu mchunguzi ambaye anatafutwa na watu waliosababisha kifo cha bosi wake. Kisa hiki kinapatikana katika filamu ya “Those Who Wish Me Dead” inayopatikana katika jukwaa la Netflix.

Ni asubuhi na mapema wanaonekana watu wawili katika nyumba ya muendesha mashtaka wa wilaya. Watu hao wanajitambulisha  kama maafisa wa mamlaka ya gesi na moto na wanapokelewa na mke wa muendesha mashtaka akiwakaribisha ndani na kuwaeleza kuwa mumewe yuko bafuni. 

Ni Jack na Patrick ambao wanatekeleza mauaji katika nyumba hiyo na kuacha mlipuko mkubwa unaoteketeza kila kitu baada ya wao kuondoka.  

Mwendesha mashata huyo anafariki dunia na taarifa zinamfikia Owen ambaye ni mfanyakazi wake wa karibu. Owen akijua fika kuwa yeye ndiye anayefuata anaingiwa na hofu na kuchukua jukumu la kuondoka mbali na mahali anapoishi na kuelekea kwa shemeji yake aitwaye Ethan ambaye ni askari anayeishi Montana.

Wakiwa katika harakati za kuondoka Conor anahoji kutokana na kuona hali ya baba yake kuingiwa na wasiwasi na kumsihi baba yake kuwa kama kuna jambo baya basi wawahusishe polisi.

Lakini Owen anajibu na kumuambia ulinzi wa hao askari haukufua dafu mbele ya wale wauwaji kwani taarifa walizonazo zinawahusu watu wengi ikiwemo watu wa mamlaka ya juu serikalini na kitu pekee walichotakiwa kukifanya ni kwenda kwa wale tu wanaowaamini.

Baada ya muda, Jack pamoja na Patrick wanaonekana wakiingia nyumbani kwa Owen kwa ajili ya kutekeleza mauaji ili kumaliza kabisa wote waliokuwa waliokuwa wanafahamu mambo ya mwendesha mashtaka.

Wanakagua nyumba ya Owen wanagundua kuwa watu wanaowatafuta hawapo mahali pale. Jack na Patrick wanakutana na kompyuta ndogo inayowadhihirishia kuwa Owen ameshajua nini kinaendelea na hivyo ameamua kuokoa maisha yake.

Wakiwa wanaendelea na upekuzi kupata chochote kitakachowasasaidia kupata taarifa, Patrick anakutana na picha ya familia iliyowapelekea kujua ni mahali gani Owen na Conor watakuwa wakielekea. Wanafunga safari kuwafuata walipo.

Jack na Patrick wanatangulia kufika Montana kwa usafiri wa ndege kabla ya Owen na Conor na wanaelekea katika barabara iliyokuwa inatumiwa na Owen kuelekea Montana na kuweka mtego ili kuwanasa Owen na Conor.

                           

Baada ya muda kupita na ukaguzi wa magari yaliyokuwa yakipita ukifanywa kwa kutumia bunduki wanafanikiwa kuwaona Owen na Conor na kumimina risasi nyingi zinazompata Owen na kusababisha gari walilokuwa wakisafiria kupoteza uelekeo na kuingia bondeni.

Katika hali ya maumivu Owen anamkabidhi siri zote mtoto wake na kumsihi afuate miteremko ili atafute mtu atakayemuamini na kuweza kufikisha yale aliyomuachia katika mikono ya vyombo vya habari.

Conor anaamua kuondoka na kumuacha baba yake ndani ya gari akimiminiwa risasi kwa mara ya pili baada ya kugundulika na Wauwaji wale kuwa bado yu hai.

Walipokuwa wamemaliza kutekeleza hayo anatokea mwanamama mmoja ambaye anahoji juu ya usalama wa eneo hilo ambaye naye anauwawa.

Punde baada ya Wauwaji kutoweka Ethan anafika na kushuhudia hali iliyokuwepo pale ikiwa ni pamoja na mauaji ya ndugu yake aliyekuwa akielekea mahali anapoishi huku kijana Conor akiwa hayupo eneo la tukio.

Conor anafika mbali na kukutana na askari wa zimamoto mwanadada ajulikanaye kwa jina la Hannah. Katika hali ya uoga, Conor anakimbia lakini anafuatwa na Hannah ambaye anamshika na kujitambulisha kuwa yeye si mtu mbaya.

Conor anaridhia kubaki na Hannah ambaye alimuahidi kupiga simu kwa mtu yeyote ambaye Conor angehitaji na wanarejea mahali ambako ndiko Hannah alikuwa katika zamu ya uangalizi wa moto katika pori hilo.

Hannah anajaribu kutafuta mawasiliano katika mnara uliokuwa ukitumika kama sehemu ya uangalizi ili kutimiza yale aliyokuwa amemuahidi Conor bila mafanikio.


Zinazohusiana


Wakiwa njiani Jack na Patrick wanapokea simu ya Tajiri aliyewaajiri katika kazi hiyo akiwataka kuonana nao na kuwapa taarifa ya kwanini hawajamuuwa Conor na  kuwataka kuhakikisha wanafanya hivyo ndani ya muda mchache.

Wanaondoka na kwenda kutekeleza jukumu hilo ambapo Jack anachukua uamuzi wa kulichoma pori ambalo Conor alikuwemo ndani yake akiamini hii itawafanya wao kuwa na kazi rahisi katika kumtafta Conor kwani Serikali, vyombo vya dora na watu wote wa mji huo watakuwa wakishughulika na moto na si vinginevyo.

Wanafunga safari kuelekea kwa Ethan ambako ndiko ilikokuwa hatma ya Owen na mwanae Conor. Wauwaji wanafika na kumkuta Allison mke wa Ethan ambaye ni mjamzito.

Wanajitambulisha kama maafisa wa FBI lakini Allison anagundua kuwa siyo kweli na hivyo wanaazisha mapigano ambapo Allison anazidiwa nguvu na kuwekwa chini ya ulinzi wakimtaka apige simu kwa mumewe ili arejee nyumbani. 

Allison kwa ujanja anafanya hivyo kwa namna ya kutoa taarifa kwa mumewe katika hali hiyo wauaji wanaligundua hilo  na purukushani za hapa na pale zinatokea na Allison anafanikiwa kuwakimbia.

Ethan anafika nyumbani bila kujiandaa vyema akiwa na jazba hali inayosababisha kufikia mikononi mwa wauaji kwa urahisi zaidi. Wanamtaka kuongozana nao porini ili kuweza kumpata Conor wakimtisha kuwa mke wake wanamshikiria na wangemuua tu endapo angewasumbua. Wanaondoka kwa pamoja kuelekea porini kumtafuta Conor.

Mke wa Ethan anagundua kuwa mumewe hayupo anatumia kifaa cha kufuatilia kujua mumewe mahali alipo, baada ya kugundua hivyo anachukua silaha na farasi kulekea huko.

Je, Allison atafanikiwa kumuokoa mumewe? Na Je, Hannah na Conor watafanikiwa kutoka katika pori lenye moto na kufikia malengo ya Owen?

Kwa majibu ya maswali haya na mengine mengi usiache kuangalia filamu hiyo ambayo inaonyeshwa katika kumbi za kuangalizia filamu zikiwemo za Century Cinemax zilizopo katika maduka  makubwa (malls) jijini Dar es Salaam.

Enable Notifications OK No thanks