Ifahamu filamu ‘inayotrend’ kwenye mitandao ya Kijamii Tanzania
- Ni filamu ya Binti inayozungumzia changamoto za kimaisha zinazowakumba mabinti wanaoishi mjini.
- Filamu imeongeza orodha ya filamu za kitanzania zinazoonyeshwa ‘Netflix’
Dar es Salaam. Leo nakusogeza karibu na filamu ya “BINTI”. Ambayo kama wewe ni mdau wa mitandao ya kijamii, hauwezi kuwa umepitwa na walau kusikia jina hilo.
Iwe WhatsApp, Instagram na kwenye mtandao mingine ya kijamii, jina la filamu hii limesambaa haswaa.
Ni nini kinafanya filamu hii kujitofautisha na filamu zingine zilizowahi kutolewa na Watanzania? Chukua ‘popcorn’ zako maana safari yetu, hapa ndipo inapoanzia.
Tukubali. Filamu hii imejua kuzungumzia uhalisia bwanaa! Hasa ukweli wa chamgamoto za kimaisha wanazopitia mabinti wengi Tanzania, hasusan maeneo ya mjini kama Dar es Salaam.
Changamoto za mahusiano, malezi, umaskini na mategemeo zote zimeelezewa kupitia wahusika wanne: Tumaini, Angel, Stella pamoja na Rose.
Mabinti hawa wanapitia changamoto za mahusiano , umaskini, mategemeo na mahusiano. Picha| Netflix
Tumaini anapambana na hali ya umaskini waliyonayo yeye na mama yake. Anafanya hivyo kwa kufanya shughuli za hapa na pale ili apate chochote kitu cha kupeleka mkono kinywani.
Kusambaza mayai kwa baiskeli, kung’ang’ana na duka ambalo kwa kulitazama tu unajua limeshafirisika, ni sehemu ya mapambano ya binti huyo.
Kinachosikitisha zaidi ni kuwa, pesa zote anazozipata kwa jasho, hazifaidi hata kidogo. Zote zinatumika kwenye kulipa deni waliloachiwa na baba yake.
Maisha huwa na namna ya kukukutanisha na watu bwana. Kwa Tumaini, ulimwengu unamkutanisha na Angel. Kumbukumbu inayomjia ni kuwa, wamewahi kusoma pamoja.
Licha ya kufundishwa na walimu wale wale, tofauti ya Tumaini na Angel ni kuwa, Angel ameshapiga hatua kimaisha. Tayari ana duka la kuuza mavazi ya mabibi harusi na kama inavyoweza kuwa ndoto ya mabinti wengi, Angel ana mchumba mwenye mapene yake. What a difference!
Fumbo lililopo kwa wengi ni kama fedha hizo au maisha hayo yanampatia mtu amani.
Tumaini ana maisha magumu lakini moyo wake una amani haswa lakini kwa Angel, mambo sivyo yanavyoonekana kwenye luninga ya mitandao yake ya kijamii.
Maisha ya Angel ni ya kilio na vipigo kila uchwao kutokana na kuwa na mwanaume mwenye wivu kupitiliza. Ndiyo ana fedha lakini wivu wake, ni wakutisha.
Angel anajikuta akiangua kilio kila siku kutokana na manyanyaso anayoyapitia kwenye mahusiano yake. Picha| Pro Tv movies.
Ukikutana na Angel nje ya chumba chake na mpenziwe, Weeeeeh! Utabaki mdomo wazi. Make up imekaa, unyunyu unanukia haswaa, gari anayotembelea, MashaAllah lakini ipo siri chini ya tabasamu, mng’aro na hata “kujimwambafai” kwake mjini.
Angel hana la kufanya kwani “mtaka cha uvunguni, sharti ainame” anachagua kuvumilia mateso, shida na vipigo kwani ‘Fenty’,’ Gucci,’ Versace’ na hata safari za ‘ATM’ haziji bure bure.
Maisha ya Stella na Rose
Katika upande wa pili wa shilingi, maisha ya Stella ni kinyume na yale ya Angel. Stela hajui hata kofi kutoka kwa mumewe linafananaje.
Kwake ni huba iliyokolea moto na maisha yake ya ndoa yana amani tele. Hii inanikumbusha vile mabinti huomba wapate mume kama wa mwanamuziki Ciara.
Mume Mhot, mchapa kazi pesa ipo, upendo upo, utake nini sasa? Lakini wengi husahau kuwa utampata wa kufanana naye.
Licha ya hayo yote kipo kinachomkoseha raha Stella. Ni uhitaji wa kelele kwenye nyumba. Vishindo vidogo vidogo vya viumbe vikikimbizana ndani. Stella anatamani watoto.
Stella amefanya “almost” kila kitu. Mazoezi, ‘diet’, vidonge, safari za hospitali kukutana na kila mtaalamu lakini wapi. Maumivu yanayomsababisha hadi agombane na mumewe kwa kuona huenda haumizwi na ile hali kama yeye.
Kwa Rose, yeye ana maisha mazuri. Mume anayempenda, watoto na kazi nzuri, unaweza sema ana kila kitu ukilinganisha na wengine. Lakini kumbe naye lipo linalomsibu.
Malezi ya mwanaye wa kiume, Chriss yanamuumiza kichwa. Chriss ni wa kulia kila muda bila mapumziko. Chriss ni wa kuamka na hili na kulala na lile. Kutwa kuna sintofahamu.
Hilo linamwacha Rose kwenye njiapanda kwani wakati mwingine anashindwa kutimiza majukumu yake ya kazi kutokana na kutakiwa kuwa karibu na mwanaye tena muda wote.
Najua unatamani kujua nini hatima ya mabinti hawa kama endapo waliweza kutatua changamoto wanazozipitia au maisha ndiyo yaliwapiga.
Nisikutafunie muwa wote. Tazama filamu hii ya Kitanzania ambayo ni ya pili kuingia kwenye jukwaa la Netflix iliyoongozwa na mwanamama Seko Shamte akiwa na waigizaji wakali kama Godliver Gordian na wengine.