Filamu ya Brazen: Maandishi yanayomuwinda mwandishi wa vitabu
- Filamu hii inamuhusu mwandishi wa simulizi za mauaji ambaye anajikuta simulizi zake zikitokea katika maisha halisi.
- Huku mtu wa kwanza kuuwawa akiwa ni dada yake.
Dar es Salaam. Filamu ya “Brazen” inamuhusu mwanamama Grace Miller ambaye ni nyota maarufu wa vitabu vya simulizi nchini Marekani. Simulizi zake zilizobeba visa vya mauaji wanayofanyiwa wanawake, zinafanya watu kutoa fedha kupata vitabu vyake bila hata kuomba punguzo.
Kifupi Grace amebarikiwa haswa kwenye tasnia ya uandishi.
Uchaguzi wa maneno yake, masimulizi, fanani anaowatumia ni utaalamu unaoweza kumfanya hata mtu asiyependa kusoma vitabu asome.
Siku moja akiwa kwenye moja ya matamasha yake ya kuwasomea watu vitabu, dada yake Kathleen Miller anampigia simu na kumueleza changamoto anazopitia baada ya kutalakiana na mumewe.
Jambo hilo linamfanya Grace kufunga safari hadi nyumbani kwa dada yake, kwani anaamini undugu ni kufaana siyo kufanana.
Akifika huko, anashangaa Kathleen haonyeshi kufurahishwa na ujio wake.
Grace anapata wasiwasi kwanini dada yake asifurahie ujio wake, na zaidi anahisi kuna kitu dada yake anamficha.
Grace anajikuta yale anayoyaandika kwenye vitabu vyake yanaanza kutokea katika maisha halisi. Picha| Variety.com
Licha ya mapokezi ya kishingo upande, Grace anaamua kupotezea kwani upendo alionao kwa dada yake asingeweza kuvumilia kuwa mbali wakati dada yake akipitia magumu.
Bila shaka kila mtu anatamani apate ndugu wa namna hii.
Nikwambie tu huruma ya Grace inamponza, kwani ujio wake unafanya maisha yake yaingie kwenye kimbunga cha jangwani. Kimbunga ambacho hakuna jengo, mti wala chochote cha kupunguza kasi yake.
Upepo unabadilika
Unakumbuka mwanzo nilisema vitabu vya Grace vimebeba visa vya mauaji?
Haya kaa sawa sasa kwani hapa ndipo maandishi yake yanapoanza kugeuka uhalisia. Tena, uhalisia kwake na siyo kwa wanawake asiowajua.
Kimbunga kinaanza kwenye maisha ya Grace pale mtu wa kwanza kufanyiwa mauaji hayo ni dada yake na wala hayakuishia hapo.
Kabla hata kidonda cha maumivu ya Grace hakijapoa, na upelelezi haujakamilika, mvua ya mauaji ya wanawake inaanza kushuka.
Mwanamke mwingine anauawa, na hesabu inazidi kwenda juu na hapo ndipo kengele ya malaika mtoa roho inapoanza kugonga kwenye vichwa vya watu waliokaribu na Grace.
Edd ambaye ni askari na mpenzi wa Grace anamwambia mpenziwe kuwa kwa kasi ya mauaji inayoenda, huenda yeye ndiye “target” inayofuata.
Kwa taarifa hizo, unaweza kuhisi Grace alikimbia au kujificha lakini cha ajabu ni kuwa Grace anajitoa sadaka kwa kujifanya mtego ili kurahisisha kumpata muuaji huyo.
Ubaya ni kuwa mtego anaojiwekea Grace hata mchumba wake Edd sidhani kama ataweza kumuokoa.
Edd anamtahadharisha Grace kuwa yawezekana akawa ‘target’ inayofuata ya muuaji. Picha| Glamour.com
Kinachomsumbua zaidi binti huyu wa Mzee Miller ni kuwa, kuna siri ambayo Kathleen alionekana kumficha Grace na ni wazi kuwa inahusiana moja kwa moja na mauaji yanayoendelea.
Ni siri ipi hiyo? Mimi najua lakini sitaki ukatazame filamu hii ukiwa tayari na majibu.
Unadhani nini kitamkuta mwanadada huyu ambaye maandiko yake yanaanza kumuwinda yeye mwenyewe?
Ama yale ya wahenga waliosema uzima na mauti upo katika kinywa cha mtu hawakumaanisha kinywa tu bali na maandishi pia?
Sehemu pekee ya kupata majibu ya maswali hayo ni kwenye filamu ya Brazen ambayo utaipata Netflix.