Mwongozo mpya wa upimaji wa Corona huu hapa

July 1, 2021 8:39 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • WHO imeboresha mwongozo  wake kuhusu upimaji wa ugonjwa wa virusi vya COVID-19.
  • Utapanua wigo wa upimaji katika mazingira mbalimbali ya virusi hivyo.
  • Walio katika hatari kuambukizwa wapewa kipaumbele katika upimaji.

Mwanza. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limeboresha mwongozo  wake kuhusu upimaji wa ugonjwa wa virusi vya COVID-19 ili kupanua wigo wa upimaji katika mazingira mbalimbali ya virusi hivyo katika nchi tofauti duniani. 

Mwongozo huo wa WHO  unaelezea mapendekezo kwa mikakati ya kitaifa ya upimaji na uchunguzi  kwa kutumia vipimo vya kina (PCR) na vile vya papo kwa papo na wakati huo huo kuzingatia hali ya rasilimali za upimaji zinazopatikana kwa nchi husika.

Hatua hiyo ya WHO imekuja wakati huu ambapo virusi vya Corona vinabadilika na kunyumbulika katika maeneo mbalimbali duniani na vingine kuonekana kuwa vinaambukizika kwa urahisi zaidi kuliko vingine.

WHO imesema uchunguzi wa wakati muafaka na sahihi ni muhimu katika kuzuia kusambaa kwa COVID-19.

“Uchunguzi wowote ule lazima ufuatiliwe na hatua thabiti za afya ya umma ikiwemo kuwatenga wale waliothibitika kuwa na Corona na kuwapatia huduma sahihi huku wale waliokuwa karibu nao wakifuatiliwa na kutengwa vile vile kwenye karantini,” imesema WHO katika taarifa yake iliyotolewa jana.

Mapendekezo mapya

WHO inataka nchi ziwe na mkakati wa kitaifa wa upimaji au uchunguzi wa COVID-19 unaoainisha malengo yanayoendana na mabadiliko ya mwongozo mpya kulingana na aina ya mlipuko wa Corona, rasilimali za upimaji zilizopo katika nchi husika.

Pia pimaji na uchunguzi wa virusi hivyo aina ya SARS-CoV-2 lazima uoanishwe na hatua zozote za ulinzi wa afya ya umma na kuhakikisha kuna huduma za tiba na usaidizi kwa wale ambao watakutwa na virusi vya Corona au wale ambao wamekuwa karibu na wagonjwa hao ili nao pia waweze kufuatiliwa na hivyo kudhibiti kuenea kwa virusi.

WHO pia inataka mtu yeyote ambaye atashukiwa kuwa na COVID-19 basi lazima achunguzwe iwapo ana virusi hivyo aina ya SARS-CoV-2, bila kujali amepatiwa chanjo au la na iwapo amewahi kuugua ugonjwa huo wa au la.

Kwa watu ambao wamekidhi vigezo ikiwemo kuwa na COVID-19 inashauriwa wapatiwe kipaumbele katika kupimwa ugonjwa huo.

Na iwapo hakuna rasilimali za kutosha kwa ajili ya kupima watu wote wanaoshukiwa kuwa na Corona, basi walio hatarini kupata magonjwa hatari wapewe kipaumbele katika uchunguzi.

Makundi hayo ni wahudumu wa afya, wagonjwa waliolazwa hospitalini, watu wasio na dalili za Corona lakini wako katika vituo vya huduma ya tiba kwa muda mrefu.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW