Hawa ndio wanasoka 5 wanaoingiza mkwanja mrefu zaidi duniani

July 18, 2026 1:37 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na Cristiano Ronaldo, Messi, Mbappe, Haaland na Vinicius Jr ambao wameendelea kuwa vinara ndani na nje ya uwanja.

Dar es Salaam. Wakati macho ya dunia yakielekezwa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026, vita kubwa haipo tu uwanjani katika kusaka ushindi, mabao na taji, bali pia nje ya uwanja ambako nyota wa soka wanaendelea kuvuna mabilioni ya fedha kupitia mishahara, bonasi na mikataba ya matangazo.

Kwa mujibu wa jarida la Forbes la nchini Marekani, wachezaji 11 wanaoshiriki Kombe la Dunia la mwaka huu wameingiza kwa pamoja kiasi cha takribani Dola za Marekani milioni 950 ambazo kibongo bongo ni zaidi ya Sh2.4 trilioni ndani ya miezi 12 iliyopita, lakini kati yao, wapo watano wanaotawala kilele cha fedha na umaarufu. 

Hawa si tu mastaa wa timu zao, bali ni chapa za kibiashara ambazo kila mechi ya Kombe la Dunia inaweza kuongeza thamani yao sokoni, kwa wadhamini na hata kwenye historia ya mchezo.

5. Vinicius Jr 

Kwenye orodha hii, Vinicius Jr ndiye anayefunga pazia la tano bora, lakini usidanganyike na nafasi yake. Nyota huyo wa Brazil na Real Madrid bado ni mmoja wa wachezaji wanaovuta fedha nyingi zaidi duniani, akikusanya Dola za Marekani milioni 60 ndani ya miezi 12 iliyopita (zaidi ya Sh156 bilioni)

Mbali na mapato anayopata ndani ya uwanja, nyota huyo ambaye ameingia kwenye Kombe la Dunia akiwa na presha ya kuiongoza Brazil kumaliza ukame wa miaka 24 bila taji la dunia bado ni bidhaa kubwa ya kibiashara. 

Nyota huyo ameendelea kuvutia kampuni kubwa za matangazo, huku dalili za ushirikiano mpya na Nike zikionekana.

4. Erling Haaland 

Kama kuna mshambuliaji anayebeba taswira ya nguvu, kasi na mabao ya kikatili, basi huyo ni Erling Haaland. Straika huyo wa Norway anashika nafasi ya nne akiingiza Dola za Marekani milioni 80 (zaidi ya Sh208 bilioni)  kiasi kinachomfanya kuwa miongoni mwa nyota wachache wanaogeuza mabao kuwa mamilioni ya fedha.

Nje ya uwanja, thamani yake imeendelea kupanda baada ya kusaini mkataba mnono wa kuongeza muda na Manchester City. Hata hivyo, hilo halijazima kelele za soko la usajili, hasa kutoka Real Madrid, ambako bado jina lake linaendelea kuzungumzwa.

3. Kylian Mbappé 

Ukizungumzia kizazi kipya cha wafalme wa soka, jina la Kylian Mbappé haliwezi kukosekana. Mshambuliaji huyo wa Ufaransa anashika nafasi ya tatu kwa mapato ya Dola za Marekani  milioni 95 (zaidi ya Sh247 bilioni) na bado anaonekana kuwa mmoja wa wachezaji wenye nafasi kubwa zaidi ya kutikisa si tu Kombe la Dunia hili, bali pia biashara nzima ya soka kwa miaka ijayo.

Mbappé anaingia kwenye fainali hizi akiwa tayari na historia ya kuiongoza ufaransa kutwaa ubingwa wa dunia mwaka 2018 akiwa na miaka 19 tu kisha akairudisha tena kwenye fainali mwaka 2022.

Nje ya uwanja Mbappe amesaini mikataba mipya ya kibiashara ikiwemo ushirikiano na kampuni ya hoteli ya Fairmont Hotels & Resorts pamoja na kampuni ya bima ya afya ya Alan, ambako si balozi tu bali pia mwekezaji.

2. Lionel Messi 

Akiwa na umri wa miaka 38 kuelekea 39, Lionel Messi bado hajashuka kwenye jukwaa la wakubwa. Nahodha huyo wa Argentina anashika nafasi ya pili kwa mapato ya Dola a Marekani milioni 140 (zaidi ya Sh364 bilioni) kiasi kinachoonyesha kuwa hata miaka inapokwenda, thamani yake sokoni na kimichezo bado haijapoa.

Kombe la Dunia 2026 linampa halimpi Messi sura ya kuwa miongoni mwa wanasoka wanaolipwa zaidi bali mchezaji mwenye rekodi ya kushinda mabao mengi zaidi katika mashindano hayo akiwa na mabao 21.

Mbali na kuwa moja ya wanasoka wanaolipwa zaidi Forbes inamtaja Messi kama mwanasoka kati ya wanasoka wachache wenye hadhi ya ubilionia akiwa na utajiri wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 1.1 za Marekani.

Messi pia anamikataba ya kibiashara na kampuni za Adidas na Michelob Ultra, ishara kwamba hata nje ya uwanja, jina lake bado ni dhahabu.

1. Cristiano Ronaldo 

Na juu ya wote, kama ilivyozoeleka kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, anasimama Cristiano Ronaldo. 

Kuna msemo unasema kadiri divai inavyozidi kukaa kwa muda mrefu basi ndivyo thamani yake inazidi kuongezeka, basi huyo ndiye Cristiano Ronaldo.

Licha ya kuwa na umri wa miaka 41, nahodha huyo wa Portugal ndiye mchezaji anayelipwa zaidi kwenye Kombe la Dunia 2026, akiwa ameweka kibindoni Dola za Marekani milioni 300 ndani ya miezi 12 iliyopita fedha inayokadiriwa kuwa zaidi ya Sh780 bilioni za kitanzania. 

Ronaldo ndiye mwanamichezo pekee aliyevuka Dola za Marekani bilioni 2 za mapato ya maisha akiwa bado hajastaafu akimpiku bondia wa ngumi za kulipwa Floyd Mayweather. Picha | Football365

Forbes inamtaja Ronaldo si tu mchezaji anayelipwa zaidi kwenye soka, bali ndiye mwanasoka tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa Dola bilioni 1.2 za Marekani duniani bila kujali michezo.

Ronaldo ndiye mwanamichezo pekee aliyevuka Dola za Marekani bilioni 2 za mapato ya maisha akiwa bado hajastaafu akimpiku bondia wa ngumi za kulipwa Floyd Mayweather. 

Lakini licha ya mafanikio aliyonayo kwenye soka na kubeba karibu kila taji linalowezekana katika soka la klabu na ngazi ya taifa bado kuna kitu kimoja kinakosa kwenye kabati lake la mataji nalo ni Kombe la Dunia. 

Katika msimu huu Ronaldo aliingia kwenye kombe la sita la maisha yake akiliwinda taji hilo kwa matamanio makubwa lakini juhudi hizo hazikufua dafu mara baada ya Ureno kupokea kipigo cha bao moja kwa bila kutoka kwa Spain katika hatua ya mtoano wa taji hilo ambalo kwa mujibu wa Ronaldo itakuwa ndio mara ya mwisho kuonekana akiwa katika jezi ya taifa ya Ureno.

Kwa sasa Ronaldo ndiye nyota maarufu zaidi akiwa na zaidi ya wafuasi bilioni moja katika mitandao ya kijamii ikiwemo mtandao wake wa Istagram ambapo ndiye binadamu mwenye wafuasi wengi zaidi akiwa na wafuasi milioni 673. 

Ama hakika unaweza ukasema Ronaldo si mcheza soka tu bali ni chapa ya kibiashara ndani na nje ya uwanja. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
18 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
18 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Msemaji Geita: Vijana msikurupuke kuja Katoro

Msemaji Geita: Vijana msikurupuke kuja Katoro

Nukta TV

Magonjwa haya matano yanayoongoza kwa kuua watu duniani

Magonjwa haya matano yanayoongoza kwa kuua watu duniani

Nukta TV

Mambo yakuzingatia kabla ujawasha gari lako asubuhi

Mambo yakuzingatia kabla ujawasha gari lako asubuhi

Nukta TV