Uzushi: Rais Samia hakupata madhara baada ya kuchomwa chanjo ya Corona

August 2, 2021 1:33 pm · TULINAGWE ALSON
Share
Tweet
Copy Link
  • Wapotoshaji wamemzushia Rais kupata madhara baada ya kuchomwa chanjo ya Corona.
  • Hakuna madhara yaliyoripotiwa kwa Rais baada ya kupata chanjo Julai 28. 
  • Watanzania watakiwa kujilinda dhidi ya habari za uzushi.

Dar es Salaam. Julai 28, 2021 Raisi Samia alipata chanjo ya Corona aina ya Johnson & Johnson wakati wa uzinduzi wa zoezi la kitaifa la utoaji chanjo kwa hiari.

Uzinduzi huo ulifanyika baada ya Tanzania kupata msaada wa dozi milioni 1 za chanjo hiyo kutoka Marekani kupitia mpango wa chanjo wa Umoja wa Mataifa (COVAX).

Hata hivyo, baada ya Rais kupata chanjo hiyo, wapotoshaji wameibuka na kudai kuwa mara baada ya mkuu huyo wa nchi kupatiwa chanjo hiyo alipata madhara mbalimbali, jambo ambalo siyo la kweli.

Habari ya uzushi kuhusu suala hilo iliwekwa katika mtandao wa Youtube huku picha inayomuonyesha Rais Samia akiwa ameshikiliwa na askari wa jeshi akipelekwa kwenye gari la wagonjwa. 

Habari picha hiyo imebeba kichwa “KILICHOTOKEA BAADA YA RAIS SAMIA KUCHOMWA CHANJO YA CO…”

Picha ya uzushi inayomhusu Rais Samia. Picha | Mtandao.

Ukweli wa habari hiyo ni upi?

Kwa kutumia zana za kidijitali ikiwemo “Google Image”, timu ya NuktaFakti imebaini kuwa picha hiyo haipo mtandaoni na hakuna tukio kama hilo.

Rais hakupata madhara yoyote baada ya kupatiwa chanjo na aliwahimiza Watanzania kupata chanjo hiyo kwa sababu ni salama.

“Nenda leo Moshi, nenda Arusha, nenda Kagera hata Dar es Salaam, uonane na zile koo ambazo wameshaguswa na haya maradhi, wana maneno ya kukuambia na kama wangeweza wote wangekuwa leo hapa kutaka kuchanja kuepukana na ile hasara waliyoipata,” alisema Rais Samia muda mfupi kabla ya kupatiwa chanjo hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kuthibitisha kuwa huo ni uzushi, siku hiyo hiyo, Rais aliendelea na majukumu yake ikiwemo kutembelea hospitali ya jeshi ya Lugalo ya jijini Dar es Salaam. Na sasa yuko katika ziara nchini Rwanda.

Ili kupata taarifa sahihi za Corona Tanzania, Watanzania wanashauriwa kutumia vyanzo sahihi ikiwemo Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW