Maradhi yalivyochangia kukua kwa ubunifu, ujasiriamali Tanzania

December 30, 2021 8:17 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Vijana wabunifu waibuka na suluhu za changamoto za jamii baada ya Uviko-19. 
  • Wajasirimali wabuni mbinu mpya za kukuza biashara.
  • Wadau washauri vijana wabunifu kuwezeshwa kimtaji, mikopo.

Arusha. Wakati biashara na kampuni zinazochipukia (startups) zikifunga au kupunguza shughuli zao kutokana na athari za janga la Corona (Uviko-19), kwa baadhi ya vijana wabunifu hiyo ilikuwa ni fursa. 

Wameitumia changamoto ya Uviko-19 kukuna vichwa na kuibuka na suluhu mbalimbali kukabiliana na matatizo ya kijamii yaliyosababishwa na ugonjwa huo ambao bado unaitesa dunia kwa sasa.

Wakati Uviko-19 unaingia Tanzania Machi 2020, baadhi ya vijana walikata tamaa kutokana na kupoteza ajira na kukosa kipato kwa ajili ya kuendesha maisha yao. Lakini baadhi walikomaa na kuwa tofauti. 

Frank Kisamo ni miongoni mwa vijana ambao waliamua kuanzisha kampuni (startup) ili kutatua changamoto ya upatikanaji wa mbolea kwa wakulima wadogo hasa wa bustani za nyumbani.

Frank na wenzake wanne ambao ni wakazi wa Mkoa wa Arusha walitumia changamoto hiyo kuunda kampuni ya ‘KSM organic fertilizer’ ya kutengeneza mbolea mbadala inayotokana na kinyesi cha ng’ombe, mabaki ya vyakula na mimea hai.

“Kwa hiyo tukaja na startup hii ambayo imeanza kukua sana. Kipindi cha Corona tuliweza kupata wateja wengi ambao walikuwa wanahitaji kuanzisha bustani na wale ambao walikuwa wanapata changamoto kutokana na bei kuwa juu,” anasema Frank.

Maradhi ya Uviko-19 yalisababisha uhaba wa mbolea ulimwenguni ikiwemo Tanzania kutokana na kuathiri shughuli za viwanda vinavyozalisha pembejeo hiyo muhimu kwa wakulima. 

Hali hiyo ilisababisha bei ya mbolea kupanda kuanzia mwaka jana na hata baadhi ya wakulima kukosa kabisa mbolea hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao yao.

Frank anasema mbolea hiyo mbadala imekuwa msaada siyo tu kwa watu wanaolima bustani nyumbani wakati wa Uviko-19 lakini inatumiwa na wakulima wadogo wadogo kumwagilia kwenye mimea yao shambani kwa sababu iko katika mfumo wa kimiminika.

“Kwa upande wetu imekuwa ni fursa kwa sababu kipindi cha Corona kulikuwa na uhitaji mkubwa wa vyakula ambavyo ni organic, na sisi kama wazalishaji wa mbolea tuliweza kuja na kampeni kuhamasisha jinsi ya kufanya kilimo hai nyumbani,” anasema Frank.

                       

 
Vijana hao ambao ni wahitimu wa vyuo mbalimbali nchini wanatumia teknolojia ya kusindika mbolea hiyo ndani ya mashimo yenye uwezo wa  kuzalisha tani 1 ya mbolea kila mwezi.

Mbolea hiyo husambazwa katika mikoa mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Pwani na hivyo kujipatia kipato kuendesha maisha huku wakiboresha maisha ya wananchi wanaofanya kilimo.

“Kampuni hii imetusaidia tumeweza kunufaika, tumeweza kujitangaza na kuwa miongoni mwa kampuni bora kwa mwaka 2021. Pia tumeweza kutunukiwa tuzo ya “Best Startup of the year”. Unaweza ukaona ndani ya mwaka mmoja tumeweza kutatua matatizo ya wakulima wengi,” anasema kijana huyo.

Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo, katika msimu wa mwaka 2020/21 hadi kufika April 2021 uzalishaji wa mbolea kutokana na viwanda vya ndani ulifikia tani 32,239 huku tani 426,572 ziliagizwa toka nje. 

Mahitaji halisi ya mbolea kwa msimu wa mwaka 2020/21 yalikuwa tani 718,051. 

Hii ina maana kuwa hadi kufika April 2021 viwanda vya ndani vilizalisha takribani asilimia 5 ya mahitaji ya mbolea, na kuifanya Tanzania kutumia takriban Dola za Marekani milioni 200 (Sh463.8 bilioni) kwa mwaka kuagiza mbolea za viwandani kutoka nchi za nje. 

Wabunifu kama Frank wakiwezeshwa kwa teknolojia za kisasa wanaweza kusaidia kupunguza tatizo la upatikanaji wa mbolea hata katika kipindi cha majanga makubwa kama Uviko-19.


Zinazohusiana


Uviko-19 yawaibu wataalam wa bustani

Wakati baadhi ya vijana wakiangazia mbolea mbadala, wengine wameamua kuwasaidia wananchi kulima bustani za mboga mboga katika maeneo wanayoishi ili kukidhi mahitaji ya bidhaa hizo muhimu za afya ambazo zinahitajika zaidi kipindi hiko cha Uviko-19.

Changamoto hiyo ikawaibua vijana wengine mkoani hapa ambao wameanzisha kampuni ya Kwokote Enterprises Llimited inayowasaidia watu kulima na kutunza bustani nyumbani.

“Kampuni hii imeanzishwa baada ya kuona wakati wa Uviko-19 kulikuwa na uhitaji mkubwa sana watu kupata vyakula na lishe bora,” anaeleza mmoja wa waanzilishi wa kampuni hiyo, Kennedy Kamondo. 

Kampuni hiyo, ambayo ni zao la Uviko-19, inatekeleza mpango unawasaidia vijana ambao wako mtaani waliosomea kilimo kuwasaidia watu kwenye maeneo yao kuweza kutengeneza bustani hizo kwa utalaam na kuwahamasisha kulima kwa wingi mboga mboga.

Kennedy anasema kampuni hiyo imeajiri zaidi ya vijana watano ambao hujipatia kipato kwa kutoa ushauri wa kutengeneza bustani kwa wakazi wa Arusha.

Wataalam wa afya ikiwemo Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC) wanashauri  watu kuzingatia ulaji unaofaa kwa kuzingatia makundi matano ya vyakula ikiwemo mboga mboga ili kujenga kinga ya mwili na kukabiliana na maambukizi ya magonjwa mbalimbali hususani katika kipindi hiki cha maambukizi ya ugonjwa wa Covid -19.

TFNC imetaja makundi hayo ya vyakula ambayo ni vyakula vya asili ya nafaka, mizizi, ndizi mbichi, kundi la pili ni vyakula vya asili ya wanyama na jamii ya mikunde, kundi la tatu ni mboga mboga, kundi la nne ni matunda na kundi la tano ni sukari, mafuta na asali.

Jukwaa la Kisomo limekuwa ni kiungo muhimu kwa wanafunzi Tanzania kujipatia maarifa na ujuzi wakiwa mtandaoni. Picha| Kisomo App.

Hata wakati startups nyingine zikianzishwa wakati wa Uviko-19, zilizokuwepo kabla ya janga hilo ilikuwa ni wakati wa kupambana kuhakikisha zinaendelea kuwepo katika soko la ushindani na kutoa huduma kwa namna tofauti ili kutokuwapoteza wateja.

Mkurugenzi wa kampuni jamii ya Smartcore inayomiliki programu tumishi ya Kisomo, George Kitomari anasema kabla ya Uviko-19 kuingia Tanzania programu yao ilikuwa haijaanza kutumika mtandaoni lakini baada ya janga hilo wamelazimika kubadili mfumo wa utendaji ili kubaki sokoni.

“Wakati Kisomo inaanza Kisomo ilikuwa inapatikana offline (nje ya mtandao) ilikuwa lazima twende shuleni lakini baada ya Corona kutokea tukasema tutengeneze namna ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaendelea kusoma hata wanapokuwa nyumbani,” anasema Kitomari.

Jukwaa hilo la Kisomo inawasaidia wanafunzi kusoma kwa urahisi kupitia video, majaribio pamoja na katuni . Pia inawasaidia walimu kufuatilia wanafunzi wanavyojifunza na kuboresha ufundishaji wao jambo lililofanya Uviko-19 kuwa fursa.

“Uelewa wa kutumia teknolojia ya Kisomo uliongezeka zaidi na tukapata matokeo chanya walianza kutumia jukwaa letu kwa sababu hakukuwa na mbadala mwingine,” anasema.

Hata hivyo, kampuni hiyo haikufaidika kimapato kwa sababu walikuwa wanatoa huduma bure ili kuwawezesha watu wengi kutumia huduma zao ili kujiimarisha kiteknolojia.

“Kwa sababu tulilazimika kutoa huduma hizi bure. Baada ya hali kuwa imetulia kidogo maana yake biashara zimefunguliwa tumeanza kurejea katika hali ya kawaida,” anasema Kitomari ambaye kampuni yake inapatikana jijini Arusha.

Wakati baadhi ya startups zikianzishwa na kuimarika wakati wa Uviko-19, kwa wengine imekuwa tofauti. Wapo ambao wamefunga biashara au kupunguza shughuli zao.


‘Biashara bila mapato’

Ripoti ya Chama cha Kampuni zinazochipukia Tanzania (TSA) kuhusu athari za Uviko-19 ya mwaka 2020, inaonyesha kuwa asilimia 65 ya startups za Tanzania  mapato yake yalipungua kwa zaidi ya asilimia 50 wakati wa janga hilo mwaka jana.

Pia asilimia 2.5 ya startups zinazojihusisha na uingizaji na usafirishaji bidhaa nje ya nchi zilishindwa kufanya shughuli zake kutokana na vikwazo vya usafiri kukabiliana na Uviko-19. 

Licha ya changamoto hizo, ripoti hiyo iliyotolewa hivi karibuni inaonyesha kuwa startups tatu kati ya 10 zimeimarika huku asilimia 30 ya kampuni hizo zikipata ongezeko la mapato katikati ya janga la uviko-19.

Haikuwa rahisi

Mafanikio waliyopata vijana wabunifu na startups hizo pia yametokana na kusaidiwa kimawazo na kifedha na wadau wa teknolojia vikiwemo vituo atamizi (hubs) jijini hapa. 

Meneja wa kituo atamizi cha Obuntu Hub, John Mushi anasema wamewasaidia  vijana wabunifu na startups wakati huu wa Uviko-19 kwa kuwapatia mafunzo ya mtandaoni ya jinsi ya kuendesha biashara wakati majanga.

“Tumeanzisha programu ya kuwashauri wajasiriamali namna ya kusimamia matumizi ya fedha katika biashara zao hasa kipindi cha Uviko-19 lakini baada ya Corona kupita,” anasema Mushi.

Anasema njia nyingine iliyosaidia kuzivusha salama baadhi startups ni kuzikutanisha na washauri wa masuala ya biashara ili kuwawejengea uwezo wa kumudu athari za Corona na kuendelea kutoa huduma kwa jamii.

Ripoti ya TSA inashauri kuwa hatua zinapaswa kuchukuliwa ili kuzisaidia startups kuendelea na biashara ni pamoja na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa kampuni hizo, wajasiriamali na wabunifu wa teknolojia ili waweze kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao wakati wa Uviko-19.

Pia kupunguza na kuziongezea muda wa kulipa kodi mpaka zitakapoimarika tena na kuundwa kwa mfuko wa mawasiliano kuzisaidia wakati wa majanga makubwa kama Uviko-19.

Makala hii imefadhiliwa na Shirika la maendeleo ya habari la International Media Support (IMS) na Umoja wa Ulaya (EU).

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
23 Jun, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
24 Jun, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
24 Jun, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Baba Levo: Wazo la kuongeza tozo kwenye bodaboda litolewe, tuleteeni watu wa tungi

Baba Levo: Wazo la kuongeza tozo kwenye bodaboda litolewe, tuleteeni watu wa tungi

Nukta TV

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Mwanzo mwisho mapokezi ya Rais wa Namibia Netumbo Nandi Ikulu Dar es Salaam

Nukta TV

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Sikia kisa cha bibi wa Mbagala, chanzo Jaji Mkuu Masaju kupanda cheo

Nukta TV