Ni panga, pangua: Rais Samia afumua baraza la mawaziri Tanzania
- Ateua mawaziri wapya watano.
- Mawaziri wanne watupwa nje akiwemo Prof Kabudi.
- Awabadilishia wizara mawaziri tisa.
Dar es Salaam. Huenda leo baadhi ya watu watalala na maumivu au tabasamu baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kutimiza ahadi yake ya kulifumua na kulisuka upya Baraza la Mawaziri aliyoitoa hivi karibuni.
Rais Samia leo Januari 8, 2021 amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri kwa kuwabadilisha baadhi ya mawaziri na manaibu mawaziri, kuwapumzisha na kuingiza wapya akiwemo Nape Nnauye ambaye anaenda kuongoza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi alidokeza hayo Jumanne Januari 4, 2022 Ikulu ya Dar es Salaam wakati akipokea taarifa ya Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19.
Alisema baada ya kukaa kwenye nafasi hiyo miezi nane,amewasoma mawaziri na utendaji wao hivyo ametoa orodha mpya ya wateule ambao anaona watamsaidia kuwaletea wananchi maendeleo.
Mawaziri Wapya
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga akitangaza mabadiliko hayo leo Ikulu jijini Dar es Salaam, amewataja mawaziri wapya watano walioteuliwa kuwa ni Nape Nnauye ambaye anaenda kuongoza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Hamad Masauni (Mambo ya Ndani) na Dk Pindi Chana ambaye amekabidhiwa Wizara iliyopo Ofisi ya Waziri Mkuu inayoshughulikia Sera Bunge na Uratibu.
Pia aliyekuwa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjelina Mabula amekuwa waziri wa wizara hiyo na Husein Bashe amekuwa Waziri wa Kilimo.
Katika orodha hiyo, Nape na Dk Chana wanaingia kwa mara ya kwanza katika Baraza hilo tangu Rais Samia aingie madarakani Machi 17 mwaka huu.
Pia uteuzi mwingine umefanyika kwa manaibu mawaziri wapya katika wizara tano akiwemo Mbunge wa Dodoma Mjini, Anthony Mavunde ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Kilimo akichukua nafasi ya Bashe, Jumanne Sagini (Mambo ya Ndani) na Dk Lemomo Kiruswa ambaye anaenda Wizara ya Madini akichukua nafasi ya Prof Shukrani Manya.
Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa Rais mstaafu wa Tanzania, Jakaya Kikwete ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Atupele Mwakibete anaenda Ujenzi na Uchukuzi akichukua nafasi ya Mwita Waitara.
Waliotemwa katika baraza hilo
Mawaziri wanne waliokuwa katika Baraza la Mawaziri wamewekwa pembeni akiwemo aliyekuwa Waziri wa Ardhi nchini Tanzania, William Lukuvi na aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Geoffrey Mwambe, aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo nao wameondolewa katika baraza hilo.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
Waliobadilishiwa wizara
Pia, Rais Samia amewabadilisha na kuwahamisha mawaziri katika wizara tisa.
Mawaziri waliohamishwa ni Profesa Adolf Mkenda amepelekwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia akitokea Kilimo, Dk Doroth Gwajima (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu) baada ya wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kugawanywa.
Mohamed Mchengerwa aliyekuwa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora amepelekwa Utamaduni, Sanaa na Michezo huku Dk Ashatu Kijaji akipelekewa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuchukua nafasi iliyoachwa na Mwambe.
Awali Dk Kijaji alikuwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Jenista Mhagama aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Kazi, Uratibu na Bunge amehamishiwa wizara ya Nchi Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), Ummy Mwalimu anaenda Wizara mpya ya Afya akitokea Tamisemi.
Aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene anakuwa Waziri wa Katiba na Sheria huku Profesa Joyce Ndalichako anaenda Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu akitokea Wizara ya Elimu na Innocent Bashungwa anaenda Tamisemi.
Manaibu waziri waliohamishiwa wizara ni pamoja na; Khamis Khamis (Muungano na Mazingira), Hamad Chande (Fedha na Mipango) na Mwanaid Khamis (Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu).
Latest