Rais Samia awapangia kazi mpya Profesa Kabudi, Lukuvi
- Ni baada ya kuwaondoa kwenye Baraza la Mawaziri
- Watapewa kazi maalum Ikulu ikiwemo kuwasimamia mawaziri.
- Prof Kabudi kuongoza mashauriano ya Serikali na taasisi za kimataifa.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema aliamua kuwaondoa aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na William Lukuvi wa Nyumba, Ardhi na Maendeleo ya Makazi kwenye Baraza la Mawaziri ili awe nao karibu kwa ajili ya kumsaidia majukumu maalum Ikulu.
Ufafanuzi huo wa Rais Samia unakuja baada ya kufanya mabadiliko madogo ya Baraza la Mawaziri Januari 8, 2022 ambapo aliteua mawaziri wapya watano, mawaziri tisa kuwabadilishiwa wizara huku akiwaweka kando mawaziri wanne akiwemo Prof Kabudi na Lukuvi.
Wengine ambao hawakutajwa katika mabadiliko hayo ni aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji, Geoffrey Mwambe.
Rais Samia aliyekuwa akiwaapisha mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu Ikulu jijini Dodoma leo Januari 10, 2022 amesema Prof Kabudi na Lukuvi umri wao umeenda hivyo atakaa nao karibu ili wamsaidie baadhi ya majukumu ikiwemo kuwasimamia mawaziri waliopo sasa kwa sababu wana uzoefu wa muda mrefu serikalini.
“Nataka niseme jambo moja tu nina kaka zangu wawili William Lukuvi na Kabudi ukiwatizama hawa age (umri) yao kama yangu na ukitizama niliowateua hamfanani kabisa. Kwa hiyo kaka zangu wawili hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisamamie kuwasimamia nyie,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema miongoni mwa majukumu ya Prof Kabudi ni kuongoza timu ya Serikali katika mazungumzo au mashauriana na mashirika au taasisi za kimataifa katika masuala mbalimbali ikiwemo uwekezaji.
“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi nataka nimkabidhi kindakindaki aendelee na kazi hiyo, ila kazi yake kwa sababu haiko kwenye muundo haitangazwi wala nini lakini atasimamia hiyo kazi,” amesema Rais na kubainisha kuwa,
“Mashirika yote, kazi zote zitakazoingia ubia na Serikali Kabudi ataongoza hiyo timu, kwa hiyo yeye ni baba mikataba ni baba negotiation (mashauriano).”
Prof Kabudi aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki amekuwa akipewa majukumu mbalimbali ya kitaifa ikiwemo kujadiliana na wawekezaji katika migogoro mbalimbali inayohusisha Serikali ikiwemo sakata la kampuni ya madini ya Acacia ambapo aliongoza jopo la Serikali katika majadiliano na kampuni ya Barrick Gold.
Majadiliano mengine makubwa aliyowahi kuongoza na kufikia suluhu ni yale yaliyohusu utata wa umiliki katika kampuni ya simu ya Airtel ambapo Bharti Airtel walikubali kuiongezea hisa Serikali hadi kufikia asilimia 49 kutoka asilimia 41 za awali.
Bila kutaja majukumu atakayopewa Lukuvi, Rais amesema naye atakua karibu yake Ikulu ili kumsaidia majukumu atakayopangiwa ikiwemo “kushika kiboko kuwasimamia mawaziri na makatibu wakuu wa wizara.
“Kaka yangu Lukuvi yeye ana kazi na mimi nitaitangaza baadaye lakini namvuta Ikulu kazi yetu ni kuwasimamia nyie kwa sababu nikiwatizama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili wengine mna safari ndefu.
“Mimi na wale tulishastaafu kwa hiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu,” amesisitiza Rais.
Soma zaidi:
- Rasmi: Samia Suluhu Hassan aapishwa kuwa Rais wa Tanzania
- Huyu ndiye Samia Suluhu Hassan, Rais mwanamke wa kwanza Tanzania
- Ni panga, pangua: Rais Samia afumua baraza la mawaziri Tanzania
Amesema wale waliomzushia lukuvi kuwa uanataka kugombea nafasi ya uspika iliyoachwa wazi baada ya Spika Job Ndugai kujiuzulu wafahamu kuwa hana mpango huo na waache kumchafua.
“Wengine wameanza kumletea meseji za ajabu ajabu wakijua atagombania uspika, hatagombania, ana kazi na mimi. Kwa hiyo, hatakuwa spika wala hatagombania msianze kumchafua ametumikia Taifa hili kwa uadilifu kwa mda mrefu muache aende na mimi tumalize kazi atakayopangiwa,” amesema Rais.
Amesema kwa kuanzia, yeye na wateule hao wawili watakutana na mawaziri, manaibu mawaziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara Januari 13 mwaka huu ili kujadili mambo muhimu ya utendaji wa Serikali.
Aidha, ameziagiza wizara ambazo zimegawanywa: Wizara ya Afya na ile ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu kukutana ili kupangiana majukumu na kuanza kazi mara moja.
Latest