Wanahabari watano waliofia ajalini waagwa Mwanza

January 12, 2022 8:04 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Majeneza yenye miili ya wanahabari waliofariki katika ajali ya gari jana Januari 11 inaagwa na kupewa heshima za mwisho katika uwanja wa michezo wa Nyamagana jijini Mwanza. Picha| Mwananchi.


Dar es Salaam. Miili ya wanahabari na dereva wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza waliofariki katika ajali ya gari jana Januari 11 inaagwa na kupewa heshima za mwisho katika uwanja wa michezo wa Nyamagana jijini Mwanza.

Wanahabari hao ni sehemu ya watu 14 waliofariki dunia baada ya gari la waandishi wa habari iliyokuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu.

Waandishi wa habari walipoteza maisha katika ajali hiyo ni Husna Mlanzi kutoka kituo cha televisheni cha ITV, Vanny Charles (Icon), Antony Chuwa, Johari Shani (Uhuru Digital) na Abel Ngapemba ambaye ni Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Mwingine ni Paulo Silanga aliyekuwa dereva ofisi ya mkuu wa mkoa aliyekuwa anaendesha gari lililobeba wanahabari siku ya ajali.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye na viongozi wengine wanawaongoza waombolezaji wakiwemo wanahabari, ndugu na jamaa wa familia waliofiwa kutoa heshima za mwisho kabla ya kila mwili kuzikwa katika eneo lake.


Soma zaidi:


Husna Mlanzi utapumzishwa katika nyumba yake ya milele mkoani Mwanza ambapo watakaosafirishwa kwenda Dar es Salaam ni Maofisa Habari wa Serikali Ngapemba na Msengi.

Mwili wa Johari Shani wa Uhuru Digital atasafirishwa kwenda mkoani Arusha huku mwili wa Anthony Chuwa wa habari leo Digital utasafirishwa kwenda mkoa wa Kilimanjaro. 

Vilio, simanzi na huzuni zimetawala uwanjani hapo wakati taratibu mbalimbali za kuaga miili ya marehemu.

Waandishi waliofariki katika ajali hiyo walikuwa katika ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Gabriel kuelekea Wilaya ya Ukerewe kupitia Bunda kukagua na kupokea miradi ya madarasa yaliyojengwa kwa fedha za Uviko-19. 

Msafara wa magari yaliyobeba miili hiyo imewasili uwanjani asubuhi na kuzunguka uwanja kabla majeneza yaliyobeba miili ya marehemu kushushwa na maaskari wa vikodi vya ukinzi na usalama na kuwekwa eneo maalum iliyoandaliwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW