Hoja maboresho sheria ya vyombo vya habari yaibuka tena msibani Mwanza
- Wanahabari waiomba Serikali kuwaboreshea mazingira yao ya kazi na uhuru wa kujieleza.
- Watoa hoja hizo msibani Mwanza wakiaga miili ya wenzao watano waliofariki ajali ya gari.
- Serikali yaahidi kuipitia na kuiboresha sheria hiyo.
Dar es Salaam. Serikali imesema itaipitia upya na kufanya maboresho ya Sheria ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016 ili ikidhi matarajio na kuondoa mapungufu yanayominya haki za waandishi wa habari ikiwemo uhuru wa kujieleza na mazingira mazuri ya kufanya kazi.
Tamko hilo la Serikali lililotolewa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye leo Januari 12, 2021 baada ya Waandishi wa habari kutumia msiba wa wenzao watano waliofariki katika ajali ya gari kuiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari nchini.
Wanahabari waliofariki ni Husna Mlanzi kutoka kituo cha televisheni cha ITV, Vanny Charles (Icon), Antony Chuwa, Johari Shani (Uhuru Digital) na Abel Ngapemba ambaye ni Afisa Habari Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza walifariki jana baada ya gari lao kugongana na gari ya abiria aina ya Toyota Hiace katika eneo la Nyamikoma, Wilaya ya Busega katika Mkoa wa Simiyu.
Wanahabari hao walikuwa kwenye msafara wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza (RC), Robert Gabriel uliokuwa unaelekea wilayani Ukerewe kukagua na kuzindua madarasa yaliyojengwa na fedha za Uviko-19.
Majeneza yenye miili ya wanahabari waliofariki katika ajali ya gari jana Januari 11 inaagwa na kupewa heshima za mwisho katika uwanja wa michezo wa Nyamagana jijini Mwanza. Picha| Mwananchi.
Waziri Nape ambaye ameanza majukumu katika wizara hiyo wiki hii amesema tangu kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo, yapo mambo ambayo yameibuka yanayohitaji kurekebishwa ili vyombo vya habari viwe huru.
“Ninajua kwa sababu ilitungwa na binadamu yawezekana yapo mapungufu ya hapa na pale. Rais Samia alishaagiza tuyapitie mapungufu hayo tutarekebisha na kuhakikisha inakidhi matarajio yale ambayo wanahabari wanayataka.
“Kazi ya Serikali ni kuhakikisha tunawatengenezea mazingira mazuri ya nyinyi kufanya kazi. Niwakikishie uhuru wenu, haki zenu ziko salama mikononi mwa Rais Samia na mimi kama mwakilishi wake nitasimamia.”
Amesema sheria hiyo ilitungwa baada kushindikana kwa miaka 23 lengo moja kubwa la kwanza ilikuwa ni kuifanya tasnia ya habari iwe taaluma inayoheshimika ili haki za waandishi wa habari pia ziheshimike.
“Najua katikati kulikuwa na kusua sua kutekeleza sheria hii nataka niwahakikishie wanahabari nimerudi nyumbani kuisimamia sheria hii na tutaitekeleza haki zenu zitalindwa,” amesisitiza Waziri Nape aliyekuwa akizungumza katika viwanja vya Nyamagana mkoani Mwanza leo wakati wa kuaga miili ya waandishi wa habari waliofariki katika ajali hiyo.
Awali viongozi wa wanahabari nchi waliokuwa wakitoa salamu katika tukio hilo wameiomba Serikali kuboresha sheria na mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko ameiomba wizara yenye dhamana kurekebisha kasoro zilizopo ikiwemo kuwapa uhuru wao wa kazi.
“Nitumie fursa hii kumwomba Waziri Nape Nnauye ambaye ndiye muasisi wa Sheria ya Huduna ya Habari ya mwaka 2016 kuwezesha waandishi wa habari kufanya kazi katika mazingira bora,” amesema Soko.
Pia ameomba sharti la kiwango cha elimu kwa wanahabari cha angalau diploma, waandishi wanaojiendeleza kielimu waruhusiwe kuendelea kutekeleza majukumu yao kabla ya muda ulioweka kuisha.
Baadhi ya wadau wa habari likiwemo Baraza la Habari Tanzania (MCT) Wanasema kuna baadhi ya vifungu katika sheria hiyo vinavyowanyima wanahabari haki na uhuru wa kuchapisha taarifa mbalimbali.
Aidha, wanapinga kifungo cha sheria hiyo kinachowataka wanahabari kupewa kibali cha kufanya kazi na kuwepo kwa mamlaka inayoweza kuwazuia wanahabari kupewa kibali hicho.
Soma zaidi:
-
Rais Samia atuma salamu za pole vifo vya watu 14 Simiyu
-
Wanahabari watano waliofia ajalini waagwa Mwanza
-
Nape aagiza uchunguzi vifo vya wanahabari misafara ya viongozi wa Serikali
Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Abubakar Karsan naye amesema waandishi wa habari wengi nchini hawalipwi mishahara na stahiki zao muhimu.
“Ninapozungumza sasa, hapa mbele yangu wapo waandishi wa habari waliolala ambao leo tunawaaga hawajalipwa mishahara yao kwa miaka miwili. Kama yupo aliyelipwa, basi amelipwa miezo minane iliyopita,” amesema Karsan.
Amesema usimamizi duni wa mamlaka katika utekelezaji wa sheria hiyo ni miongoni mwa sababu zinazotoa mwanya kwa waajiri kutotimiza wajibu wa malipo sahihi na stahiki kwa watumishi wa vyonbo vya habari.
“Waajiri hawalipi mishahara kwa madai ya kukosa fedha; lakini tunakutana nao baa. Fedha ya kwenda baa zinapatikana isipokuwa ya kuwalipa mishahara waandishi,” amehoji Karsan.
Rais SamiaSuluhu Hassan kutana kuzungumza na waandishi wa habari Ikulu, Dar es Salaam Juni 28, 2021 aliahidi Serikali kuboresha maslahi ya wanahabari ikiwemo kufanya maboresho ya sheria na kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi wao.