Tabasamu: Mikopo kwa sekta binafsi yaongezeka Tanzania

January 14, 2022 2:16 pm · Wilson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeongezeka kwa asilimia 7.8 katika mwaka ulioishia Desemba 2021 kutoka asilimia 5.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2020
  • Ukuaji huo unachagizwa na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanywa na serikali  ikiwemo kuboresha mazingira ya kibiashara na sera zinazosimamia  sekta ya fedha.
  • Sehemu kubwa ya mikopo imeelekezwa katika  shughuli za watu binafsi na biashara

Dar es Salaam. Takwimu mpya za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 7.8 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita, huku sehemu kubwa ya mikopo hiyo ikielekezwa katika shughuli za watu binafsi na biashara. 

Ripoti ya Mapitio ya Uchumi ya mwezi Desemba 2021 (Economic Monthly Review) iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hivi karibuni imeeleza kuwa mikopo kwa sekta binafsi imeongezeka kwa asilimia 7.8 katika mwaka ulioishia Desemba 2021 ikilinganishwa na asilimia 5.6 katika kipindi kama hicho mwaka 2020. 

Hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.2 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

BoT imeeleza katika ripoti hiyo kuwa ahueni endelevu ya ukuaji huo inatokana na juhudi mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali ikiwemo kuboresha mazingira ya kibiashara na sera zinazosimamia sekta ya fedha.

“Ahueni endelevu ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa inachangiwa na hali ya kifedha kukidhi mahitaji, vile vile  juhudi zinazoendelea kufanywa na serikali kuboresha mazingira ya kibiashara,” inasomeka sehemu ya ripoti hiyo inayopatikana pia katika tovuti ya BoT.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa ukuaji  wa mikopo kwa sekta binafsi unatarajiwa kuendelea kukua kwa kiwango cha hadi asilimia 10.6  kama malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2021/22 yatatimia ikiwa ni utekelezaji wa sera zilizowekwa hivi karibuni na BoT ambayo ni kukuza kiwango cha mikopo na kupungua kwa riba.


Soma zaidi:


Ukuaji wa mikopo katika shughuli zote kubwa za uchumi unaendelea kuongezeka, isipokuwa kwa shughuli za kilimo, ujenzi, usafiri na mawasiliano. 

“Katika kipindi kilichoishia Novemba 2021, ukuaji wa mikopo ulishuhudiwa zaidi katika shughuli za watu binafsi, viwanda na biashara,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.  

Sehemu kubwa ya mikopo hiyo ilielekezwa katika shughuli za watu binafsi kwa asilimia 19.4 ikifuatiwa na biashara (asilimia 14.2) na sekta ya viwanda  kwa asilimia 7.1.

Mikopo inayoelekezwa katika sekta binafsi imekuwa chachu ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi nchini kwa sababu hutumika kutunisha mitaji na ununuzi wa malighafi na utoaji huduma katika shughuli mbalimbali. 

Hata wakati mikopo kwa sekta binafsi ikiongezeka, riba inayotozwa na benki za biashara imeongezeka pia, jambo ambalo linaweza kuwaumiza wakopaji na kuzifaidisha zaidi benki za biashara nchini. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, riba iliyotozwa na benki kwa mwaka ulioishia Novemba  2021 ilikuwa asilimia 6.8 ikipanda kutoka asilimia 6.6 katika  mwaka ulioishia Novemba  2020 huku kiwango cha riba kwa wateja maalumu wa benki kikibaki kama kilivyo kwa asilimia 9.7.

Benki kutoza riba kubwa, kunaweza kupunguza kasi ya wananchi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo yao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW