Uchafuzi wa hewa waangamiza mamilioni duniani
Dar es Salaam. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) limesema watu 9 kati ya 10 wanapumua hewa iliyochafuliwa duniani, hali ambayo kila mwaka inasababisha vifo vya mapema vya watu milioni 7 huku ukihimiza udhibiti wa vyanzo vya uchafuzi wa hewa.
Kati ya vifo hivyo, 600,000 ni vya watoto, na idadi hiyo inaweza kuongezeka maradufu ifikapo mwaka 2050.

Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres amesema kuwa sehemu kubwa ya vifo vinavyohusiana na jambo hilo vinatokea katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati, na katika vitongoji masikini vya mataifa tajiri.
Guterres amekumbusha kuwa uchafuzi wa hali ya hewa ni “dhihirisho la wazi la ukosefu wa usawa ulimwenguni.”.
Amesema umaskini unalazimisha watu kuishi karibu na vyanzo vya uchafuzi wa mazingira, kama vile viwanda na barabara na pia husababisha watu bilioni 3 kuendelea kutumia mafuta kisukuku au mafuta ya taa kwa kupikia na kwa kupasha nyumba joto na kuwasha taa”.
Uchafuzi wa mazingira siyo tu unaharibu afya zetu, lakini pia unachangia kuongeza shida ya hali ya hewa, ingawa amesisitiza kuwa kuna suluhisho za kukabiliana na changamoto hii.
Guterres alitoa angalizo hilo Septemba 7, 2021 katika siku ya kimataifa ya “hewa safi kwa ajili ya anga ya bluu” ambapo amehizihimiza nchi zote kuongeza juhudi zao za kuboresha hali ya hewa na kuhakikisha udhibiti bora wa vyanzo vya uchafuzi wa hewa.
Wakati huo huo, Guterres ametaka kuwe na viwango vikali vya kudhibi kuchafua hewa kunakotokana na magari, mitambo, ujenzi na viwanda, kuondoa matumizi ya makaa ya mawe na kuwekeza katika nishati mbadala badala ya mafuta kisukuku.
“Ikiwa tutachukua hatua hizi, tunaweza kuokoa hadi maisha ya watu milioni 150 katika karne hii na kusaidia kusafisha mazingira yetu,” amesema.
Latest
