UN: Tukiigeuza dunia kuwa dampo la taka tunajichimbia kaburi

March 31, 2023 6:33 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Kuna mamia ya madampo ya taka nchini Kenya kubwa zaidi likiwa Dandora mjini Nairobi. Picha | UNEP/Duncan Moore.


  • Imesema taka zina athari kubwa kwa afya za watu na mazingira.
  • Yahimiza kuimarisha kwa mifumo ya urelezaji wa taka. 

Dar es Salaam. Umoja wa Mataifa umesema (UN) umeeleza kuwa ili kukabiliana na athari mbaya za taka kwa afya za binadamu, uchumi na mazingira kila mtu ana wajibu wa kuzuia, kupunguza utupaji taka na kuhimiza mabadiliko ya mtazamo wa jamii kuelekea uchumi wa mzunguko.

Ujumbe huo umetolewa Machi 30, 2023 wakati dunia kwa mara ya kwanza ikiadhimisha “siku ya kimataifa ya kutozalisha na kutotupa taka kiholela”.

“Wakati umefika wa kuacha kugeuza sayari dunia dampo na badala yake kila mtu azingatie matumizi ya tena na tena ya bidhaa kadri inavyowezekana kwani kuigeuza sayari kuwa dampo tunajichimbia kaburi,” amesema Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hiyo. 

Amesema ni wakati wa kuamka na kusongesha harakati za kiuchumi zisizozalisha taka na walaji wajenge tabia ya kutumia bidhaa tena na tena kabla ya kuzitupa ili kupunguza kiwango cha taka kinachozalishwa.

“Mgogoro wa taka unadhoofisha uwezo wa dunia wa kudumisha maisha. Taka hugharimu uchumi wa dunia mabilioni ya dola kila mwaka. Ni wakati wa kutafakari juu ya madhara ambayo yanaletwa na taka katika sayari yetu  na kusaka suluhu ya vitisho hivi vikali,” amesema Guaterres. 

Siku ya kutozalisha na kutotupa taka kiholela imeanzishwa kupitia azimio la Baraza Kuu la UN lililofuata maazimio mengine kuhusu taka, ikiwa ni pamoja na dhamira ya Baraza la Mazingira la UN la Machi 2, 2022 kuendeleza makubaliano ya kimataifa ya kukomesha uchafuzi wa taka za plastiki. 

Siku hii ya kimataifa inaratibiwa kwa pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Mazingira Duniani (UNEP) na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi (UN-Habitat).

Siku hii inatoa wito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na serikali, mashirika ya kiraia, wafanyabiashara, wanazuoni, jamii, wanawake na vijana kushiriki katika shughuli zinazoongeza ufahamu wa mipango ya kutoondoa taka.

Binadamu huzalisha zaidi ya tani bilioni 2 za taka ngumu kila mwaka, ambazo asilimia 45 kati yake hazidhibitiwi ipasavyo.

UNEP inasema bila hatua za haraka, kiwango hicho kitapanda hadi karibu tani bilioni 4 ifikapo mwaka 2050. 

“Taka zinakuja za aina zote na za ukubwa wa aina zote ikiwa ni pamoja na plastiki, uchafu kutoka kwenye madini na maeneo ya ujenzi, vifaa vya elektroniki na chakula. Zinaathiri vibaya maskini, na hadi watu bilioni 4 hawana fursa za maeneo ya kudhibiti taka,” imeeleza UNEP.

Siku ya Kimataifa ya kutozalisha na kutotupa taka kiholela inalenga kuitanabaisha dunia kuhusu athari za taka na kuhimiza hatua za kimataifa katika viwango vyote ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na taka.

“Udhibiti wa taka ni muhimu katika kukabiliana na changamoto za makazi, jinsi tunavyodhibiti changamoto za usafi wa mazingira katika miji yetu na mabadiliko ya tabianchi. Ni muhimu katika kuboresha maisha ya watu kila mahali kudhibiti taka hizo.” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UN-Habitat,  Maimunah Mohd Sharif.

Kwa mujibu wa UNEP, kukuza mipango ya kuondoa taka kunaweza kusaidia kuendeleza malengo na shabaha zote katika Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, ikijumuisha lengo la 11 la kufanya miji na makazi ya watu kuwa jumuishi, salama, yenye mnepo na endelevu na lengo namba 12 la kuhakikisha mifumo ya matumizi na uzalishaji endelevu.

“Tunahitaji kuchukua hatua sasa. Tuna utaalamu wa kiufundi na msukumo wa kufanya uvumbuzi. Tuna maarifa ya kisayansi na ya asili ili kupata suluhisho kwa changamoto ya taka,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP Inger Andersen.

Amesema maadhimisho hayo ya kwanza ya kimataifa ya siku ya kutozalisha na kutotupa taka kiholela ni fursa muhimu ya kuendeleza mipango ya ndani, kikanda na kitaifa ili kuimarisha usimamizi wa taka unaozingatia mazingira na kuchangia katika Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW