Kutokomezwa kwa kemikali ya risasi kwenye petroli kutakavyookoa maelfu ya watoto

November 3, 2021 12:14 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Petroli iliyo na risasi husababisha ugonjwa ya moyo, kiharusi na saratani.
  • Husababisha  vifo milioni 1 vya watoto waliokuwa wanazaliwa kabla ya wakati kila mwaka.
  • Mwaka 2021 ndiyo mwisho wa matumizi wa kemikali hiyo kwenye petroli.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Antonio Guterres amesema kufanikiwa kwa juhudi za kutokomeza matumizi ya kemikali ya risasi katika mafuta ya petroli kutasaidia kuokoa maisha ya watoto milioni 1 kila mwaka duniani. 

Kwa mujibu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), petroli iliyo na risasi husababisha ugonjwa ya moyo, kiharusi na saratani.

Pia inaathiri ukuaji wa ubongo wa mwanadamu hasa kudhuru watoto, huku tafiti zikieleza kuwa hupunguza uwezo mtu wa kufikiri (IQ) wa alama kati ya 5 na 10. 

“Wakati kampeni ya kuondoa kemikali ya risasi ilipoanza (2002), nchi 86 zilikuwa zinatumia petroli yenye kemikali hiyo, lakini leo hakuna nchi hata moja duniani inayotumia,” amesema Guterres.

Amesema kutokomeza kwa kemikali hiyo kutaondosha vifo milioni 1 vya watoto waliokuwa wanazaliwa kabla ya wakati kila mwaka, matatizo ya moyo, kiharusi, saratani na kutalinda uwezo wa akili wa watoto (IQ) ambao ulikuwa unaharibiwa kutokana na kemikali hiyo.

Katika ujumbe wake uliotolewa Agosti 30, 2021 mjini New York nchini Marekani, Guterres amesema zoezi hilo limechukua miaka 20 likisimamiwa na UNEP

Guterres amesema kwa mafanikio haya ni wazi kuwa lolote linawezekana iwapo kutakuwa na ushirikiano wa nchi zote duniani ili kufikia lengo mahususi, akitolea mfano itifaki ya Montreal juu ya vitu vinavyoharibu tabaka la ozoni. 

“Mfano mwingine bora ni Itifaki ya Montreal juu ya vitu vinavyoondoa tabaka la ozoni. Ni lazima sasa tugeukie dhamira ya kumaliza shida tatu kubwa ambazo ni uharibifu wa hali ya hewa, kupotea kwa bayoanuwai na uchafuzi wa mazingira. Tunahitaji kuhama kutoka kwenye matumizi ya mafuta, hadi nishati mbadala. Tunahitaji dunia iendelee kusafiri bila kuwa na uchafuzi wa hewa,” amesema. 

Baada ya kampeni ya miaka 20 matumizi ya mafuta ya petroli yenye kemikali ya risasi yamekoma ulimwenguni kote. Picha| UN News/Daniel Dickinson.

Katibu huyo Mkuu amesisitiza kuwa lazima ulimwengu ufanye mabadiliko kwenye nishati, mifumo ya chakula na fedha ili kuunda ulimwengu wenye kulindana na siyo kuharibu uoto wa asili. 

Kwa mujibu wa UNEP, mwaka wa 2021 umeashiria mwisho wa petroli iliyo na risasi ulimwenguni, baada ya kuchafua hewa, vumbi, udongo, maji ya kunywa na mazao ya chakula kwa sehemu kubwa ya karne.

Kemikali hiyo ilikuwa inaongezwa kwenye petroli ili kuimarisha utendaji wa injini ya gari lakini madhara yake kwa binadamu na mazingira ni makubwa.

Hatua za dharura bado zinahitajika ili kukomesha uchafuzi wa risasi kutoka kwa vyanzo vinginevyo ikiwemo rangi iliyo na risasi, betri zilizo na risasi, na risasi kwenye vitu vinavyotumiwa majumbani.

Kukomesha kwa matumizi ya petroli iliyo na risasi kunalenga kuwezesha kufikia mengi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG’s).

Pia inatoa fursa kwa uboreshaji wa mifumo ya ekolojia, haswa katika mazingira ya mijini, ambayo yameharibiwa na uchafuzi huu wa sumu, imeeleza UNEP. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW