Dk Mwigulu: Hatuhitaji fedha za Azaki zije Serikalini

March 28, 2022 10:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kauli yake ya kuiomba USAID ielekeze Sh3 trilioni za Azaki katika miradi ya kimkakati.
  • Baadhi ya watu wasema Azaki zinastahili kupata fedha hizo.
  • Asema “hatujataka fedha za Azaki zije hazina”.

Dar es Salaam. Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba amesema Serikali haina nia ya kuzichukua takriban Sh3 trilioni za Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) ambazo zimepangwa kutolewa kwa asasi za kiraia (Azaki) za Tanzania. 

Kauli ya Dk Nchemba imekuja wakati kukiwa na mjadala mkali kuhusu kauli yake aliyoitoa Machi 25, 2022 mkoani Dodoma, alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mkurugenzi wa USAID, Kate Samvongsiri akimuomba fedha hizo zielekezwe katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali.

Waziri huyo katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango alisema ni kweli fedha hizo zina umuhimu katika miradi iliyokusudiwa kutekelezwa na azaki lakini zielekezwe katika vipaumbele vya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo sekta za afya, elimu, kilimo ili kuchochea ukuaji wa uchumi.

 

Baadhi ya watu hasa katika mitandao ya kijamii wamesema suala hilo halileti tafsiri nzuri kwa sababu Azaki zinafanya kazi nzuri ya kuboresha maisha ya watu kama inavyofanya Serikali na wakipatiwa fedha hizo zitachochea zaidi kazi zao nchini.

“Ndo hivyo! Yaani NGO pesa zao zinapangiwa matumizi na serikali!,” ameandika Maria Sarungi, mwanaharakati wa haki binadamu wakati akichangia mjadala kuhusu fedha hizo.

Watu wengine wameshauri Serikali ijielekeze katika vyanzo vyake vya mapato kulingana na bajeti inayopangwa kila mwaka kuliko kuchukua fedha hizo.

“Najiuliza tu inakuwaje Serikali inataka chukua pesa zinazotolewa kwa ajili ya asasi za kiraia? Je hizo asasi zitaendeshaje shughuli zake? Yaani pesa ya asasi za kiraia mnazipangia kazi serikali? Hii Inastaajabisha sana,” amesema mtumiaji wa Twitter, @V2Electronic.


Soma zaidi: 


Hata hivyo, Waziri Dk Nchemba katika ukurasa wake wa Twitter leo Machi 28, 2022 amesema kama waziri mwenye dhamana ya fedha alikuwa na wajibu wa kuwaeleza washirika wa maendeleo (USAID) kuhusu mifumo ya bajeti na siyo kuhamisha matumizi ya fedha za Azaki zilizopangwa kutolewa na shirika hilo. 

Amesema kauli yake ililenga kukumbusha kuwa ufadhili huo utakaotolewa na USAID uendane na malengo ya maendeleo ya Tanzania kwa sasa.

“Fedha ambazo washirika wa maendeleo wanazipeleka moja kwa moja kwa Azaki zinasimamiwa na menejimenti/Bodi za Azaki kwa mujibu wa Sheria ya NGO (mashirika yasiyo ya kiserikali). 

“Fedha zinazotumiwa na Serikali zinapaswa kufuata Sheria ya Bajeti na sheria za fedha za umma. Hatujataka fedha za Azaki zije hazina,” amesema waziri huyo.

Aidha, ameziomba Azaki kuwianisha shughuli zao na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Maendeleo wa Miaka mitano (5) ili fedha wanazopata kutoka kwa wafadhili zisaidie kuleta maendeleo ya nchi.

Waziri huyo amewasihi washirika wa maendeleo kuongeza fedha kwa Azaki ili kuimarisha utendaji wao nchini.

USAID imepanga kutoa Sh3 trilioni kwa asasi za kiraia katika kipindi cha miaka mitano ijayo ili kuimarisha utendaji na utekelezaji wa shughuli za kuwasaidia na kuboresha maisha ya wananchi. 

Akijibu ombi la Dk Nchemba, Mkurugenzi wa USAID, Kate Samvongsiri, alisema kuwa wanapenda kushirikiana na Serikali ya Tanzania na watakaa pamoja na kuangalia vipaumbele vya Serikali na kuona namna watakavyoziwezesha.

/
No matches found for this filter
No forex gainers today
No forex losers today
25 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
25 May, 2026
No active movers today
Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

MIKOA 5 YA KIPOLISI INAYOONGOZA KWA MAKOSA BARABARANI

Nukta TV

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

SERIKALI YAKAMILISHA MAZUNGUMZO MRADI WA LIGANGA NA MCHUCHUMA

Nukta TV

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

🔴LIVE: KAPINGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA 2026/2027 BUNGENI.

Nukta TV