Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine wazalisha wakimbizi zaidi milioni 11
- Zaidi ya watu milioni 4.3 wamekimbia nchi yao.
- Wakimbizi wengine milioni 7.1 wametawanywa ndani ya Ukraine.
- UNCR yaimarisha usaidizi wa chakula na malazi kwa wakimbizi.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, (UNHCR) limesema uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umesababisha moja ya ongezeko kubwa na la haraka la watu kutawanywa na janga la kibinadamu katika kipindi cha muda mfupi.
Shirika hilo limesema ndani ya wiki sita pekee zaidi ya watu milioni 4.3 wamekimbia nchi yao na kuwa wakimbizi huku wengine milioni 7.1 wametawanywa ndani ya Ukraine.
UNHCR inashirikiana kwa karibu na mamlaka ndani ya Ukraine ili kuongeza uwezo wa meneo yanayopokea wakimbizi.
Akizungumza na waandishi wa Habari mjini Geneva Uswis hii Aprili 8, 2022 msemaji wa UNHCR Matthew Saltmarsh amesema kutoa misaada bado ni changamoto katika sehemu za nchi ambako kuna mapigano makali.
“Tunaendelea kujitahidi kufikia maeneo yaliyoathirika sana kama vile Mariupol na Kherson kwa usaidizi wa kuokoa maisha kama sehemu ya misafara ya mashirika ya misaada ya kibinadamu.
“Tumechangia misafara minne kama hii chini ya mfumo wa taarifa za kibinadamu, miwili kwa eneo la Sumy, mmoja Kharkiv na mmoja Sieverodonetsk, na kusaidia misafara kadhaa ya ziada kwa msaada wa washirika, na kuweza kufikia watu 15,600 kwa vitu vya misaada,” amesema Saltmarsh.
Soma zaidi:
-
Mjue askari aliyekataa kubeba silaha vitani na kuokoa watu 75 kwenye pambano kali
-
ICC yaelekeza macho yake Ukraine, Urusi ikiendelea na mashambulizi
-
UN yakwaa kisiki kuiwajibisha Urusi uvamizi Ukraine
Msafara wa hivi karibuni zaidi ulikuwa Aprili 6, ambapo UNHCR ilikuwa miongoni mwa wale waliopeleka misaada Sievierodonetsk huko Luhansk, mashariki mwa Ukraine.
“Timu yetu iliweza kutoa taa za sola, mablanketi, vifaa vya usafi, maziwa ya mtoto na maturubai kwa watu 3,000,” amesema msemaji huyo.
UNHCR pamoja na washirika wa mashirika yasiyo ya kiserikali inaendelea kutoa huduma za ulinzi na kuwaelekeza wakimbizi kwenda katika vituo vya mpakani na vituo vya mapokezi.
Watu wapatao 36,000 wamepokea usaidizi kama huo na taarifa katika vituo vya mpakani, vya mpito, na vituo vya kupokea wageni na kupitia simu za dharura. Huduma hizi ni pamoja na usaidizi wa kisheria na usaidizi wa kisaikolojia.
UNHCR pia hutoa huduma za ulinzi karibu na maeneo yenye mizozo, mara tu wanapowasili.
Latest