Hapana: Pombe haizuii maambukizi ya Uviko-19
- Wataalamu wa afya wasema haina uwezo wa kuzuia wala kuponya Uviko-19.
- Watu waonywa kutohusianisha kemikali iliyopo kwenye pombe na vitakasa mikono.
Dar es salaam. Kumekuwepo na dhana potofu kwa baadhi ya watu kuamini kuwa matumizi ya vilevi hususani pombe husaidia kuzuia maambukizi ya Uviko-19 unaoshambulia mifumo ya upumuaji.
Uwepo wa dhana hiyo umetokana na wataalamu wa afya kuhimiza kunawa mikono kwa kutumia vitakasa mikono ambavyo huwa na kemikali inayofanana na ile iliyopo kwenye pombe na hivyo watu kudhani zinaweza kufanya kazi sawa.
Hata hivyo, wataalamu kutoa Shirika la Afya la Kimataifa WHO kupitia kwa Dk Sylvie Briand ambaye ni Mkurugenzi wa Idara inayoshughulika na Magonjwa Hatari ya Kuambukiza (GHI) amesema madai hayo siyo sawa.
“Kunywa pombe hakukuponyi wala kukukinga na Uviko-19,watu wanahusianisha na kemikali iliyopo kwenye vitakasa mikono ambayo si kwa ajili ya kunywa kwani inaweza kusababisha madhara makubwa, ni kwa ajili ya kuosha mikono tu,” anasema Dk Briand.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza( BBC) watu 10 waliripotiwa kupoteza maisha nchini India baada ya kunywa vitakasa mikono Julai 31, 2020.
Utofauti upo wapi?
Unatakiwa kufahamu kuwa kemikali iliyopo kwenye pombe inayotumiwa kama kinywaji na kemikali iliyopo kwenye vitakasa mikono zina utofauti mkubwa.
Kwa mujibu wa tovuti inayotoa taarifa za kitabibu ya Medicine net ya nchini Marekani imeainisha aina nne za kemikali ambazo ni Isopropyl, Methyl, Ethyl, pamoja na Ethanol ambazo hutumika katika mazingira tofauti ingawa zote huwa na viambata vya kilevi.
Zinazohusiana:
Kemikali ya Isopropyl
Kemikali hii hutegenezwa kwa kutumia gesi ya ‘propylene’ na hutumika katika bidhaa za usafi kama dawa na sabuni za kufulia au kuoshea vitu mbalimbali kutokana kuwa na uwezo wa kupambana na bakteria na wadudu waharibifu.
Kemikali hii si ya kunywa kwani kwa mujibu wa Medicine net, mtu anaweza kupata madhara kama shinikizo la juu la damu, kizunguzungu, kutapika au kushindwa kupumua iwapo atakunywa kemikali hiyo.
Kemikali ya Ethyl
Hii ni kemikali inayopatikana katika aina zote za pombe na ni salama kwa kunywewa na binadamu. Kemikali hii hutengenezwa kupitia mchakato wa kuchachusha nafaka au matunda kutegemeana na aina ya pombe inayotengenezwa.
Hivyo ni muhimu kufahamu kuwa pombe haina uwezo wa kukukinga na virusi vya Corona kwa sababu kemikali zilizopo si maalumu kwa kufanya kazi hiyo na ile iliyopo kwenye vitakasa mikono si kwa ajili ya kunywa.
Unaweza kuendelea kujikinga na ugonjwa wa Uviko-19 kwa kupata chanjo, kuepuka mikusanyiko na kuvaa barakoa.
Licha ya kasi ya maambukizi kupungua kutokana na afua zilizochukuliwa bado ugonjwa huu upo na kwa mujibu wa takwimu za WHO za leo Septemba 29, 2022 katika siku saba zilizopita kumeripotiwa maambukizi milioni 2.8 na vifo 8,338 duniani kote.
Latest