Hivi ndivyo Mkoa wa Mwanza ulivyojipanga kukabiliana na Ebola
- Wananchi watakiwa kuondoa hofu kupata maambukizi.
- Timu ya kufuatilia ugonjwa huo yaundwa.
Mwanza. Mwanza ni miongoni mwa mikoa mitano iliyotajwa na Serikali ya Tanzania iliyo katika hatari zaidi ya kupata ugonjwa wa Ebola endapo utaingia nchi, baada ya Uganda kushambuliwa na ugonjwa huo.
Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, Septemba 28, 2022 aliitaja mikoa mingine iliyo katika hatari hiyo ni Kagera, Kigoma, Geita na Mara
Mikoa iliyo katika hatari ya kati ni pamoja na Dar es Salaam, Kilimanjaro, Songwe, Dodoma na Arusha kutokana kuwa na viwanja vya ndege ambavyo vinapokea wageni wa kimataifa.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), hadi kufikia Oktoba 5, 2022, watu 63 wameambukizwa ugonjwa wa Ebola nchini Uganda huku 29 wakifariki dunia.
Baada ya mlipuko huo, Waziri Ummy alisema tayari wamejipanga kuudhibiti ugonjwa huo usiingine nchini na kuwaomba wananchi kuchukua tahadhari kujikinga.
Ugonjwa huo ni miongoni mwa magonjwa yanayosambaa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kwa kula au kugusa mnyama mwenye maambukizi kama nyani, kima, popo na swala.
“Ugonjwa wa Ebola unaenea kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa kwa mfano mate, machozi, damu, matapishi, mkojo na kinyesi. Endapo mtu ataona dalili hizi awahi kituo cha kutolea huduma za afya,” alisema Waziri Ummy, Septemba 28.
“Tunatakiwa kuongeza jitihada za kuzuia ugonjwa wa Ebola, kwani mgonjwa anaweza kuingia njia ambazo siyo rasmi”, @ummymwalimu
pic.twitter.com/bjBbYq4Jd5— Wizara ya Afya Tanzania ?? (@wizara_afyatz) October 4, 2022
Hali ikoje mkoani Mwanza?
Baada ya Mwanza kutangazwa kuwa katika hatari ya kupata ugonjwa huo kutokana na muingiliano wa watu uliopo kati yake na Uganda, baadhi ya wananchi wamekuwa na hofu kuhusu hatma ya afya zao.
Mwenyekiti wa soko la dagaa Kirumba Mwaloni, Elias Daud anasema mwingiliano wa watu kutoka mikoa mbalimbali na nchi jirani ya Uganda kuja kufuata dagaa katika soko hilo ni mkubwa hivyo ni vyema ulinzi ukaimarishwa zaidi mipakani na kwenye maeneo ya vivuko.
“Elimu inahitajika zaidi hasa kwetu sisi wafanyabiashara iwapo tutapokea fedha kupitia kwa mtu mwenye ugonjwa huo hatuwezi kuambukizwa?,” amehoji Daudi.
Wasiwasi huo pia umekuwepo kwa wafanyabiashara wa usafirishaji ikiwemo bodaboda na wanaofanya biashara ya fedha mtandaoni.
Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda Mkoa wa Mwanza, Joseph Msabila ametaja kundi ambalo lipo hatarini iwapo ugonjwa huo utaingia nchini ni la waendesha pikipiki.
“Kwa sababu tunabeba abiria wa aina tofauti na hatujui wanapotokea na kuna abiria wengine unapowapakia wanajiegemeza mgogoni na kama huo ugonjwa unaambukizwa kwa jasho na mate anaweza kuhimili kuwa hai kwa muda gani”, anasema Msabila.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima akizungumza kwenye kikao cha kuweka mikakati ya kujikinga na ugonjwa wa Ebola hivi karibuni. Picha | Mariam John.
‘Waondoe hofu wako salama’
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa katika taarifa yake ya Oktoba 7, 2022 kwa waandishi wa habari ni kuwa mkoa huo tayari umeshaanza maandalizi ya kujikinga na ugonjwa huo.
Dk Rutachunzibwa anasema wameshaandaa vituo maalum kwa wagonjwa watakaobainika na tayari timu ya watalaam wa afya 250 wamepewa mafunzo ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Timu hiyo ina madaktari, wauguzi, maafisa afya, wataalam wa maabara, waratibu wa afya, wahudumu ngazi ya jamii, madereva na timu ya wazikaji.
“Mpaka sasa Mkoa wa Mwanza na nchi kwa ujumla haijathibitisha kuwa na mgonjwa wa Ebola lakini timu za wataalamu wa afya zimeanza kutoa elimu ya kujikinga na ugonjwa huo hasa wakielimisha jamii kuwahi hospitali pale watakapohisi dalili za kuumwa,” anasema Dk Rutachunzibwa.
Ametaja dalili za mgonjwa wa Ebola kuwa ni maumivu ya kichwa, misuli, homa, koo, mwili kuuma, kutapika, kuhara na kutokwa damu sehemu zilizo wazi za mwili wake.
“Mtu mwenye dalili hizo anatakiwa awahi kituo cha afya kwa ajili ya matibabu na iwapo ataenda kubainika na ugonjwa huo atapelekwa kwenye vituo maalum vilivyotengwa kwa ajili ya wagonjwa hao,” anasisitiza Dk Rutachunzibwa.
Kwa Mkoa wa Mwanza tayari imetenga vituo kwenye hospitali za Sekou-Toure, Mkuyuni na Busweli.
Soma zaidi:
- Nusu ya wanafamilia walivyokatwa miguu kwa “ugonjwa wa ajabu”- 1
- Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi
- Simulizi ya familia, nyumba zilizozingilwa na maji ya Ziwa Victoria
Tahadhari za kuchukua
“Tunasisitiza kuwekwa ndoo za kunawia mikono kwenye maeneo ya mikusanyika ya watu kama stendi, masoko na kwenye taasisi za umma ili mtu anapofika anawe mikono au kupaka vitakasa mikono ili kuzuia kuenea au kusambaa kwa ugonjwa huo,” anasema Dk Rutachunzibwa
Mwenyekiti wa Masoko mkoani Mwanza, Ahmad Nchora amesema wamepokea maelekezo ya Serikali kuweka vifaa vya kunawia mikono kwenye masoko zoezi ambalo limeanza kuchukuliwa hatua.
Mfanyabiashara wa huduma za fedha kwa njia ya mtandao, Mary Masanja anasema elimu inahitajika kwa kuwa hata kama wakiweka vifaa vya kunawia mikono au kupaka vitakasa mikono wengi wanapuuzia.
Kiongozi timu ya uhamasishaji kujikinga na Ebola, Profesa Deodatus Kakoko anawataka wananchi kuacha mila na tamaduni za kusalimiana kwa kushikana mikono ili kujikinga na ugonjwa huo.
Amesisitiza kuwa mtu aliyefariki kwa ugonjwa huo hatazikwa na kundi la watu na kwamba ipo timu maalum ambayo huvaa vifaa vya kujikinga ambayo itashughulika na masuala ya kuzika na ndugu wachache huku suala la kiimani likipewa kipaumbele.
Amesema kirusi cha ugonjwa wa Ebola kinaweza kuishi ndani ya saa 24 au chini ya hapo na inategemea na sehemu kilipo kama kwenye joto au majimaji, “hivyo suala la usafi linatakiwa kuzingatiwa ili kujikinga na ugonjwa huo.”
Tangazo

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima amewataka wananchi kuchukua tahadhari za ugonjwa huo kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na watoa huduma za afya.
Mkuu huyo amesisitiza wananchi kuacha kula nyama hasa inayotokana na mnyama wa porini na kwamba nyama zote zinatakiwa kupikwa na kuiva.
“Ni wakati sasa wananchi kutopuuzia maelekezo yanayotolewa na wataalam wa afya ni vyema kila mmoja kuchukua hatua za kujikinga, kuacha mila na desturi za kusalimia kwa kushikana mikono na kukumbatiana,” anasema Malima.
Mkuu huyo amewataka viongozi wa dini kueneza elimu ya ugonjwa huo kwa waumini wao ili waweze kujikinga na ugonjwa huo.
“Tunaamini viongozi wa dini wanaaminiwa zaidi na waumini wao, tumieni makanisa yenu kutoa elimu hii, lakini pia kuweka vifaa vya kunawia mikono kwenye nyumba zenu za ibada na kukaa kwa kupeana nafasi,” anasema Malima.