Uzalishaji mayai waongezeka Tanzania
- Waongezeka hadi bilioni 4.9 mwaka huu kutoka bilioni 4.5 mwaka jana.
- Kuongezeka kwa vituo vya kutotolesha vifaranga kwachangia.
- Serikali yashauri watu kuongeza kasi ya ulaji mayai.
Dar es Salaaam. Uzalishaji wa mayai nchini Tanzania umeongezeka kwa asilimia 8.8 mwaka 2021, jambo ambalo limekuwa likifungua fursa kwa wazalishaji na wafanyabiashara kufaidika ufugaji huo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki katika hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2022/23, Tanzania ilizalisha mayai bilioni 4.9 mwaka 2020/21. Mayai hayo yaliyozalishwa ni hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu.
Idadi hiyo imeongezeka kutoka mayai bilioni 4.5 yaliyozalishwa katika mwaka wa fedha wa 2020/21.
Ongezeko hilo siyo la bahati mbaya kwa sababu tangu mwaka 2018, uzalishaji wa bidhaa hiyo iliyojaa protini umekuwa ukiongezeka mfululizo. Mathalan, mwaka 2017, mayai bilioni 2.7 yalizalisha na mwaka uliofuata yakapanda hadi bilioni 3.1 kabla hayajapanda zaidi hadi bilioni 3.5 mwaka 2019.
Waziri Ndaki, kuongezeka kwa uzalishaji wa mayai kumechangiwa na kuimarika kwa vituo 28 vya kutotolesha vifaranga vya kuku vilivyopo nchini kutokana na uhamasishaji na mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya mifugo.
“Pia, wananchi wamehamasika kufuga kuku ili kujikomboa kiuchumi,” alisema Ndaki.
Soma zaidi:
- Kigoma kinara wa usajili mashamba Tanzania bara
- Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika
- Wakulima washauriwa kutumia teknolojia ya kisasa ya kilimo cha umwagiliaji
Licha ya mayai kuwa sehemu ya kuwapatia wananchi kipato, ni chakula muhimu kwa afya ya binadamu kwa sababu imejaa virutubishi mbalimbali ikiwemo protini.
Shirika la Chakula Duniani (FAO) unaeleza kuwa ulaji wa mayai kwa mtu mmoja kwa mwaka ni wastani wa mayai 106 tu, huku idadi inayotakiwa kuliwa na mtu mzima ni mayai 300 kwa mwaka.
Mayai yana protini, vitamini A, D, B na B12 na madini ya lutein na zeaxanthin yanayoweza kuzuia mtu kupata matatizo ya macho atakapozeeka.
Pia mayai yana kemikali iitwayo ‘choline, ambayo ni muhimu kwa ukuaji na afya ya ubongo wa mtoto tumboni. Mwanamke mjamzito anashauriwa kutumia yai moja hadi mawili kwa siku.
Mayai yana Omega-3 nyingi. Husaidia kupunguza mafuta yapatikanayo katika damu yaani ‘triglycerides’.
Latest



