Ripoti: Tanzania ni miongoni mwa nchi 11 zinazowekeza kwenye utafiti wa GMO Afrika

Daniel Samson 0431Hrs   Agosti 08, 2018 Biashara
  • Nchi 11 zaridhia utafiti wa mazao ya kibayoteki Afrika.
  • Mazao hayo kuongeza uzalishaji na soko kwa wakulima.
  • Wasomi wataka tathmini ifanyike kabla ya kuwapa wakulima.

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiadhimisha siku ya Wakulima nchini  (Nanenane), Tanzania imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 11 barani Afrika zilizo katika mwelekeo mzuri wa kuzalisha mbegu na mazao yatokanayo na uhandisi jeni (GMO) licha ya kukabiliwa na upinzani kutoka kwa wadau wa afya na mazingira.

Ripoti ya Utafiti ya Hali ya Biashara na Kukubaliwa kwa Mazao ya Kibayoteki ya mwaka 2017 iliyozinduliwa hivi karibuni jijini hapa inaeleza kuwa kuna ongezeko kubwa la matumizi ya mbegu zilizoboreshwa na eneo la kilimo cha mazao hayo duniani jambo linaloleta matumaini ya kuongezeka kwa uzalishaji na kupunguza tatizo la njaa katika nchi zinazoendelea kama Tanzania.

“Nchi 11 za Afrika zinafanya utafiti wa mazao ya kibayoteki huku Afrika Kusini na Sudan zikiwa tayari zinafanya biashara ya mazao hayo na kufanya jumla ya nchi 13 zinazowekeza katika  utafiti wa mazao ya kibayoteki katika bara hili. Nchi hizo ni Burkina Faso, Cameroon, Ethiopia, Ghana, Kenya, Malawi, Mozambique, Nigeria, Swaziland, Tanzania and Uganda,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Mazao ya kibayoteki yanatokana na teknolojia ya uhandisi jeni ambayo hutumika kutengeneza mbegu zilizoboreshwa katika maabara (Genetically Modified Organism) ambazo zinatajwa na watafiti kuwa zina uwezo mkubwa wa kuhimili ukame na kuongeza uzalishaji wa mazao na soko kwa wakulima.

Katika uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Matumizi na Upataji wa Kilimo cha Kibayoteki (ISAAA) kituo cha Afrika, Dk Margaret Karembu anasema kuwa Tanzania na Msumbiji zilipitisha mbegu za mahindi yenye uwezo wa kuhimili wadudu waharibifu na ukame chini ya mradi wa Water Efficient Maize for Africa (Wema).

Dk Karembu anasema hiyo ni  ishara ya wazi kuwa serikali hizo za Msumbiji na Tanzania zina nia ya kuwekeza teknolojia hiyo katika kilimo.

Majaribio ya mazao ya kibayoteki yaliingia Tanzania mwaka 2008 chini ya mradi wa Wema uliofadhiliwa na taasisi ya Bill & Merinda Gates ya nchini Marekani. Hata hivyo, mradi huo ulianza mwaka 2016 na majaribio hayo yanafanyika chini ya uangalizi wa Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo cha Makutupora, Dodoma.

Kutokana na mkanganyiko wa kisheria kuhusu mazao ya kibayoteki  katika jamii, serikali haijaridhia matumizi ya teknolojia ya uhandisi jeni lakini imeruhusu majaribio ya kisayansi yafanyike katika kituo hicho cha Makutupora kabla ya kuwaruhusu wakulima kuanza kutumia kwenye mashamba yao.

Dk Karembu amesema teknolojia ya uhandishi jeni ina manufaa mengi kwa wakulima na uchumi wa nchi kinyume na tafsiri potofu za baadhi ya wanaharakati na wanasiasa ambao wamekuwa wakidai kuwa sio rafiki kwa mazingira na afya ya binadamu.

“Kutoka mwaka 1996-2016, Mpango wa uchumi wa PG uliripoti kwamba mazao ya GMO kiuchumi yalitoa faida ya Dola bilioni 186.1 kwa wakulima milioni 17, ambao wengi wao ni wakulima wa kike, wadogo wadogo wenye majukumu ya kukimu maisha ya familia zao na jamii,” anabainisha Dk Karembu.

Mazao ambayo yanazalishwa kwa wingi kupitia teknolojia ya GMO ni pamoja na mahindi, pamba, maharage ya soya na viazi ambavyo hutegemewa na nchi za Afrika kama sehemu ya kuboresha usalama wa chakula na kuingiza kipato.

Ripoti hiyo inaeeleza kuwa  mwaka 2017 zaidi ya hekta 189.8  za ardhi zilipanda mazao yatokanayo na GMO ikiwa ni ongezeko la asilimia tatu ukilinganisha na mwaka 2016. Nguvu ya matumizi ya mazao hayo inachagizwa na mataifa makubwa ya Marekani, Brazil, Argentina, Canada na India ambayo yanatumia teknolojia hiyo kijinufaisha kiuchumi duniani.
Mpaka sasa ni nchi 24 duniani ambazo zinalima mazao ya kibayoteki, huku nchi mbalimbali zikiendelea na utafiti wa mbegu hizo kabla hazijapelekwa kwa wakulima. Nchi 19 zinafanya biashara na kutumia bidhaa za mazao hayo, kwa mujibu wa ripoti hiyo.


Watafiti nchini wanabainisha kuwa ili wakulima waongeze tija katika uzalishaji, Serikali haina budi kukubali mabadiliko ya teknolojia katika kuzalisha mazao.

Mtafiti wa  Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Nicholous Nyange anasema ni wakati muafaka kwa Tanzania kuikubali teknolojia hiyo ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuongeza uzalishaji.

Pamoja na faida zinazoendelea kutajwa, baadhi ya wakosiaji wa teknolojia hiyo wanaeleza kuwa kuna athari kubwa zinazotokana na matumizi ya mazao ya kibayoteki ikiwa ni pamoja na kuharibu mfumo wa ikolojia, kuharibu ama kubadilisha kabisa virutubisho katika mimea na kusababisha magonjwa kwa binadamu kama kansa.

Athari nyingine ni kuharibu rutuba ya ardhi na kusababisha wakulima kuwa tegemezi wa madawa ya kilimo, kujitokeza kwa magugu ambayo yanajikinga na madawa ya kuua magugu, na hasara kwa wakulima kutokana na ununuzi wa kiasi kikubwa cha madawa.

Hata hivyo, Katibu Mtendaji wa muda kutoka Chama cha Bayoteki Tanzania, Dk. Emmarold Mneney anabainisha kuwa tathmini ya kina ifanyike nchini kuhusu mazao ya kibayoteki ili wakulima wapate fursa ya kufaidika na uzalishaji wa mazao unaoendana na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani.

Marekani inaongoza ulimwenguni kwa utengenezaji wa mbegu ZA GMO zikizambazwa na  kampuni kubwa ulimwenguni kama Monsanto, Syngenta AG, na DOW Chemicals.


Related Post