TMA: Mvua kubwa kunyesha kesho katika mikoa mitano
- Mikoa hiyo ni pamoja na Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.
Arusha. Mamlaka ya Hali ya HewaTanzania (TMA) imewatahadharisha Watanzania juu ya hali mbaya ya hewa inayoweza kusababisha mvua kubwa katika mikoa mitano.
Taarifa ya TMA iliyotolewa jana Disemba 10, 2025 imebainisha kuwa mvua hizo zinatarajiwa kunyesha kesho Disemba 12, mwaka huu ikiwataka wananchi kuchukua tahadhari.
“Angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa maeneo machache ya mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa Disemba 12, 2025. Wakazi wa maeneo husika mnapaswa kuzingatia na kujiandaa,” imesema taarifa ya TMA.
Mbali na angalizo hilo, TMA imetangaza uwepo wa mvua zitakazoambatana na radi na ngurumo kuanzia leo Desemba 11 hadi 20, 2025 katika maeneo ya Ziwa Victoria, nyanda za juu kusini-magharibi huku maeneo machache ya pwani na nyanda za juu kaskazini-mashariki kupata mvua kwa kiwango kidogo.
Maeneo hayo ni Kanda ya Ziwa Viktoria inayohusisha mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Simiyu na Mara na nyanda za juu kaskazini- mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro) mvua ikitarajiwa kunyesha katika maeneo machache mengine yakibaki na mawingu kiasi na vipindi vya jua.
Pwani ya kaskazini (Mikoa ya Tanga, maeneo ya kaskazini mwa Morogoro, Pwani na Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba) mvua zinatarajiwa katika maeneo machache.
Huenda kunyesha kwa mvua hizo kukapoza machungu ya jua kali lililowaka mfululizo kuanzia mwezi Oktoba na kusababisha hali ya joto kufikia hadi nyuzi joto 35 katika baadhi ya mikoa nchini.
Hali ilikuwa mbaya kwa wakulima wanaotegemea mvua ambao mashamba yao yalibaki makavu na kupelekea baadhi ya mazao kufa wengine kupata mavuno machache.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu waTMA n Dkt. Ladislaus Chang’a , Oktoba 17 mwaka huu alisema mwenendo wa mvua nchini unaweza kutengemaa katika kipindi cha nusu ya pili ya msimu (Februari – Aprili, 2026) ikilinganishwa na nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2025 – Januari, 2026).
Latest