Wafanyakazi wa nyumbani wabunifu njia mpya kupata taulo za kike

April 7, 2023 10:28 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni zile zinazoweza kutumiwa zaidi ya mara moja.
  • Zitawasaidia kuwapunguzia gharama za maisha.

Mwanza. Kutokana na changamoto za kujisitiri wakati wa hedhi wanazokabiliana nazo wanawake, baadhi wabunifu wamekuja na taulo za kike zinazoweza kufuliwa na kutumiwa zaidi ya mara moja. 

Wabunifu hao ni wasichana 15 ambao wanafanya kazi za nyumbani ambao wameamua kuwasaidia wanawake na wasichana ambao hawawezi kumudu gharama za kununua taulo za kike zinazouzwa madukani.

Wasichana hao kutoka jijini Mwanza na Ngara mkoani Kagera wanaofanya wamejikita kutengeneza taulo za kike (Sodo) ili kumsaidia mtoto wa kike azipate kwa gharama nafuu.

Taulo hizo zinaweza kutumiwa kwa muda wa miezi 12 kabla hazijapoteza ubora wake hivyo kumpunguzia mwanamke gharama za kununua taulo mara kwa mara.

Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanikiwa kuzungumza na baadhi ya wasichana hao ambao wamesema wanajisikia fahari kuwasaidia wenzao kuboresha afya.

Mmoja wa wanachama wa kikundi hicho na mkazi wa jijini Mwanza, Deisa Elia anasema amekuwa na ndoto ya kuwa na kiwanda cha kutengeneza taulo na kuelimisha namna ya kuzitumia.

Anasema hataki wasichana wapitie mapito aliyopitia kwa sababu wakati anaanza kupata hedhi hakuwa na mtu aliyemsaidia namna ya matumizi sahihi ya taulo kitendo ambacho kilimpa wakati mgumu.

“Kwa mara ya kwanza kukutana na hali hii sikuwa nafahamu chochote na wakati huo tayari nilikuwa nafanya kazi za nyumbani hivyo mwajiri wangu hakuhangaika na mimi kwahiyo nilifanya kadiri ya uwezo wangu kujistiri, lakini sasa angalau nina mwanga na tayari nina uwezo wa kutengeneza taulo za kufua,” anasema Deisa.

Elimu hiyo haitakuwa yake peke yake badala yake aitatumia kuelimisha wengine ili kuwe na hedhi salama lakini pia kupunguza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya kujisitiri wakati wa hedhi.

” Taulo tunazotengeneza hapa ni nzuri na rahisi kutumia na zinapatikana kwa gharama nafuu hivyo kila mmoja anaweza kumudu kununua,” anasema Deisa.

Kikundi cha wasichana 15 wakipata elimu namna ya kushona taulo za kike za kufua (sodo) ili kuhakikisha jamii inakuwa na hedhi salama. Picha na Mariam John.

Ndiyo kwanza wanaanza

Deisa bado hawajaanza kufanya uzalishaji kwa sasa lakini tayari wamepata mafunzo ya kuzitengeneza taulo, ambapo ndoto yao ni kuwa na kiwanda kikubwa cha bidhaa hiyo ambayo wangependa iwafikie wafanyakazi wengi wa nyumbani.

Mwanachama mwingine wa kikundi, Neema Ishengoma anasema suala la upatikanaji wa taulo za kike ni changamoto kwa kuwa zinauzwa kwa gharama kubwa hivyo kwa mtu mwenye kipato cha chini kushindwa kumudu kuzinunua.

“Tunaomba kuungwa mkono wa mitaji  ili tuweze kutengeneza bidhaa nyingi ziweze kuuzika sokoni,” anasema Neema. 


Soma zaidi:


Nini tafsiri ya hedhi salama

Afisa Msimamizi wa makao na Uwezeshaji wa Shirika la Wotesawa lililopo jijini Mwanza, Demitila Faustine anasema hedhi salama kwa watoto wa kike na wanawake huchangia kuwa na familia salama na kuwasaidia kutimiza ndoto zao. 

Ili kuwa na hedhi salama wameamua kutoa mafunzo kwa kikundi hicho ili kiweze kutengeneza taulo za kike za kufua ambazo zitawasaidia katika kukuza kipato chao.

“Tunaratajia wanufaika kutengeneza taulo 1,000 za kufua ambazo zitauzwa kwenye jamii kwa gharama nafuu ambayo wasichana na wanawake wengine wataweza kumudu,” anasema Faustine. 

Mkufunzi wa utengenezaji wa taulo hizo, Vicky Edward anasema lengo la mafunzo hayo ya vitendo ni kuwapatia ujuzi na uelewa wa namna ya kutumia taulo za kike.

Zipo fursa katika hedhi ambapo mnufaika akifahamu sodo namna inavyotengenezwa hatoishia kuitumia mwenyewe bali ataigeuza na kuwa fursa ya kiuchumi kwake.

“Katika uchunguzi mdogo tuliofanya taulo za kike za kufua zina uwanda mpana na watumiaje wake ni wengi hapa duniani na kwamba suala la utumiaji wa taulo ni endelevu la kila siku ambalo msichana yeyote atakutana nalo,” anasema Edward.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW