Taka za taulo za kike: Tishio jipya kwa mazingira Tanzania

March 24, 2023 9:05 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ukosefu wa elimu wasababisha taka hizo kuzagaa mitaani.
  • Zachangia kuziba kwa mitalo, miundombinu ya maji taka.
  • Serikali yaanza kutoa elimu na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na uhifadhi wa taka hizo. 

Mwanza. Wakati Serikali ya Tanzania ikifanikiwa kudhibiti taka za plastiki, taka taulo za kike na za watoto (diapers) zinatajwa kuwa ni changamoto nyingine ya mazingira katika mitaa mbalimbali jijini Mwanza.

Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imepita katikamitaa mbalimbali jijini hapa, na kubaini uwepo wa taka hizo ambazo zimetelekezwa kwenye mitalo na sehemu za wazi.

Rebecca Musogomba (45), mkusanya taka katika Mtaa wa Mwembe Sangara anakiri kuwa taka za taulo za kike na watoto zimekuwa changamoto ya usafi wa mazingira kwa kuwa katika maeneo wanayoenda kuzoa taka huzikuta zimekaa muda mrefu na zinatoa harufu kali.

“Kwa ujumla tunapozikuta taka za aina hiyo na zingine za vioo na zenye ncha kali haturuhusiwi kuzibeba, lakini inapotokea unaziacha wahusika hulalamika kwa mamlaka husika na mamlaka hizo kushindwa kutulipa mishahara yetu hivyo tunakuwa hatuna namna inatubidi tu kuzichukua,” anasema Musogomba, ambaye amekuwa akifanya kazi ya kuzoa taka tangu mwaka 2014.

Mfanya usafi mwingine, Omary Lukanavya anasema kwa kawaida taka za aina hiyo zinatakiwa kufungwa vizuri kwenye mifuko ndipo zihifadhiwe, lakini kinachofanyika kwa sasa ni tofauti kwani zinatupwa hovyo huku zikiwa na harufu kali.

“Pamoja na wananchi kupewa elimu ya namna ya kutunza taka hizo lakini haifuatwi badala yake watu wanatupa hovyo kwenye mitalo na hata barabarani,” anasema Lukanavya.

Maeneo ambayo taka hizo hupatikana kwa wingi ni mahotelini, majumbani na sehemu za starehe ikiwemo baa na nyumba za kumpumzikia wageni, jambo linalosababisha kuziba kwa mitalo, vyanzo vya maji, muonekano usioridhisha wa mitaa. 

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Kirumba Kati, Ramadhan Magige anakiri kuwa miezi mitatu iliyopita hali hiyo ilikuwa mbaya ambapo kila baada ya muda walikuwa wanaita gari la kuzibua chemba lije kwenye maeneo yao.

Baadhi ya wazoa taka katika kata ya Kirumba Mwanza, wakizikusanya na kuziweka kwenye mapipa ya kuhifadhia kabla ya gari kuja kuzichukua eneo hilo na kuzipeleka kenye dampo lilipo Buhongwa Mwanza. Picha | Mariam John.

Amezitaja chemba tatu ambazo ni korofi kwa kutupa taka hizo kuwa ni Mwembe Sangara, Sokoni na Mtaa wa Vijana.

“Ni kweli kwamba maeneo hayo kulikuwa kunapatikana taka nyingi sana na kila baada ya muda tulikuwa tunaitisha gari la maji taka kuja kuzibua chemba hizo, na zinapozibuliwa pampasi na pedi zilikuwa zinatolewa kwa wingi,” anasema Magige.

Kutokana na changamoto hiyo waliitisha mkutano kwa ajili ya kutoa elimu ya namna ya kuhifadhi taka hizo ili kupunguza changamoto hiyo.

“Na tulitengeneza sheria na faini kwenye nyumba au hoteli itakayokutwa na changamoto hiyo kwamba mhusika atatozwa faini ya Sh50,000 kwa mwenye hoteli au lodge (nyumba ya kulala wageni) na Sh10,000 au Sh15,000 kwa mwenye nyumba,” anasema Magige.

Pia adhabu nyingine ni kupewa eneo la kusafisha kwa muda mrefu unaoweza kumchukua hadi saa tatu.

Ni zaidi ya taka za taulo za kike

Ujio wa taulo za watoto wadogo (pampers/diapers) nao unatajwa kuwa kero kwenye mitaa mingi jijini Mwanza. 

Licha ya kuwaletea ahueni akina mama katika kuwasitiri watoto wao wanapopata haja ndogo na kubwa, lakini uhifadhji wake baada ya kutumika umekuwa ni tatizo kubwa kwa sababu hutupwa bila mpangilio mzuri.

Wakizungumzia changamoto hiyo baadhi ya wananchi wanasema zinachangia uchafuzi wa mazingira kwa kuwa hazihifadhiwi sehemu inayotakiwa.

“Utakuta pampasi imetupwa nzi wamejazana kwenye eneo hilo na wakati mwingine zinatupwa karibu na makazi ya watu au sehemu ya biashara ya chakula hivyo nzi wanapotoka hapo wanaenda kwenye chakula au vyombo,” anasema Martha Lume, mkazi wa Nyamanoro jijini Mwanza.

Martha anaiomba Serikali kutafuta suluhisho za taka hizo kwani pamoja na kuchafua mazingira lakini pia zinaweza kusababisha magonjwa kwa watu kutoka na harufu kali.


Soma zaidi: 


Mwanga waonekana

Mkazi wa Mtaa wa Twiga, Kata ya Kirumba, Veronica Jonas anasema angalau sasa wana mtaa ambao hauna harufu mbaya na uchafu wa taka hizo kama ilivyokuwa kipindi cha nyuma kwa sababu elimu imeanza kuwafikia watu.

“Tukapeana elimu unapotumia taka aina ya pedi na pampasi ifunge vizuri kwenye mfuko kisha idumbukize kwenye mfuko mwingine ili wanapopita wanaozoa taka wasione kinyaa kwa kuwa zile ni taka chafu,” anasema Jonas.

Mamlaka zathibitisha uwepo wa taka hizo

Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mkoa wa Mwanza (Mwauwasa) Mohamed Seif anasema kuwa taka hizo kuwa kero na kisababishi kikubwa cha uharibifu wa miundombinu ya maji taka jijini hapa.

Kwa mujibu wa Seif, Mtaa wa Kirumba kuwa moja ya mitaa korofi kwa utupaji wa taka hizo ambazo zinachangia kuharibika kwa miundombinu ya mabomba ya maji taka.

Mwauwasa wanaendelea kutoa elimu mara kwa mara ya utunzaji wa mazingira hususani katika suala la utupaji wa taka hizo kwenye mabomba ya maji taka ambapo hutumia gharama kubwa za matengenezo.

Afisa Misitu na Mratibu wa Shughuli za Mazingira Mkoa wa Mwanza, Mangabe Mnilago anasema baada ya kudhibiti taka za plastiki, sasa nguvu inapaswa kuhamishiwa kwa taka za taulo za kike na watoto. 

“Tumefanikiwa kudhibiti taka za plasitiki na sasa kuna taka mpya ambazo ni pedi na pampasi, hizi tusipozidhibiti kwa haraka zinaweza kusababisha ongezeko la taka nyingi kwenye maeneo yetu,” anasema Mnilago.

Anasema asilimia 40 hadi 60 ya vitu au taka zinazofanya mfumo wa maji taka kuziba inatokana na utupwaji wa taulo za kile kwenye vyoo majumbani hasa vya kuflashi. 

Maeneo ambayo yanazalisha taka hizo kwa wingi ni pamoja na vyuoni, kwa mujibu wa Mnilago.

Ni kwa namna gani taka hizo zihifadhiwe

Afisa Afya kutoka Kituo cha Afya cha Kirumba Mwanza, Veronica Massawe anasema utupaji taka hizo bila mpangilio zinasababisha kutokutunza utu wa mwanamke kwa sababu hedhi ni fahari yake.

Anasema hata kutupa kwa kuchanganya na taka nyingine katika vyombo vya kuhifadhia taka si sahihi kwa kuwa haziozi.

“Kunahitajika kuwepo na sehemu ya kutupa taka za hedhi mara tu zinapotumika na utamaduni wa mwanamke aliyefundishwa ni kuhifadhi ipasavyo mahali sahihi taka hizo baada ya kuzitumia aidha kwa kuchoma ili mwingine asione,” anasema Massawe.

Anasema kwa sasa wanaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhakikisha wanahifadhi vizuri taka hizo ili kulinda utu wao lakini kuzuia usambazaji wa taka hizo.

“Tunawaeleza wanapomaliza kutumia wazifunge vizuri kwenye mfuko au gazeti kisha wakaweke kwenye debe au mfuko wa taka ambao baadaye wafanya usafi wanapopita wazikute zikiwa zimefungwa vizuri hiyo itasaidia kupunguza kuenea kwa bakteria wanaoweza kueneza magonjwa,” anasema Massawe.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...