Pedi za kufua zinavyosaidia kupunguza uchafuzi mazingira

October 4, 2024 5:11 pm · Yuster Massawe
Share
Tweet
Copy Link
  • Ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu stahiki ya uhifadhi wa taulo na nepi hizo.

Katika moja ya kumbi mashuhuri za mikutano za Mlimani City jijini Dar es Salaam, baadhi ya watu wanaenda kutazama bidhaa mbalimbali na makasha madogo yaliyowekwa kwenye meza iliyokuwepo katikati ya ukumbi huo. 

Ndani ya makasha hayo madogo yanayoweza kubebeka kuna moja ya bidhaa adimu na muhimu zaidi kwa afya ya mwanamke: Visodo maarufu kama pedi. 

Tofauti na pedi zilizo zoeleka, pedi zinazo tazamwa hapa ni zile zinazofuliwa mara baada ya kuzitumia. 

Mkurugenzi Uendeshaji wa Kampuni ya Jollie Reusable Pads and Accessories, inayotengeneza pedi hizo, Mwanaharusi Mwilima anaeleza kuwa ndani ya kasha moja kuna pedi nne ambazo zikitunzwa ipasavyo zinaweza kutumika kwa zaidi ya mwaka mmoja na nusu. 

Pedi za kufua kuokoa mazingira

Miongoni mwa faida za pedi au taulo za kike za kufua, Mwanahamisi anasema ni pamoja na kusaidia kutunza mazingira, na unafuu katika upatikanaji.

“Taulo za kutupa ambazo ziko sokoni sasa hivi zimekuwa chanzo cha uchafu mitaani na kushindwa kutunza utu wa mwanamke,” anasema.

Anasema pedi hizo zinapunguza uchafuzi wa mazingira kwa kuwa mtumiaji anazitumia nne kwa muda mrefu na kuzifua kila zinapotumika tofauti na zile ambazo kila baada ya kuzitumia mtumiaji huhitajika kuzitupa. 

Hata hivyo, si wote wanafahamu vyema namna ya kuzihifadhi pedi zilizotumika jambo linalochochea uchafuzi wa mazingira. 

Ni kawaida kwa sasa kukutana na taka za pedi zilizotumika katika majalala madogo na makubwa jijini Dar es Salaam na majiji mengine mikubwa kama Mwanza na Arusha, vikichagizwa zaidi na mfumo mbovu wa kuhifadhi taka hizo.

Mwonekano wa pedi na nepi zinazoweza kufuliwa. Taulo hizo za kike pamoja na kumsitiri mwanamke wakati wa hedhi zinasaidia kupunguza uchafuzi wa mazingira. Picha|Davis Matambo.

Taka za pedi ni hatari kwa viumbe

Taulo za kike za kutupa zisipo hifadhiwa vizuri zinaweza kuathiri mazingira kwa kuwa nyingi zimetengenezwa na vifaa visivyooza kwa urahisi kiasi cha kuathiri wadudu na mimea katika udongo.

Uchafuzi huo si tu unaathiri mimea na wadudu, bali kuna hatari ya kuathiri afya za binadamu na wanyama hasa kwa taka zinazozalishwa na wanadamu katika shughuli za kila siku.

Ikiwa ni sehemu ya majukumu yao, Mwanahamisi anasema kwa sasa wanatoa elimu kwa jamii ifahamu vema taulo za kike za kufua, namna zinavyotengenezwa na faida zake.

Mwanahamisi ni miongoni mwa wabunifu waliokuwa wakionyesha bidhaa na huduma zao katika maonyesho ya tisa ya Sahara Spark yaliyo fanyika Septemba 27 mwaka huu jijini Dar es salaam. Maonyesho hayo ambayo huambatana na mikutano huandaliwa na kampuni ya Sahara Ventures. 

Shirika lisilo la kiserikali la Actionaid, linalofanya kazi na mabinti na wanawake Tanzania, limesema kuwa pedi za kufua zina faida nyingi ikiwa ni pamoja na afya bora kwa wanawake na mabinti, hali nzuri ya kazi na elimu na gharama ndogo

“Wanawake wengi na mabinti duniani wanalazimika kutumia vitu visivyo rafiki ili kudhibiti hedhi zao ikiwa ni pamoja na nguo chafu, magazeti pamoja majani ya miti,” limesema shirika hilo kwenye tovuti yake.

Elimu ni kila kitu

Licha ya kuwa baadhi ya wadau wanasema kuwa pedi za kufua zitapunguza zaidi uchafuzi wa mazingira, baadhi wanaona utokomezaji wa taka hizo na nepi unahitaji utoaji wa elimu zaidi kwa watumiaji wake. 

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la kiserikali la Maji Safi Group, Rachel Stephen anasema taulo za kike za kufua si suluhisho pekee la kutunza mazingira kwa kuwa nazo zinatengenezwa na malighafi ambayo haiozi kirahisi. 

Rachel anasema pedi za kufuliwa nazo zitatutupwa baada ya muda wa matumizi kuisha.

“Naamini kuwa taulo za kike za kufua ni sehemu ya suluhisho lakini sio suluhisho pekee, suluhisho ni watu kupewa elimu stahiki ya matumizi yalio sahihi ya uteketezaji wa taka hizo,” anaeleza Rachel.

Upunguzaji wa taka za nepi na pedi zinazotumika mara moja ni miongoni mwa masuala yanayoangaziwa kwa karibu na mataifa mbalimbali duniani na taasisi za Umoja wa Mataifa (UN). 

Mnamo Machi 2019, Mpango wa Life cycle Initiative chini ya Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) ulianza ukaguzi wa tathmini ya mzunguko wa maisha wa nepi zinazotumiwa mara moja na njia mbadala ya uhifadhi wake.Ili kudhibiti, Ripoti ya UNEP inasema watumiaji wote wa nepi na taulo za kike za kufua na zisizo za kufua wanapaswa kupewa elimu stahiki ikiwa ni mpango kazi wa kudhibiti uchafuzi wa mazingira.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks