Wanawake wajasiriamali wabeba mzigo kutunza familia
- Sehemu kubwa ya mapato yao hutumika kuhudumia familia.
- Serikali yasema itawawezesha zaidi kuinuka kiuchumi.
- Pia kuwatafutia masoko ya kimataifa.
Mwanza. Kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaojihusisha na shughuli za ujasiriamali kumesaidia kujipatia kipato ambacho kwa sehemu kubwa kinatumika katatua changamoto mbalimbali za familia ikiwemo chakula, matibabu na elimu.
Mapato hayo pia ni fursa ya kuvunja mnyororo wa umasikini na kuwapa wanawake fursa ya kuwa huru kiuchumi, jamba linalosaidia kuwapunguzia utegemezi na ukatiliwa kijinsia.
Hata hivyo, huenda ujasiriamali haufaidishi moja kwa moja wanawake kwa sababu zaidi ya nusu ya kipato wanachopata kinatumika kutatua changamoto za familia.
Waziri wa viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo aliyekuwa akizungumza katika maonyesho ya wafanyabiashara ya Afrika Mashariki jana Desemba 6, 2021 jijini Mwanza amesema asilimia 6O ya washiriki katika maonyesho hayo ni wanawake hivyo mapato yao yataenda kusaidia katika familia zao na kuwatoa katika umasikini.
Kutokana na mzigo walionao wanawake katika familia zao, amesema Serikali itaendelea kuwawezesha na kuwawekea mazingira rafiki ya biashara ili watoe mchango kwa jamii.
“Biashara ndogo zinafanywa zaidi na Wanawake na Vijana jambo ambalo ni muhimu na katika maonesho haya Zaidi ya asilimia 60 ya wajasiriamali walioshiriki ni wanawake ambapo tafiti zinaonyesha kwamba asilimia 90 ya mapato yatakayopatikana katika biashara zao zitasaidia familia na kutatua changamoto mbalimbali,” amesema Prof Mkumbo.
Pia waziri huyo amesema, wanafanya jitihada za kuwasaidia wanawake wajasiriamali kupata masoko na kushiriki maonyesho ya kimataifa kwa ajili ya bidhaa zao ili kuwaongezea wigo wa mapato.
“Maonyesho haya yana umuhimu mkubwa kwani nchi zote duniani ujasiriamali unachukua nafasi kubwa ,” amesema Mkumbo.
Maonyesho ya wajasiriamali hutoa fursa kwa wafanyabiashara kuonyesha bidhaa zao, kukutana na wateja wapya na kuunda mtandao wa wawekezaji ambao unasaidia kukuza biashara katika nyanja.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Josephat Rweyemamu amesema maonyesho hayo yalianza mwaka 1999 yakiwa na washiriki 59 sasa wameongezeka hadi kufikia 1,400. Pia bidhaa zimeongezeka na zingine zimepata nembo za ubora.
Wakizungumza kwenye maonyesho ya 21 ya wajasiriamali wadogo na wakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kwa jina la Nguvukazi/ Jua kali baadhi ya wajasiriamali hao wamesema maonyesho hayo yatasaidia katika kutangaza bidhaa wanazozalisha na kuzifanya kwenye maeneo yao.
“Ni maonyesho mazuri mwitikio wa watu ni mkubwa na biashara zinafanyika, licha ya kuwepo kwa janga la Uviko-19 lakini angalau sasa biashara inafanyika,” amesema Annabella Jackson, mfanyabiashara wa jijini Mwanza.
Maonyesho hayo yameshirikisha wafanyabiashara 1,304 kutoka nchi za Afrika Mashariki, kati ya wafanyabaishara hao asilimia 60 ni wanawake. Pia kati yao 794 ni kutoka nchi mbalimbali na 510 wanatoka mikoa mbalimbali hapa nchini.
Kauli mbiu katika maonyesho hayo ni “Ukuzaji ubora na ubunifu ili kuinua ushindani wa ujasiriamali wadogo wadogo wa Afrika Mashariki na ahueni baada ya UVIKO-19”.
Latest
