Ulaya kuachana na magari yanayotumia mafuta 2035
- Wabunge wa Umoja wa Ulaya wapiga kura kuunga mkono muswada wa kuachana na magari yanayotumia mafuta ifikapo 2035.
- Lengo ni kupunguza hewa ya ukaa duniani.
Dar es salaam. Wakati kilio cha mataifa mengi ulimwenguni kikiwa ni kupanda kwa bei za mafuta mara baada ya Urusi kuivamia Ukraine, mataifa 27 yaliyopo ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) yanakusudia kuachana na nishati hiyo ya kuendesha vyombo vya moto ifikapo 2035.
Hatua hiyo imekuja baada ya Wabunge wa Bunge la EU kupiga kura ya kuzuia utengenezaji na uuzaji wa magari yanayotumia mafuta ya dizeli na petroli ifikapo mwaka 2035.
Lengo ni kupunguza uchafuzi wa hewa na kuhimiza teknolojia ya magari ya umeme duniani.
Mkutano wa Bunge hilo umefanyika Juni 8 2022, jijini Strasbourg nchini Ufaransa ambapo wabunge wamepiga kura wakiyataka makampuni ya utengenezaji na uuzaji wa magari kusitisha uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa asilimia 100 ifikapo katikati ya muongo ujao.
Jumla ya wabunge 339 walipiga kura za ndiyo wakipendekeza muswada huo upitishwe huku 249 wakipiga kura za hapana na wabunge 24 hawakupiga kura kutokana na kutokuwepo katika mkutano huo.
Wabunge hao pia wamependekeza kupunguza kwa asilimia 55 ya kiwango cha hewa ya ukaa ifikapo mwaka 2030, pendekezo ambalo linaenda kutilia mkazo sheria iliyopitishwa awali ya kupunguza hewa ya ukaa mpaka kufikia asilimia 37.5 katika muongo ujao.
Mara baada ya tukio la upigaji wa kura kukamilika, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Umoja wa Ulaya, Pascal Canfin alichapisha katika ukurasa wake wa Twitter kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuhakikisha usalama wa mazingira duniani.
‘Asilimia 0 ya magari yatumiayo mafuta ifikapo 2035, nawakaribisha kwa dhati katika upigaji wa kura “ ameandika Canfin.
Mataifa ya EU yanashika nafasi ya tatu katika uzalishaji wa hewa ya ukaa yakiwa nyuma ya Marekani na China. Hata hivyo, muswada huo ili uanze kufanya kazi unatakiwa kupigiwa kura kwanza kwenye kamisheni ya Umoja wa Ulaya.
Upigaji kura wa muswada huo unatarajiwa kufayika mwishoni mwa mwaka huu na iwapo sheria hiyo itapitishwa basi huenda soko la mafuta barani Ulaya lenye wakazi takribani milioni 447 likaathirika na kusababisha unafuu katika maeneo mengine ambayo mafuta ndiyo msingi mkuu wa uchumi ikiwemo barani Afrika.
Latest
