Rais Samia aagiza mahakama za chini zimulikwe

May 24, 2023 4:25 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni hukumu iliyotolewa na mahakama mkoani Lindi iliyoibua utata. 
  • Mahakama ilimuachia huru mfugaji anayedaiwa kuingiza mifugo katika hifadhi ya Nyerere. 
  • Mkuu wa mkoa naye atofautiana na hukumu hiyo. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan umemuagiza Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma kutupia jicho utendaji wa mahakama za chini kwa sababu maamuzi yanayofanywa na baadhi ya mahakimu yana “ukakasi”.

Rais Samia ametoa agizo hilo baada ya kurejea uamuzi wa hivi karibuni wa mahakama mkoani Lindi kumuachia huru mfugaji anayedaiwa kuingiza mifugo katika hifadhi ya Taifa ya Nyerere kinyume na sheria kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumtia hatiani.

Baada ya uamuzi huo kutoka, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack kwa mujibu wa Rais Samia alikataa akisema mifugo ya mfugaji huyo ilikutwa hifadhini na alistahili kupewa adhabu.

“Tumesikia kesi ya Lindi kwamba wafugaji wamefanya makosa ya wazi wazi, wamekamatwa kwenye makosa, Jaji akasema nami nakwenda hukohuko kutizama na kurudi akasema hawana makosa,” amesema Rais Samia leo Mei 23, 2023 wakati akiwaapisha majaji sita wa Mahakama ya Rufaa Ikulu, Chamwino mkoani Dodoma.

Rais Samia amesema “sasa utajiuliza kuna nini hapo. Hiyo kesi moja ya Lindi, Mkuu wa Mkoa akasema sikubali niambiwe nakiuka maamuzi ya mahakama lakini sikubali hili ni kosa. Sasa inaleta mushkeli wa vyombo viwili ndani ya Serikali,” 

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema huenda kuna maamuzi mengi yanafanyika katika mahakama za chini ambayo anadhani yanakuwa hayajatolewa kwa kuzingatia haki.

“Sasa hilo ni moja hatujui yako mangapi huko chini, lakini ukisikiliza kesi za wanaoingia kwenye hifadhi, Tanapa wapi zikifika mahakamani mh! Mambo magumu kidogo, wafugaji ile pesa inafanya kazi kweli. Kwa hiyo naomba mtupie macho huko chini ili wananchi wa kawaida wapate haki zao,” amesisitiza Rais Samia. 


Soma zaidi: 


Mkasa ulivyokuwa

Kwa mujibu wa Afisa Uhifadhi wa hifadhi ya Nyerere Julius Shija Januari 29,2023 askari wa kituo cha Liwale waliwakamata jumla ya ng’ombe 547 na punda 11 wakiwa  ndani ya Hifadhi ya Nyerere. 

Pia walikamatwa watuhumiwa wawili wakichunga mifugo hiyo ndani ya hifadhi waliojulikana kwa majina John Lucas na Simbi Masingija.

Baada ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kufuata taratibu za polisi, Februari 1 mwaka huu, shauri la mashtaka lilifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Liwale. Shauri hilo lilisikilizwa na mashahidi wawili walitoa ushahidi kisha mahakama ilihamia eneo la tukio (ndani ya hifadhi) kwa ajili ya kupokea kielelezo ambacho ni ng’ombe 547 na punda 11. 

Pamoja na kujiridhisha kwa kutembelea eneo la tukio na kuwasikiliza mashahidi, baada ya kuwapa nafasi ya kujitetea, Februari 10 mahakama iliwaachia huru watuhumiwa na kuamriwa warudishiwe mifugo yao kutokana na ushahidi upande wa Serikali kutojitosheleza. 

Hata hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Telack alisikitishwa na maamuzi ya Mahakama ya Wilaya kumuachia huru mmiliki huyo wa mifugo ambapo baada ya hukumu hiyo Serikali iliahidi kukata rufaa. 

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Wabunge waliokwenda Morocco bila kibali kikaangoni , utoro ukiibuliwa bungeni

Nukta TV

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Mfahamu Leonard Mususa Alama ya Ungozi iliyoacha majonzi kwa 'MACEOs' Tanzania

Nukta TV

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Bei za mafuta mwezi Juni hizi hapa, dizeli ikipaa kwa Sh85

Nukta TV